Baadhi ya matukio mazito ya kihistoria kitaifa kuanza kudharauliwa na mamlaka husika

Baadhi ya matukio mazito ya kihistoria kitaifa kuanza kudharauliwa na mamlaka husika

The introvert

JF-Expert Member
Joined
Sep 15, 2023
Posts
1,508
Reaction score
3,136
Anaandika Michael Mbiti

BARUA YA WAZI KWA VIONGOZI WETU.
291261.jpg

Historia Inafutika Tanzania, Tunaweka Wapi Utu Wetu?

Ndugu Viongozi Tuliowapa Dhamana,

Leo ni Mei 21. Siku ambayo miaka ya nyuma (1996), Taifa letu lilikumbwa na simanzi kubwa baada ya meli ya abiria ya MV Bukoba kuzama katika Ziwa Victoria.

Nasikitika kuona kuwa, siku baada ya siku, kumbukumbu hii muhimu inaenda ikifutika polepole bila ninyi wasimamizi wa dhamana yetu kusituka. Historia hii inapotea kwa sababu moja tu: Viongozi mmetupa desturi ya kuiishi na kuienzi historia ya maumivu ya watu wenu.

Hivi mnasahau ukubwa wa msiba huu?

Meli ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 430 tu, lakini ulafi na uzembe ulisababisha ipakizwe zaidi ya watu 1,000.

Kumbukumbu rasmi za serikali zinasimama kwenye vifo vya Watanzania 894, huku kukiwa na manusura 114 tu. Huu unatajwa kuwa miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya majini katika Ukanda wa Kusini mwa Ikweta.

Miongoni mwa waliopotea, walikuwemo watoto wa shule wapatao 40 waliokuwa wanarudi nyumbani baada ya kumaliza mitihani yao kule Bukoba.

Kama ingekuwa ni nchi za wenzetu wanaothamini utu na uzalendo wa vitendo:

Vyombo vya habari vyote nchini leo vingekuwa vinapiga nyimbo za maombolezo na kusoma historia ya vifo hivi vya kinyama ili kutoa mafunzo kwa kizazi cha sasa.

Bendera ya Taifa ingepepea nusu mlingoti nchi nzima, huku serikali ikiwa kiongozi namba moja wa maombolezo haya, badala ya kuacha maadhimisho haya kuwa ya kimya na ya mkoa mmoja tu.

Tuna kizazi kipya cha akina Ever na Ellen. Hawa walizaliwa baada ya tukio hili kutokea. Kama msipoishi hii historia na kuifundisha, watajuaje thamani ya usalama wa usafiri wa majini? Watajuaje maumivu ya Taifa lao? Uzalendo gani mnaouhubiri majukwaani ikiwa hamtaki kuiishi historia iliyotia simanzi Taifa zima?

Tujifunze Kutoka Japan.
Wajapani hadi leo wanawaenzi na kuwakumbuka raia wenzao waliouawa kwa mabomu ya nyuklia kule Hiroshima na Nagasaki. Siku hiyo ikifika, utawaona viongozi na wananchi wakinamisha nyuso zao, wakitokwa na machozi huku wakisoma historia ile. Kama Wajapani wasingekuwa wanaishi historia yao, mimi na ninyi tusingejua lolote kuhusu madhara ya mabomu yale. Wao walichagua kutofuta historia yao.

Makosa ya Kimkakati Katika Kumbukumbu Zetu.
Huu ukosefu wa utaratibu thabiti wa kihistoria haupo kwenye MV Bukoba pekee. Je, mmeshasahau maafa ya Ajali ya Treni ya Igandu kule Dodoma (Juni 24, 2002)?

Pale tulipoteza ndugu zetu 281 ndani ya siku moja na kuacha majeruhi mamia. Leo hii hata makaburi yao ya halaiki kule Miyuji yanasahaulika.

Na nini mnafanya kuhusu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere?

Hivi hamuoni kama ni kosa na chukizo kubwa kuchanganya siku ya maombolezo ya kifo cha Muasisi wa Taifa hili (Oktoba 14) na shamrashamra, vifijo na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru? Maombolezo yanageuka kuwa sherehe! Tunajifunza nini hapo?

Wito Wangu (My Take)
Nawaomba ninyi viongozi mliopo kwenye dhamana:

Tufundisheni kupendana kwa vitendo kwa kujali utu wa waliotutoka.

Tufundisheni kuwa pamoja wakati wa furaha na hata kwenye kumbukumbu ya majanga yetu.

Tufundisheni kuiishi historia ya matukio yaliyoliza Taifa, ili tujifunze kutokurudia makosa ya uzembe na ulafi wa kukanyaga sheria za usalama.

Utu uwekwe mbele ya siasa na sherehe. Historia yetu ndio utambulisho wetu.

Mungu Ibariki Afrika.
Mungu Ibariki Tanzania.

Wenu Katika Kulinda Historia,

Cc:Michael Mbiti

View: https://www.facebook.com/1642392426/posts/10229015054314696/?app=fbl

Michael S. Mbiti Jr.

Mtunza Misingi kutoka Gamboshi.
 
Back
Top Bottom