Source: Habari leo
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia CCM, Emmanuel Luhahula ameonja joto ya jiwe baada ya wananchi kumkataa mbele ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa kampeni.
Luhahula anayeomba tena ridhaa ya kuongoza jimbo hilo la wilayani Bukombe mkoani Shinyanga, alijikuta akizungumza huku akizomewa kwa kupigiwa miluzi na wananchi juzi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Igulwa Mjini Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Shinyanga.
Kwanza alikutwa na dhahama hiyo wakati akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2005-2010 na hata alipotambulishwa kwa wananchi hao na Rais Kikwete, bado hakukubalika.
Kwa kusoma hali ilivyokuwa uwanjani hapo, Rais Kikwete aliwauliza wananchi hao kama wanamkubali awe Rais wao, walimjibu "Ndiyo", lakini wakasema "Hapana" kwa Luhahula aliyeongoza katika kura za maoni ndani ya CCM.
Hata hivyo, mshindi wa pili katika kura hizo za Agosti mosi, mwaka huu, Profesa Kulikoyela Kaige, aliihama CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ndiye mgombea wao wa ubunge.
Wakati wote akisoma utekelezaji huo wa Ilani ya CCM, Luhahula alikumbana na kelele za wananchi hao zilizotokana na kuzomea na kupiga miluzi huku wakionesha ishara ya vidole viwili hewani, alama inayotumiwa na Chadema.
Hata Luhahula alipopewa fursa ya kuwasalimia wananchi baada ya Rais Kikwete kumaliza kuzungumza, hali ilikuwa ile ile ya kumkataa mbunge huyo aliyeingia madarakani mwaka 2005.
Alitumia muda huo kuwatambia wananchi hao waliomkataa kwa kusema, "najua wanaoninyooshea mikono, watakuwa wa pili, Luhahula atakuwa wa kwanza katika uchaguzi.
Ushindi wa CCM ni lazima." Awali, katika hotuba yake, Rais Kikwete aliwaponda wanachama wa CCM ambao baadhi yao baada ya kushindwa kura za maoni hukimbilia vyama vya upinzani, akiwafanan isha na wanafiki.
"Maisha yako yote uko CCM, siku ulipokosa uteuzi unakuwa kada wa chama kingine, unafiki mtupu," alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa CCM bado ni chama imara kuliko vya upinzani.
Alifafanua kuwa CCM haisumbuliwi na kuwepo kwa vyama vya upinzani, kwa sababu ni Serikali ya CCM iliyoamua kupitisha uamuzi wa kuwa na mfumo wa vyama vingi nchini, licha ya asilimia 80 ya Watanzania kukataa.
"Hawa waliopo leo wasingekuwepo kama siyo CCM, serikali inayoheshimu haki za raia kuchagua chama unachokitaka. Uhuru huo ni CCM ilitoa. "Hiyo ni hekima ya CCM.
Asilimia 80 wana imani na Chama Cha Mapinduzi. Asilimia 20 ndio wapinzani.
Wala msihangaike, hilo halitusumbui, tuliamua wenyewe muwepo, kwa hiyo mkiwepo, haitushangazi," alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Bukombe mkutanoni hapo.
Hata hivyo, aliwaomba kuendesha siasa bila fujo akisema, "hata kama una mbunge wako, kwa sasa Mbunge ni Luhahula, na tarehe 31 atashinda na kitakachomfanya ashinde ni mafanikio aliyoyaeleza hapa."
"Tumeanza mipango ya kuhakikisha umeme unafika Bukombe, mchakato wake unaanza Novemba, hakuna wasiwasi.
Tupeni miaka mitano tufanye vizuri zaidi. Wananchi wa Bukombe wasihangaike, hivi vyama vingine vinapita," alisema mgombea huyo wa urais wa CCM.
Kwa mujibu wa duru za siasa wilayani Bukombe, kuna mgawanyiko miongoni mwa wananchi kuhusu wagombea ubunge uliojikita katika suala la ukabila miongoni mwa wagombea hao wawili; Luhahula na Profesa Kaige.
Salma Kikwete aifananisha CCM na mwembe Na Mwandishi Wetu MWEYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amekifananisha Chama Cha Mapinduzi na mwembe ambao hurushiwa mawe kutokana na matunda yake.
Amesema wapinzani wanaisema CCM kwa sababu imefanya mambo mazuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa baada ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2005-2010.
"Ukiona wapinzani wanaisema sana CCM, ujue imefanya mambo mazuri, ni sawa na mwembe wenye matunda hupigwa mawe, kwani umeshaona mwembe usio na matunda ukipigwa mawe?" Alihoji.
Mama Salma alisema hayo jana na juzi kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika Mkoa wa Mtwara.
Kuhusu uchumi, alisema uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni ukombozi kwa wakulima dhidi ya walanguzi.
Taarifa iliyowasilishwa kwake ilieleza kwamba, uuzaji korosho kwa mfumo huo umewanufaisha wakulima ambapo hulipwa malipo kwa awamu mbili hadi tatu kulingana na bei ya soko.
Ilieleza kwamba, wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani, kilo moja ya korosho ilikuwa ikiuzwa kwa kati ya Sh 150 hadi Sh 300 na kwa sasa ni Sh 800 hadi Sh 1,000 baada ya uanzishwaji wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Mama Salma alisema wanaoupinga mfumo huo, wanataka kuendelea kujitajirisha kwa jasho la wakulima kama ilivyokuwa huko nyuma.
"Msidanganyike, uuzaji wa mazao kwa stakabadhi ya mazao ghalani ni ukombozi kwa wakulima, na Serikali ya CCM inawapenda haiwezi kuwadhulumu ndio maana inasisitiza na kusimamia mazao kuuzwa kwa vyama vya ushirika," alisema na kupigiwa makofi na vigelegele.