SoC01 Bado tunafanya maonesho katika kuwajengea vijana ujuzi wa TEHAMA

SoC01 Bado tunafanya maonesho katika kuwajengea vijana ujuzi wa TEHAMA

Stories of Change - 2021 Competition

cilla

JF-Expert Member
Joined
Jul 15, 2011
Posts
372
Reaction score
299
BADO TUNAFANYA MAONESHO KATIKA KUWAJENGEA VIJANA UJUZI WA TEHAMA

Miaka michache nyuma kabla ya kuingia kwenye karne ya 21 kauli mbiu ya Karne ya 21 kuwa ni karne ya sayansi na teknolojia ilitamalaki katika midomo ya watu wengi sana ulimwenguni na sisi kama nchi watawala walihubiri sana juu ya sayansi na teknolojia na kuhimiza vijana kujikita kwenye sayansi ili kuendana na mabadiliko ya dunia.

Baada ya kuingia katika karne ya 21 serikali imefanya jitihada za namna nyingi za kupiga hatua kwenye kuongeza matumizi ya teknolojia na kuzalisha wasomi mbalimbali katika nyanja ya Tehama.Pamoja na nia nzuri ya serikali bado kuna mapungufu mengi katika namna ya kuinua wataalamu wengi wabobezi katika Tehama.

Zawadi na misaada ya computer mashuleni .​

Tumekuwa tukishuhudia zawadi nyingi za waheshimiwa wabunge mawaziri na serikali katika kuzisaidia shule na vyuo kwa kuzipatia kupeleka computer mashuleni na katika vyuo mbalimbali nchini jambo ambalo si baya kabisa lakini mimi naliita ni maonesho.Kwanini tunaita ni maonesho?Nayaita ni maonesho kwasababu zifuatazo:

Computer si vitabu.Kutoa computer peke yake haitoshi kuonyesha kuwa tupo serious na kukuza Tehama mashuleni kwasababu computer inahitaji walimu ,lab na wasimamizi wa lab.Baadhi ya shule na vyuo vilivyowahi kupewa msaada wa computer ukizitembelea utashangaa computer zilivyogeuka kuwa takataka .Hakuna utunzaji ,hakuna mwalimu wakufundisha computer na sehemu zingine hakuna hata jengo maalumu (lab) ya computer kwahiyo aidha zipo stoo au kwenye darasa ambalo haliko katika hali nzuri .Mbaya zaidi kompyuta hizi nyingi ni matoleo ya zamani ambayo kwasasa zinaweza zisifae sana kutokana na teknolojia iliyoboreshwa kwenye software na program endeshi. Pili kwasababu yakukosekana kwa wasimamizi (lab technician) kompyuta nyingi ni mbovu au aidha vifaa vimeibiwa na wa janja wachache kwasababu hakuna mtu anayewajibika moja kwa moja katika kusimamia na kutunza kompyuta hizo.Baadhi ya vyuo hapa Tanzania vina mpaka Super computer lakini zinaozea stoo mpaka unajiuliza zililetwa za nini kama hazikuwa na shughuli ya kufanya? Na baadhi ya kompyuta hizo zilikuja kutokana na maombi ya viongozi wetu walipoenda katika ziara za nchi za nje.

Kwa mtindo huu wakufanya ugawaji wa kompyuta bila mikakati yenye nia ya kweli, basi tutakuwa tunaigiza tu katika kukuza na kuibua wabobezi wa tahama nchini.Kompyuta si vitabu .

Maandalizi ya walimu​

Walimu hawajaandaliwa kikamilifu katika umahiri ili kwendana na teknolojia ya Tehama.Hii ndio sababu hata kompyuta mashuleni hazionekani kama ni nyenzo ya kufundishia na ujifunzaji kwasababu walimu wenyewe hawaja hamasika aidha kwasababu hawajaandaliwa vizuri, hawakujifunza kabisa au walijifunza vyuoni kwa nadharia nyingi bila vitendo.

Tuweke uzito katika kuwaandaa walimu wa Tehama pekee wakafanye kazi ya kutunza Lab za kompyuta na kufundisha tofauti na tunavyofanya sasa kubebesha mwalimu masomo mengi chuoni likiwepo somo la kompyuta kwa kigezo cha kwenda kufidia upungufu wa walimu mashuleni.

