SoC03 Bajeti za posho na mashangingi, kodi za vocha zitumike kuwezesha wahitimu wa vyuo na nguvu kazi wasio na ajira

SoC03 Bajeti za posho na mashangingi, kodi za vocha zitumike kuwezesha wahitimu wa vyuo na nguvu kazi wasio na ajira

Stories of Change - 2023 Competition

Librarian 105

JF-Expert Member
Joined
May 6, 2023
Posts
261
Reaction score
356
Ujuzi na uzoefu vimekuwa kikwazo kwa vijana (hasa wahitimu wa vyuo) kuajiriwa.Japo kuna mikakati ya kuwakomboa kiuchumi kupitia uwekezaji na miradi ya maendeleo. Bado ajira zinazozalishwa hazikidhi mahitaji ya soko la ajira nchini. Hivyo kupelekea wengi wao kuwa wazururaji mitaani.

Serikali Ijitathmini:
Unapotafakari changamoto hii,huwezi kusita kuikosoa serikali kwa kushindwa kwake kusimamia mgawanyo wa pato la taifa, pale unapoona kila uchao viongozi wake wanajineemesha kwa posho ilhali wanalipwa mishahara mizuri sanjari na kugharamiwa baadhi ya mahitaji ya msingi kimaisha. Unaishia kuumia tu. Kwanini serikali isibadilishe matumizi ya bajeti za posho na mashangingi na makusanyo ya kodi za vocha zikatumika kuwezesha nguvu kazi hii kujiajiri kupitia shughuli za ujasiriamali, kilimo na ubunifu wa tehama?
Nikiamini mbali na kuwawezesha, pia nchi itaongeza ufanisi wa uchumi wa soko huria hadi kwa mwananchi wa kawaida, na kukuza vichochezi vya ukuaji wa biashara na fursa za kiuchumi. Isitoshe kuhamasisha ubunifu wa kuendeleza maliasili na rasilimali za taifa letu kwa ustawi wa jamii yote. Kwa kujenga kizazi cha uzalishajimali chenye uzalendo wa kuchapa kazi kujiletea maendeleo.

Namna ya kuwezesha vijana/wahitimu wa vyuo walio mtaani:
Uchumi wa soko huria wenye maono ya mageuzi ya kiuchumi yanayoanzia kuleta mapinduzi ya kijani ndio mkombozi wa kukomboa nguvu kazi hii endapo malengo yake yatasimamiwa kwa uadilifu. Dhamira ikiwemo tutafanikiwa kupunguza utegemezi wa misaada ya nchi wahisani na mikopo ya taasisi za kifedha za kimataifa. Huku nguvu kazi hii ikiongeza njia za uzalishajimali, ajira, vyanzo vipya vya kodi, na fursa mbalimbali za kiuchumi.

Mathalani posho zikifutwa, mashangingi yakawa yananunuliwa kila awamu mpya ya utawala inapoingia madarakani, na chanzo cha kodi za vocha kikatolewa kama mbegu ya kuzalisha vyanzo vingine vipya. Kisha nchi ikaazimia kuboresha ubepari wa kitaifa "sio wa chama" ina maana serikali itajipunguzia mzigo wa kutegemea sekta ya umma pekee kubeba soko la ajira nchini.

Jaalia jumla ya bajeti ya posho na mashangingi ni bilioni 200 kwa mwaka, huku makadirio ya makusanyo ya kodi za vocha yakawa ifuatavyo kwa mwaka:

Awali ukipitia ripoti ya TCRA ya mwezi oktoba,2022; jumla ya laini za simu milioni 58.1 zimesajaliwa. Nikitumia mahesabu ya chini, mtu mmoja kumiliki laini nne, utapata wastani wa laini milioni 15. Ikiwa laini milioni 6 ndizo zitakazoongezwa tsh.500 kwa siku ambapo kodi yake ni tsh.75.51. Ukizidisha milioni 6 * tsh.75.51 * siku 30 * miezi 12; unapata takribani bilioni 163.08 kwa mwaka. Ukizijumlisha na bilioni 200, unakuwa na fungu la bilioni 363.08, maalumu za kuwafungulia nguvu kazi wasio na ajira nchini ulimwengu wa kujiajiri katika sekta binafsi na kilimo biashara kutegemeana na talanta na vipawa vyao vya kielimu. Halikadhalika ukirejea ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na uchambuzi wa sensa ya mwaka 2022; inaeleza kuwa nguvu kazi wasio na ajira ni watu 2,321,884; ambao ndio shabaha yangu ya kuwawezesha baada ya usaili makini na semina za kujitambua kujitegemea ili kulitumikia taifa katika timu zifuatazo:
  1. Kilimo cha chakula na biashara.
  2. Uvuvi na ufugaji.
  3. Tehama, masoko na ushauri wa kifedha.
Nikishauri miradi husika kutekelezwa kulingana na kanda za SMEs nchini kuelekea uchumi wa viwanda na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa miradi hii kujumuishwa na miradi ya maendeleo pamoja na mpango wa maendeleo wa taifa.

