Nifah
JF-Expert Member
- Feb 12, 2014
- 34,020
- 79,098
Ndugu wanajukwaa, leo familia ya Manji wamehitimisha msiba wa mpendwa wetu Yusuph Manji uliotokea Jumamosi ya wiki iliyopita kwa Dua maalumu iliyosomwa na viongozi mbalimbali wa kidini wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir katika viwanja vya Karimjee.
Katika jambo lililowashangaza wengi ni ratiba rasmi ya dua hiyo iliyotolewa na familia hiyo ya Manji kutokuonekana kwa Klabu ya Yanga ambayo marehemu aliifadhili kwa miaka mingi!
Ratiba imeweka wazi kwamba atakuwepo mwakilishi kutokea tasnia ya mpira na sio kama ambavyo ilipaswa kuwepo Yanga, mwakilishi kwenye soka anaweza kuwepo yeyote hata kutokea kwa watani zetu, Simba.
Yanga, tumefikaje hapa?
Hadi familia kufikia hatua hii lawama zote wanabeba uongozi wa Yanga chini ya Eng. Hersi. Tokea kutangazwa kwa kifo cha Manji macho yetu tulio wengi yaliigeukia Yanga, kinyume na matarajio ya tulio wengi Yanga walitoa pole kwa familia pekee kisha wakaendelea na mambo mengine bila kuupa uzito msiba huu wa kiongozi muhimu zaidi kutokea kwenye historia ya mpira nchi hii.
Hersi na wenzio, mnajua kwamba hadi leo hii hakuna mwekezaji yeyote aliyefadhili klabu yoyote kwa pesa zake mwenyewe bila nia ya kujineemesha kibiashara zaidi ya Manji?
Mnajua kwamba hadi sasa ufadhili wenu GSM hapo Yanga haujafikia hata nusu tu ya aliyoyafanya Manji kwa Yanga bila shinikizo wala mabandiko ya bidhaa zake kwa kutumia nembo ya Yanga?
Kwanini mmemtenga Manji kiasi hiki? Mnafikiri yote haya aliyoyafanya mtatusahaulisha kwa kuupuza msiba wake? Manji aliwakosea nini hadi kuvunjiwa heshima aliyoijenga kwa dhati hapo Yanga? Kweli Manji anafariki hadi kuzikwa na hadi leo hii dua hamjihusishi kwa lolote?
Mashabiki wenzangu tumemwamngusha Manji!
Tukiachana na GSM ambao wana maslahi yao binafsi tofauti na sisi wapenzi na mashabiki wa Yanga, pia tunabeba lawama.
Kwanini tulishindwa kuushinikiza uongozi kumuenzi Manji baada ya kuona wameupuuza msiba wa Mwananchi mwenzetu? Leo hii tumesahau alikotutoa Manji? Popote linapotajwa jina la Manji Yanga haikosi kuwepo, kwanini tumeshindwa kumpa heshima? Tumekosa fadhila kiasi hiki kwa mtu aliyetutoa kwenye mabakuli na kutupa heshima tulipokuwa dhalili?
Nimeumizwa sana, lakini nimekatishwa tamaa na uongozi niliouona makini na kuusifu mara nyingi waziwazi chini ya Hersi. Huu ni udhalimu na hakika Manji hatotusamehe!
Nikitokea hapa Karimjee, ndimi mnazi wa Yanga niliyeumizwa…
Nifah