Isichukuliwe kwamba kwasababu mtu anaenda kuwa mwalimu basi nadharia nyingi na uelewa wa juu juu unaweza kumfanya kuwa mwalimu mzuri.Serikali ifikiri sasa kuwapeleka watu kusomea ualimu wa Tehama wakiwa tayari wana astashahada ya kompyuta kwa shule za msingi na sekondari mwenye cheti cha stashahada ya kompyuta.Na ikiwa wizara itahitaji kudahili kijana ambaye ndio kwanza kamaliza elimu ya kidato cha nne au sita na hana cheti cha Tehama au kompyuta basi ni heri akapita kwenye vyuo vinavyofundisha Tehama angalau miaka 2 kabla ya kwenda kwenye masomo ya ualimu au iwe kinyume chake kwamba mwalimu ili awe na sifa ya kufundisha kompyuta basi baada ya kusoma ualimu aende akasomo kozi ya kompyuta angalau miaka 2 na kuendelea.Vinginevyo tutakuwa tunajifariji kwamba tunasomo la Tehama na walimu wa Tehama kumbe tu wasindikizaji na juhudi zote kuwa maonesho kwamba na sisi hatuko nyuma.

Uwepo wa somo la kompyuta​

Wizara ya elimu kwa nia njema kabisa iliamua kuanzisha somo la TEHAMA kwa shule za msingi na sekondari nchini.Changamoto ni kuwa somo hili limekuwa likikimbiwa na wanafunzi pamoja na shule.

Sababu kubwa ya shule nyingi za sekondari hasa za binafsi kuachana na somo hili ni kutokana na matokeo ya wanafunzi wao kutokuwa mazuri.

Wanafunzi pia kwa upande wao wanadai hili somo halieleweki lina misamiati mingi isiyoeleweka kiurahis kwao.Wanafunzi hawaamasiki kabisa kusoma somo la kompyuta japo wengi wao wanapenda kujua kompyuta na kuitumia.

Serikali iangalie upya mtaala wa somo la kompyuta na ishirikishe wadau mbalimbali na kuangalia wenzetu wanalifundisha vipi katika nchi zilizoendelea.Kwasasa somo la TEHAMA ni nadharia nyingi bila vitendo na uhalisia. Kiukweli somo la Tehama bila vitendo linachosha na kukinaisha.

Kwa maoni yangu Ingefaa sana kama wanafunzi wa shule ya msingi wajifunza program za msingi ili kuwafanya kuwa familia na kompyuta kuliko hivi sasa ambapo mwanafunzi hawezi kufanya task hata moja kwenye kompyuta au hajawahi kuona kabisa kompyuta. Kitendo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza kusoma somo la Tehama na ndani yake anajifunza kuwasha redio na simu hii haiko sawa huku ni kuua vipaji .

Siku hizi kuna program za watoto zinazoweza kumfanya mtoto kuwa na msingi mzuri wa kompyuta kuliko kumjaza mtoto nadharia .Kuna program kama scratch, kid robotics, code monkey,minecraft,codekid nk ni maarufu duniani kwa kuwafundishia watoto programing kuanzia miaka saba na kuendelea.Lakini pia zipo program za kucheza maarufu kama simultation games ambazo zinasaidia mtoto kujenga uwezo wa kufikiri kwa haraka pia zinamsaidia katika kufanya task mbalimbali za kimasomo na katika Tehama pia.

Kama kweli tupo serious kuwekeza kwenye Tehama tulipaswa kutoa wahitimu wa darasa la saba wenye uwezo kivitendo angalau wakutumia program za kompyuta kama Microsoft word,excel, publisher na ujuzi wa kuchapa(typing). Kwa sekondari tulipaswa kutoa wahitimu wenye ujuzi wa ku code au kuandika program fupi kama C++, HTML, kutengeneza kadi,kutuma na kupokea email,internet nk.

Kama taifa tuondokane na nadharia nyingi tuwekeze kwenye vitendo zaidi.Mwanafunzi wa shule ya msingi ni vizuri angefundishwa Tehama kwa vitendo zaidi na sekondari ndipo asome kwanadharia na vitendo kwa pamoja. Mama wa elimu zote ni vitendo,Tusisubirie mwanafunzi anamaliza kidato cha sita hajui hata kutuma email au kutuma maombi yake ya chuo kwa njia ya mfumo.Tusisubirie mwanafunzi afike chuo kikuu ndio tuanze kumfundisha namna ya kushika mouse au kuwasha kompyuta wakati hicho ni kitu kidogo alipaswa kukijua akiwa shule ya msingi.

Tusiridhike kwasababu tu tuna somo na mtaala wa Tehama tuangalie ufanisi wake na athari chanya zake kwa wanafunzi.Bila mikakati ya dhati na kuwekeza TEHAMA kwa njia ya vitendo kwa vijana na watoto,hatutaweza kuendana na karne hii ya sayansi na teknolojia.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom