A
Anonymous
Guest
Mume ambaye alikuwa mfanyabiashara wa kununua na kuuza vitu vilivyotumika, aliondoka nyumbani saa saba mchana na hakurudi tena. Awali familia haikuwa na wasiwasi kwa kuwa iliamini alikuwa ameenda katika shughuli zake za biashara, hali ilibadilika baada ya kufika usiku bila kurejea nyumbani na simu zake mbili zenye laini tatu kutopatikana.
Ilipofika saa mbili usiku wakaona si kawaida yake, simu haikuwa ikipatikana. Siku iliyofuata ndugu wakaanza kumsaka mume katika vituo vya polisi na hospitali, ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na mochwari lakini kote hawakupata taarifa kuhusu alipo.
Ikabidi mke atoe taarifa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, ambako alipewa namba ya kumbukumbu ya taarifa (RB) na kuacha mawasiliano yake, baada ya siku kadhaa bila kupata taarifa, alirejea kituoni na kueleza mashaka yake kuhusu dereva wa bodaboda aliyempigia simu mume wake kabla ya kuondoka nyumbani.
Dereva huyo alikamatwa na inadaiwa wakiwa mbele ya Wanausalama boda huyo akaeleza kuwa Ally Nanjasye alikuwa ametekwa na kwamba yeye ndiye aliyemshawishi kwenda eneo ambako alichukuliwa na watu waliokuwa kwenye gari aina ya Subaru.
Inadaiwa kuwa Mariam aliporejea kituoni siku iliyofuata hakumkuta yule boda ambaye alikuwa mtu wa mwisho kuwasiliana na mumewe.
Inadaiwa kuwa kuna mwanausalama alimwambia mke kuwa mumewe ametekwa na 'mtu mkubwa', ndiyo maana suala lake limekuwa gumu kuwa na mwendelezo, inawezekana ikawa ngumu kurejea moja kwa moja au hivi karibuni.
Mke ameamua kurejea nyumbani kuishi akiwa na hofu kutokana na mazingira yalivyo, akiwa ameamua kukaa kimya hajui cha kufanya.
Mume ni kada wa CHADEMA
Kuhusu kama mambo ya siasa yanahusika, Ally Nanjasye hakuwa kiongozi wa chama cha siasa ila alikuwa ni kada wa CHADEMA kama alivyo mkewe.
Ndugu wa mume waliotoka Nachingwea walifika Dar es Salaam na kushiriki katika ufuatiliaji, kabla ya kurejea walikotoka baada ya kukosa taarifa za mahali alipo ndugu yao.
Kiongozi wake naye ameingia mitini
Kuna kipindi mke alikuwa akipata ushirikiano kutoka kwa kiongozi wake mmoja ngazi ya kata alikuwa anampa msaada, akawa anaenda hadi kituo cha polisi lakini baadaye naye akaingia mitini, simu hapokei wala hatoi ushirikiano, sijui nini kimetokea au haijulikani kaambiwa nini kiongozi huyo.
Watoto watatu waathirika
Kabla ya kupotea Ally Nanjasye amebahatika kuwa na watoto watatu wameanza kupata changamoto ya kuendelea na masomo, hata malipo ya kodi yaliyofanyika yalikuwa ya mwisho na kwamba wanafikiria kurejea kijijini Korogwe, Tanga.