Slaa: Tume ichunguze kifo cha Daudi Ballali
na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amependekeza kuundwa kwa tume huru ya kimataifa itakayochunguza mazingira ya kifo cha Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa ambaye ni Mbunge wa Karatu, alisema umuhimu wa kuundwa kwa tume hiyo unatokana na utata uliozingira habari zote zinazomhusu Ballali tangu alipoondoka hapa nchini Agosti mwaka jana.
Dk. Slaa, mwanasiasa aliyeibua tuhuma kadhaa dhidi ya Ballali, na mmoja wa wanasiasa waliokuwa mstari wa mbele kutaka kurejeshwa nchini, ili aje kujibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili, ikiwa ni pamoja na kusaidia uchunguzi wa wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT, alisema kifo chake kabla ya kukamilika kwa suala hilo, ni pigo kubwa.
'‘Tunaiomba serikali iunde tume ya kimataifa ili ukweli ujulikane. Huyu ni mtu mkubwa, ana siri nyingi za taifa. Anahusishwa na ufisadi. Hatuwezi tukaliacha suala hili likaachwa hivi hivi tu.
'‘Kama serikali imeficha ugonjwa, hospitali na hata hicho kifo ambacho taarifa zake zimepatikana baada ya siku nne, tunataka tume huru iundwe ihusishe majaji na watu wenye heshima katika jamii ya kimataifa," alisema Slaa.
Mwanasiasa huyo ambaye ndiye aliyesoma orodha ya mafisadi mwaka jana na kuibua mwamko wa kipekee katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi, alirejea kauli aliyopata kuisema siku zilizopita kuhusu Ballali na umuhimu wake wa kumrejesha hapa nchini wakati akiwa hai.
'‘Nilipata kusema huko nyuma, na leo narejea tena kulisema hili kwamba, iwapo Ballali atakufa kabla ya hajarejeshwa nchini kujibu tuhuma za ufisadi ndani ya BoT na hata kabla hajahojiwa na Kamati ya Mwanasheria Mkuu inayochunguza kashfa ya EPA, basi damu yake itakuwa juu ya serikali," alisema Slaa.
Alisema mwenendo mzima wa namna serikali na Rais Jakaya Kikwete walivyolishughulikia suala zima la Ballali, kuanzia kuondoka kwake kwenda nje kwa matibabu, kulazwa na baadaye kufa, ni jambo linalotia shaka na kuibua maswali mengi.
Mwanasiasa huyo alisema anaamini haiwezekani Ballali, ambaye ugavana wake ulitenguliwa na si kufukuzwa, aende nje kwa matibabu na alazwe pasipo serikali kupitia Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Marekani, kujua mahali aliko.
Alisema anaamini kwamba gharama zote za matibabu ya Ballali zilibebwa na serikali, kwani hata baada ya uteuzi wake wa ugavana kutenguliwa, aliendelea kubakia kuwa mtumishi wa serikali.
'‘Hiki kiini macho cha serikali kudai eti hawajui alikokuwa amelazwa na anakoishi Ballali, ni ushahidi wa wazi kwamba serikali ilikuwa inaficha jambo.
'‘Walikuwa wakijua aliko, na walifanya hivyo wakijua kwamba iwapo angerejea angeweza kutoa siri kwa kuwataja wahusika wengi, na hivyo kuleta mtikisiko mkubwa serikalini," alisema Dk. Slaa.
Aliilaumu serikali kwa kutoa taarifa nyingi zinazokinzana kila mara waandishi wa habari walipokuwa wakifanya juhudi kubwa katika kufuatilia alikokuwa gavana huyo wa zamani wa BoT.
Alisema uamuzi wa serikali kukaa kimya kwa muda mrefu pasipo kutoa taarifa hata baada ya Ballali kufa, ni ushahidi mwingine wa namna ilivyokuwa ikishikwa na kigugumizi kuhusu suala hilo.
'‘Ninachosema hapa ni kwamba, wakati serikali inapotoa majibu yenye utata na yenye kupingana, haijawahi kusimama na kusema aliyeondoka ni mtu wetu, Mtanzania mwenzetu. Ni kwa nini serikali ilikuwa haifuatilii? Kwa nini ubalozi haukufuatilia? Unaweza kuona namna serikali inavyojaribu kuficha jambo," alisema Dk. Slaa.
Alisema ni jambo la ajabu kwamba, maofisa wa ubalozi wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kila mara Watanzania wanapokwenda India kwa matibabu ya moyo, tena kwa watu wa kawaida kabisa na hivyo kuzua maswali ni kwa nini kwa Ballali hali ilikuwa ni tofauti.
Kama hiyo haitoshi, Dk. Slaa alieleza kushangazwa na kifo cha Ballali ambacho kimetokea siku chache tu baada ya kuwapo kwa taarifa za makachero kutumwa kumfuatilia nchini Marekani.
'‘Ni jambo lisiloeleweka sawa sawa na linalopaswa kutolewa maelezo. Haiwezekani tunasikia makachero wamekwenda kumfuata na siku chache baadaye kupitia katika mtandao tunaambiwa amefariki na kisha siku chache baadaye inatangazwa rasmi amekufa. Nini kimemuua? Serikali itujibu," alisema.
Alisema huko nyuma na hata katika mtandao kulikuwa na taarifa za mtu huyo kuwekewa sumu, jambo ambalo serikali pamoja na kutakiwa kulitolea ufafanuzi ilikaa kimya.
Alieleza kushangazwa kwake pia na hatua ya Kamati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayochunguza Kashfa ya EPA, kuwahoji watuhumiwa wengine na wamiliki wa kampuni 22, huku ikimuacha shahidi muhimu Ballali, katika muda wote wa miezi karibu mitano ya kazi yao.
'‘Ni kwa nini wanahojiwa akina Jeetu Patel na wengine wa makampuni 22, na hawa watu hawakuteremka BoT kama Roho Mtakatifu. Ninaamini Ballali angekuwapo angeeleza siri hizo," alisema Dk. Slaa
..................
NADHANI DK. SLAA ANAPOINT NZURI HAPA. KUNA HAJA YA UCHUNGUZI WA JAMBO HILI.