KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), imeipoka
Yanga pointi tatu baada ya
kumtumia beki Nadir Haroub
'Cannavaro' katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal
Union. Hiyo ina maana kuwa Yanga
ambayo ilishinda bao 1-0 na
kufikisha pointi 46 sasa
inashuka mpaka pointi 43,
lakini inabaki nafasi ya tatu
huku Coastal Union iliyokuwa na pointi 29 sasa inakuwa na
pointi 32 na kushika nafasi ya
tano. Kamati hiyo ilikutana jana
Jumatatu usiku chini ya
Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Ligi ya TFF, Said
Mohamed, ambaye aliandika
barua ya kujiuzulu, lakini akakataliwa na Rais wa TFF,
Leodegar Tenga. Katika kikao hicho ilibainika
kuwa Yanga ilifanya kosa
kumtumia Cannavaro kwa
sababu alitakiwa kukosa
mechi tatu kutokana na
kupewa kadi nyekundu baada ya kumpiga mwamuzi, Israel
Nkongo. Kamati hiyo ilifikia uamuzi huo
baada ya kupitia ripoti ya
mwamuzi Nkongo, ambaye
aliandika kuwa alimpa kadi
Cannavaro kutokana na
kupigana uwanjani. Cannavaro alichezeshwa na
Yanga katika mechi hiyo baada
ya adhabu yake ya kutocheza
mechi sita kusimamishwa na
Kamati ya Nidhamu na
Usuluhishi ya TFF chini ya Alfred Tibaigana. Hata hivyo, Coastal Union,
ilikata rufaa kupinga
kuchezeshwa kwa Cannavaro. Cannavaro alitakiwa kukosa
michezo mitatu dhidi ya
African Lyon, Villa Squad na
Coastal Union kulingana na
adhabu ya kadi aliyoonyeshwa. Kamati ya Ligi ya TFF hivi
karibuni iliwafungia Cannavaro
(mechi sita), Stephano
Mwasika (mwaka mmoja),
Jerry Tegete(miezi sita),
Omega Seme na Nurdin Bakari mechi tatu kila mmoja kwa
kosa la kumpiga mwamuzi
Israel Nkongo katika pambano
dhidi ya Azam FC. Tibaigana alitumia Kanuni ya
129 ya Kanuni za Adhabu za
FIFA, ambayo inaipa kamati
yake mamlaka ya kusitisha
utekelezaji wa adhabu yoyote
ile pale anapoona kwamba ukiukwaji unaolalamikiwa
hautaweza kupatiwa ufumbuzi
wa haraka, isipokuwa uamuzi
wa refarii. Yanga inaonekana walifuata
kanuni ya 25 kifungu (b)
ambayo inasema; mchezaji
atakayetolewa nje kwa kadi
nyekundu ya moja kwa moja
(straight red) atakosa michezo miwili. Lakini kifungu (f) kipengele
cha iii kinasema mchezaji
atakayepewa kadi nyekundu
kwa kupiga au kupigana
atakosa mechi tatu. Lakini jana Jumatatu mchana
Mwanaspoti ilipomtafuta
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi,
Wales Kalia kabla ya uamuzi
huo wa usiku, kuhusu
mkanganyiko huo alisema: "Kama kanuni zinavyosema
mchezaji atakayetolewa nje
kwa kadi nyekundu baada
kupata kadi mbili za njano
katika mchezo wa ligi
hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata wa timu
yake. "Mchezaji atakayetolewa nje
kwa kadi nyekundu ya moja
kwa moja (straight red)
atakosa michezo miwili,
mchezaji atakayeonywa kwa
kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza
mchezo mmoja unaofuata na
mchezaji atakayeonyeshwa
kadi nyekundu ya moja kwa
moja( straight red) kwa kosa la
kupigana uwanjani, kupiga kiwiko au kuleta fujo yoyote
uwanjani atakosa mechi tatu
na faini ya Sh 500,000. " Sasa kulingana na ripoti ya
mwamuzi na kamisaa
iliyoletwa kwetu, ilionyesha
Cannavaro alipewa kadi
nyekundu kwa kosa la kuleta
fujo uwanjani hivyo anapaswa kukosa mechi tatu na faini ya
Sh 500,000 hiyo ni adhabu
kulingana na kanuni za ligi,
lakini baadaye Kamati yetu
ilipokaa ndipo tukamuongezea
adhabu nyingine ya kukosa mechi tatu zaidi kwa zile fujo
zilizotokea kwa hiyo
ikatangazwa kuwa atakosa
mechi sita. "Lakini Mwenyekiti wa Kamati
ya Nidhamu na Usuluhishi,
Alfred Tibaigana,
alizisimamisha adhabu za
kifungo cha wachezaji hao
lakini akasema adhabu za kadi uwanjani zinabaki pale pale,
hivyo Cannavaro alistahili
kukosa mechi tatu." Hivyo kanuni ya 25 kifungu f
kipengele cha (viii) ndicho
kinachoitia matatani Yanga
ambacho kinasema: "Timu
yoyote itakayomchezesha
mchezaji aliye chini ya adhabu kwa mujibu wa kanuni hii
itapoteza mchezo huo na timu
pinzani itapewa ushindi."