Badala ya kuwa mahali pa sala, maombezi na faraja kwa waumini, madhabahu ya Askofu Josephat Gwajima yamegeuka kuwa jukwaa la mashambulizi ya wazi dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan, yakisambaza chuki, hofu na hisia kali zisizo na mashiko ya kiroho.
Katika ibada ya Jumapili iliyopita, Gwajima alisikika akisema kwa kujiamini: “Niliwahi kumwambia Rais Samia nikiwa Ikulu kuwa, mtu mwenye hofu ya kupinduliwa tayari amepinduliwa.”
Kauli hii haikutoa maarifa ya kiroho wala hamasa ya kiimani, bali ilionekana wazi kuwa ni dongo la kisiasa lililolenga kuipaka tope Serikali ya Awamu ya Sita mbele ya hadhira ya waumini wake.
Badala ya kuhubiri matumaini, mshikamano wa kitaifa na sala kwa ajili ya maendeleo ya nchi, Gwajima ameendelea kugeuza mimbari kuwa uwanja wa kutupia vijembe, kusambaza jazba na kupandikiza dhana potofu miongoni mwa wananchi.
Katika kauli nyingine isiyopimika kwa mizani ya hekima ya kiroho, alisema: “Wapo wanaodhani ninaogopa kutekwa, lakini hata wakiniteka watakuwa wamechelewa.” Hii si lugha ya kiimani bali ni kejeli inayojenga mazingira ya taharuki na hofu ya kutungwa. Ni sauti ya mtu anayeona yuko juu ya taasisi, sheria na hata ukweli wa hali halisi.
Inashangaza kuona Gwajima akiwa kimya kabisa kwenye mambo muhimu yanayogusa maisha ya kila siku ya Watanzania kama mfumuko wa bei duniani, ajira kwa vijana, huduma za afya kwa mama na mtoto au mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Lakini kila mara linapokuja suala la kumshambulia Rais Samia huibuka na maneno yenye ujasiri wa ajabu, hali inayoibua maswali kuhusu malengo halisi ya hotuba zake.
Kwa miaka sasa Gwajima ameacha majukumu ya kiroho aliyokabidhiwa. Amechagua kuwa mwanasiasa wa majukwaa ya mitandaoni anayejificha nyuma ya joho la askofu huku akihubiri hofu, fitna na mivurugano.
Amebakiza sauti ya uchochezi na kiburi cha kisiasa badala ya uzito wa kiroho unaopaswa kumwongoza kiongozi wa dini.