RIWAYA; BAHARIA
NA; BAHATI MWAMBA
SIMU; 0758573660
SEHEMU YA SITA
Vedi nae akachungulia.
Lauhaula!!!
Alijiona yeye mwenyewe akiwa ametulia tuli ndani ya jokofu. Hata mavazi aliokuwa amevaa usiku wa sherehe ile, hadi mtindo wa nywele ulikuwa ni ule ule aliokuwa ameuweka siku ile.
Vedi akaruka nyuma huku vidole vyake vikiwa vimekimbilia kuziba mdomo ili asipige kelele.
Alijiona yeye mwenyewe akiwa ndani ya jokofu la kuhifadhia maiti.
Mlinzi nae alikuwa hoi akitetemeka.
Mara mlango ukasukumwa na wakaingia wale watu watatu aliowaona Vedi wakiwa wameongozana na Dr. Masimba.
Vedi akagwaya!!.
Lilikuwa ni tukio ambalo liliwastua Vedi na mlinzi aliempeleka mule.
Vedi alibaki akiwa ameganda kama sanamu asijue cha kufanya.
Yule mtu ambae awali alimuona ndani ya meli;hakuhangaika kutazama aliowakuta mle ndani badala yake moja kwa moja alielekea kwenye jokofu lililokuwa wazi ambalo lilibeba maiti ya mtu aliefanana sawa na Vedi. Wale jamaa wengine nao ambao walikuwa sambamba na mtu yule, walielekea jokofu lile.
Dr. Masimba alitoa taarifa bila kuwazatazama aliowakuta mle na wengine pia hawakutazama na ni kama walifanya makusudi kabisa kufanya vile.
Vedi hakutaka kusubiri, haraka akajitosa mlangoni na kutoka kwa kasi na alipofika nje, haraka akaondoka eneo lile bila hata kutazama nyuma.
Wakati anatoka kabisa nje ya lango kuu la hospitali ile ya mwananyamala,kuna kitu kiliingia kichwani mwake.
“Kwanini nieondoke bila kuwafahamu watu hawa?” alijiuliza na kusimama kwenye eneo ambalo watu walikuwa wanaingia na kutoka kwa wingi.
Akatulia tu kama ambae hana kazi ya kufanya aendako.
Dakika ishirini badae, aliona wale watu wakitoka na lile gari lao walilokuwa wameegemea karibu na ofisi za Dr Masimba.
Lakini gari lile halikuwa gari la kawaida, bali lilikuwa ni gari ambalo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kubebea maiti.
Na jeneza lilionekana, huku kukiwa kuna wanawake wawili wakiwa nyuma ya lile gari.
Walikotoka, hakuna aliejua.
Vedi alishindwa kuelewa kama ni maiti ya yule wanaefanana ama ni maiti ya nani iliochukuliwa.
Alihisi ni yake sababu walienda pale lilipokuwa jokofu lililobeba maiti yenye ufanano nae.
Na kama ni ile maiti; wao wanaipeleka wapi.
Mambo yale yalimchanganya Vedi; akaamua kutoka kwenye kundi la watu na kuongoza njia.
Kuna mahali alitaka kufika na kujisitiri kwa siku hiyo.
Alihitaji walau kuoga na kutoa uchovu, lakini pia alihitaji kupata mawazo kwa mtu aliemwamini na alihitaji mtu wa kumliwaza na wajue kitu wanachokifanya kwa majanga yale.
Akiwa anatembea kwa wasiwasi mwingi, akatoa simu yake baada ya kuona sehemu ya kusajili kadi za simu.
Alijongea pale na kusema shida yake kisha akatoa kitambulisho chake cha kupigia kura na walianza utaratibu wa kukamilisha usajili.
Haikuchukua dakika nyingi, tayari usajili ukawa umekamilika.
Akanunua vocha na kuondoka pale bila kuweka wala kuangalia kama simu yake imesoma usajili wake.
Akatembea taratibu hadi kona ya mwananyamala A kisha akasimamisha gari zilizokuwa zinaelekea mbagala.
Akapanda na hakukawia kupata nafasi ya kukaa.
Alipokwisha kukaa akaona ndio muda muafaka wa kuweka kadi kwenye simu yake na kisha aweke vocha na kupiga anakotaka kwenda ili ajue kama anaemhitaji yupo na kama hayupo basi afike nyumbani haraka mana yeye ndo anaelekea huko.
Ajabu tena!
Simu haikusoma na mtandao uliandika “emergency”.
Haiwezekani bwana!
Alijisemea kivivu, kisha akatoa kadi zote na kisha akazirejesha.
Hali ikawa ile ile.
Simu hazikusoma.
