Askofu Gwajima ameonya waumini wake kwamba chanjo ya corona ni hatari, na kusisitiza hakuna haja ya kuchanja watanzania kwa sababu Tanzania hakuna corona. Askofu Gwajima amesema kilichopo hivi sasa ni hofu ya corona ambayo ina nguvu kuliko corona yenyewe.
Askofu Gwajima amesema kwamba chanjo ya corona inageuza mwanadamu kuwa mwandamu wa aina nyingine, kwamba chanjo hiyo inakubadilisha uwezo wa kufikiri, hisia na maamuzi.
Amesema kwamba Tanzania itakapotengwa kwa kugoma kuchanjwa ndio itakuwa mwanzo wa Tanzania kuwa na uchumi mkubwa duniani, amesema hiyo itasababishwa na wazungu mabilionea wenye akili watakogundua kuwa kuna taifa moja pekee ambalo halichanji watu wake na hivyo wazungu hao mabilionea watakuja na kuanza maisha yao nchini Tanzania na kuhamishia biashara zao kubwa nchini Tanzania.
Amesisitiza kuwa alipata maono miaka 25 iliyopita kuwa wazungu wengi watakuwa ubalozi wa Tanzania wakifurika kuomba visa ya kuja kuishi Tanzania.
Askofu Gwajima amesali na kuomba serikali na viongozi wa Tanzania wagome kuchanja watu kwa maana ndio itakuwa mwanzo wa Tanzania kuwa na uchumi imara.