Mpango Mkakati Wake:
Kwa vile makisio ya bajeti ni bilioni 363.08, serikali inatakiwa kugharamia pia malazi, chakula na usafiri. Kwa mfano timu 1 na 2 zikitengewa bilioni 170 kila moja, na kuwa na kituo kikuu cha mradi aidha wa kilimo au cha uvuvi na mifugo vilivyoratibiwa kimkoa na kanda za kilimo. Halafu bilioni 23.08 wakatengewa timu 3 ili kuratibu Ofisi ya Taifa ya kanzidata za miradi yote husika na vituo vidogo vya kanda kwa ajili ya ufuatiliaji na utathminishaji wa miradi, utawala na masoko na ushauri wa kifedha kwa kutoa huduma hata kwa miradi mingine ya ya umma kama vile BBT wa kilimo na Mifuko ya Halmashauri ya kukopesha vijana, kinamama na walemavu.

Muundo Wa Uongozi
  • Serikali: itasimama kama mwezeshaji na mwangalizi mkuu na ikiwezekana kwa ushirikiano na baraza la vyama vya siasa nchini kama waangalizi wasaidizi. Ili kuumpa mradi huu ajenda ya kitaifa na usitumike kisiasa.
  • Bodi Ya Wadhamini:  itaundwa na wajumbe kutoka sekta ya viwanda, kilimo, uvuvi na mifugo, na mifuko kama NSSF na mengineyo.
  • Bodi Ya Wakurugenzi: itaundwa na wataalamu wabobezi wa fani za miradi husika wakishirikiana na wahitimu wa vyuo ili kuruhusu kurithishana ujuzi, taaluma na uzeofu.
  • Mameneja Wa Miradi: hawa watachakuliwa na Bodi Ya Wakurugenzi na kuidhinishwa na Bodi Ya Wadhamini ili kuwepo ufanisi pamoja na uwajibikaji kusimamia miradi.
Vivyo hivyo, ili kuwepo na tija ya kufikia malengo na utekelezaji wa miradi kwa ufasaha, taasisi kama TACRI, SIDO, VETA, TEMDO, CARMATEC, TARI, LITA, TAFIRI N.K. Hazina budi kuwa wadau wenza wa miradi hii ili kuchagiza ufanisi wa miradi kwa kasi zaidi na maendeleo kwa ujumla ya nguvu kazi hii kumiliki na kuendesha viwanda vidogo kwa kutumia teknolojia rahisi mijini na vijijini. Pamoja na kampuni ndogo ndogo za usafirishaji, ukuzaji thamani na ufungashaji wa bidhaa kwa masoko ya ndani na ya nje.

Baadhi Ya Majukumu Ya Timu Husika:
  1. Tehama: kuratibu na kuhifadhi kanzidata za miradi na kubuni majukwaa ya masoko ya mitandaoni ili kuwakomboa wazalishaji mali kama vile wakulima kulanguliwa mashambani.
  2. Masoko, uhasibu na ushauri wa kifedha: kufanya kazi za kihasibu na ukaguzi wa ndani wa vitabu vya mahesabu, utafiti wa masoko na kutengeneza fursa mpya za biashara, huduma za ushauri na kusimamia miradi kwenye masoko ya mitaji, na ushauri wa masuala ya kifedha na uandaaji wa bajeti.
  3. Kilimo: Kukuza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo. Ili nchi iondokane na kuuza malighafi badala yake iwe ya kuzalisha bidhaa na huduma zingine.
  4. Kutekeleza mipango mingine ya maendeleo na miradi ya kitaifa yenye kuendana na miradi tajwa kwa malengo ya kukuza mapato ya wazalishajimali nchini.
  5. Kubuni njia mpya za uzalishamali na shughuli za ujasiriamali.
  6. Na kadhalika.
Hitimisho
Ifahamike wakati huu tulionao sisi, hatuwezi kujenga nchi yetu kwa mbinu ya ukoloni au ukoloni mamboleo ama kwenye majukwaa ya kisiasa, bali ni kwa kuziendeleza maliasili na rasilimali tulizobarikiwa kwa kuzalisha rasimali watu wa kuzisimamia kupitia sekta binafsi na diplomasia ya uchumi tu. kwa mfumo wa kukusanya mitaji ya miradi kama hii kwa kuilazimisha serikali yetu kubana matumizi na kufuta bajeti zenye kuneemesha kada ya wanasiasa nje ya mishahara yao na stahiki zao zingine za utumishi wa umma. Hakuna njia ya mkato kujenga nchi ya uchumi wa viwanda. Shime viongozi wa serikali wajitathmini kisha waitazame nguvu kazi hii wasio na ajira ili waweze kutunga sera za nchi kuthamini sekta binafsi kama injini ya uchumi wa nchi. Ili ajira zijazo zitokamane na kujiajiri kupitia uchumi wa viwanda vidogo vya teknolojia rahisi kwenye tawala za mikoa na serikali za mitaa ili kuongeza fursa za kibiashara na uchumi kwa raia wake kote nchini. Tukiamua maendeleo ya kiuchumi yanawekana.
 
Upvote 2
Sidhani Kama ungekuwa kwenye iyo POSITION ungeandika haya uliyoyandika hapa
 
Back
Top Bottom