Akili yake ikamwambia, yawezekana tatizo sio la kadi za simu ila ni simu yenyewe.
Lakini simu ile haikuonekana kuwa ni bandia hadi ifungwe na mamlaka husika.
Hakuwa mgeni wa simu na alipoigusa gusa aliona kabisa itakuwa imefungwa.
“IPhone5 tangu lini zikawa na toleo bandia?” Vedi alijiuliza huku akirejesha simu ndani ya mkoba.
Alichoka hakika.
****
Gari ilifika kwenye kituo anachoshukia.
Akashuka na kuelekea mtaa alioukusuidia.
Tambo za miguu yake zilimfikisha kwenye nyumba ya uswahilini kidogo ila ilikuwa ni nyumba ya kisasa na ilikuwa na pande mbili.
Upande mmoja ulikuwa na milango mingi na kila mlango kulisikika sauti za muziki mkubwa huku nyimbo nyingi zikiwa ni za taarabu ya kuchambana.
Wanawake wa dar hao.
Alijisemea huku akipita na kuelekea upande wa pili ambako kulikuwa kuna nyumba iliojitegemea ikiwa na vyumba viwili na sebule.
Nyumba hii aliizoea na kila mara alifika pale.
Aliutazama mlango,alitabasamu baada ya kuona ukiwa wazi.
Akasukuma na kuingia.
Sebuleni hakukuwa na mtu ila alisikia muziki kwenye chumba alichokizoea kuliko hata sebule aliokuwapo wakati huo.
Akagonga mlango wa chumbani mara tatu kwa mtindo ambao alijua kabisa aliekuwamo angejua mgongaji ni nani.
Mlango ukafunguliwa taratibu na uso wa mtu ukatokea.
Vedi alitabasamu kwa unyonge.
Tabasamu halikujibiwa.
Ikaanza kumtia wasiwasi Vedi.
Mtu yule akaufungua mlango wote na kuingia na kumruhusu Vedi aingie ndani.
Vedi akaingia, kisha akaenda kukaa kitandani na kubaki akimtizama mwenyeji wake akiwa anavaa tai shingoni na kupamba mwili wake uliositiriwa na shati jeupe na suruali nyeusi na viatu vizuri vyeusi.
Vedi alibaki akimtizama bwana yule kwa mambo mawili.
Mosi alishangaa vile mtu yule alivyompokea bila kuonesha furaha yoyote usoni mwake, lakini pili alishangaa ni kwanini bwana yule hajastuka kwa ujio wake, au hajasikia kuhusu kifo chake? Au hajasikia kuhusu maiti inayofanana na yeye?
Sasa kama yote hajasikia;kwanini anamnunia tofauti na siku zote!
“Vedi naenda msibani” Hatimae bwana yule aliongea na kuvunja ukimya uliokuwa umeanza kutanda ndani ya chumba kile.
Vedi alistuka kidogo.
“Msiba wa nani tena” Alihoji.
Bwana yule akatabasamu kidogo kisha akamgeukia Vedi huku akifunga mkanda wa saa kwenye mkono wake wa kushoto.
“Ni kweli kwamba hujui kama umekufa na saa chache zijazo utazikwa?” Alizungumza yule bwana.
Heee!!
Vedi alishangaa.
Ilikuwa ni ngumu kumeza, mtu anazungumza kama vile ni jambo la kawaida kusema Vedi amekufa na wanazika na anaeambiwa maneno hayo ni Vedi mwenyewe.
Ajabu hii!!
Vedi alihisi hali ya ajabu ikiukumba mwili wake na wala hakuamini maneno yale makavu yanatoka kinywani mwa mchumba wake waliependana sana na walitarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
“Juma; kwa hiyo na wewe unaamini nimekufa?” Alihoji Vedi huku akilengwa na machozi.
“Ndio,najua umekufa na umekufa na umeshakufa moyoni mwangu pia” Juma alijibu huku akitungua koti kwenye enga.
Vedi aliona ua likiwa kwenye mfuko wa kushoto wa koti lile, ilimanisha kweli Juma alikuwa anaenda kuzika na zile ni nguo za maombolezo.
“Jay, kwa hiyo hapa unaongea na nani; mzimu wa Vedi au picha ya Vedi?” Alihoji Vedi huku akisimama kumfuata Juma au Jay alivyopenda kumwita.
“Vedi; tangu juzi usiku nilikuua katika moyo wangu, hivyo hata wakati naambiwa umekufa, bado sikustuka japo roho yangu ilikataa kukubaliana na ukweli na hatimae umefika kama nilivyotarajia, lakini Vedi kwanini umeamua kuyafanya haya?” Jay aliuliza kwa sauti ya uchungu huku akijitahidi kuzuia machozi yasimtoke.
Vedi aliganda kama sanamu, ni kama hakumwelewa vizuri mahabuba wake. Maneno aliyoyazungumza yalimchanganya.
“Nimefanya nini tena mimi hadi unilaumu hivyo?” Vedi alihoji kwa upole.
“Usijifanye hujui Vedi; yani Vedi unaamua kutengeneza kifo chako ili uende kuishi ulaya na mwanaume mwingine? Haya kwa nini usingevunja uchumba wetu kisha umtambulishe huyo bwana kuliko kuigiza kifo ili mtokomee?” Jay alizungumza kwa hisia.
Ebanee!
Vedi aligwaya hakika,na hakujua ajieleze vipi katika jambo jipya kama lile,hakujua ni nani alievumisha tena habari hizo mbaya.
“Mbona sikuelewi wewe!” Vedi alifoka.
“Hunielewi sio!” Jay alisema huku akichukua simu yake kwenye meza ya kitanda na kutoa nywila kisha akapekua kidogo na kumwonesha Vedi.
Asalalee!!
Vedi alitoa macho kama komba mlevi,hakuamini anachokiona kabisa.
Kwenye simu aliona picha akiwa amepiga picha mtu.
Zilikuwa picha za kimahaba kwenye bustani nzuri ya kupendeza.
Lakini mtu aliepiga nae picha zile ndie aliezua utata katika akili ya Vedi.
Alikuwa ni yule mtu anaevaa miwani usiku na mchana; mtu ambae alionesha ukatili wa kutisha licha ya kuachia tabasamu lake la kukopa.
Mtu yule alikuwa ni yule bwana aliemuona kule melini na kisha hospitali ya mwananyamala.
Tofauti ilikuwa ni moja tu, ya kuwa wakati wanapiga picha zile mtu yule alikuwa amevaa suti maridhawa ila haikumoendeza kabisa na pia hakuwa amevaa miwani na kupelekea jicho lake moja kuonekana likiwa tofauti na jicho lingine.
Bila kificho jicho moja lilikuwa la bandia; jicho la kondoo.
“Aah!! Sio mimi bwana” Vedi alilalamika akiwa haamini anachokiona.
Yani aliona mtu sawa na yeye akiwa amepiga picha za kimahaba na yule bwana ambae alikuwa na ukatili ulioonekana wazi wazi usoni mwake.
“Sasa kama sio wewe ni nani aliepiga picha hizi” Alifoka Jay.
“Jay sio mimi eti”
Vedi alijitetea.
“Hizi nguo hukuvaa wewe wakati unapita kuniaga unaenda harusini?” Jay alifoka tena.
“Ni hizo ila zimefanana na wala huyo mtu simjui kabisa Jay” Vedi alizidi kujitetea.
“Na kweli humfahamu” Alisema Jay huku akipekua simu yake na akatoka tena picha nyingine ilioonesha maongezi kwa njia ya ujumbe mfupi kwa mtandao maarufu wa whatsapp.
Vedi akausoma tena ujumbe ule.
Ulikuwa ni ujumbe wa makubaliano baina yake yeye na mtu mwingine ambae alimwandika kwa jina la “Kingbae” na namba ilikuwa ni ya kwake.
Doh!!
Vedi alichanganyikiwa kwa kushindwa kuelewa yalivyo mambo yale.
Kweli namba ni yake na hata picha iliokuwa “profile” ni yake.
Aligwaya mwanamke yule ambae taratibu uzito wa mwili wake ulianza kupungua.
“Nadhani umeona mlichokubaliana na huyo bae wako, sina mwanamke anaeitwa Vedi ila nina mwanamke anaeitwa marehemu Vedi. Si ndivyo ulitaka?” Alimaliza kwa kuhoji bwana Juma.
“Tafadhali Jay naomba unisikilize mpenzi wangu” Alisema Vedi kwa kusihi.
“Huna cha kunambia, nawahi msibani nikamzike mpenzi wangu” Jay alisema na kuendea mlango.
“Nooo!! Ja….” Hakumalizia kauli yake alijikuta peke yake ndani ya chumba huku akisikia mlango ukifungwa kwa nguvu na kutoa kelele za malalamiko huku mfungaji akiufunga kwa hasira.
Vedi alijikuta peke yake chumbani na badala ya kujadili kilichomleta na kusaidiwa mawazo ila amejikuta akikutana na jambo jipya kabisa.
Hakujua habari zile za uongo ni nani aliempa mchumba wake na aliempa alilenga nini.
Hakika ulikuwa ni mtihani usiojibika.
***
Karibu kwa maoni yako tafadhali