(Kutoka gazeti la "Kulikoni" kama ilivyoahidiwa na Halisi)
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Daudi Ballali, ambaye alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete mapema mwezi huu amedai kuwa wanaompakazia wamemfanya mbuzi wa kafara.
Kwa mujibu wa watu walio karibu na Ballali, gavana huyo kasema katika utendaji wake wa kazi BoT kwa miaka tisa amefanya kazi kwa uaminifu mkubwa na kamwe hakuhusika na ufisadi unaotajwa sasa.
Mdogo wa Ballali ambaye anaishi naye Boston, Marekani ameliambia gazeti hili kuwa kaka yake ambaye sasa anaendelea vyema baada ya kushambuliwa na maradhi, anatarajia kuuweka ukweli wa kile alichoeleza kuwa uongo unaosambazwa dhidi yake.
Amesema Ballali anasikitishwa na namna baadhi ya viongozi wa serikali wanavyojikosha kuhusu ufisadi BoT wakati wakiutambua ukweli wa kile kilichotokea.
Ballali amedai kuwa kutokuwepo kwake nchini ndiko kumesababisha yeye kubebeshwa lawama zote kwa wizi huo wa BoT.
Hata watu waliohusika na wengine wakishinikiza kulipwa kwa fedha kwa kampuni ambazo mimi sikuwa nazo shaka kwa kuwa zilikuwa na mkono wa wakubwa, nao wananilaumu, amenukuliwa Ballali akisema.
Habari za uhakika zinaeleza kuwa Ballali ameapa kuwataja wote wanaompakazia kwa wizi huo, ambao ameueleza kuwa hakuutambua mara moja.
Gavana huyo amesema anao ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuagizwa na wale aliowaita wakubwa kulipa fedha kwa sababu ambazo hata hivyo alizieleza kuwa aliambiwa ni kwa usalama wa taifa
Ballali aliyeondoka nchini kwenda kutibiwa Marekani, baada ya kupata tiba Afrika Kusini kwa muda wa wiki tatu, amekuwa akipamba habari katika magazeti zikinukuu baadhi ya viongozi wa serikali wakieleza namna alivyohusika na ufisadi wa kutisha katika Benki Kuu ya Tanzania kupitia ulipaji wa madeni ya nje (EPA).
Zaidi ya bilioni 133/- zinaelezwa kuibwa kwa utaalamu mkubwa kwa kuhusisha kampuni 22, zikiwemo hewa, za ujanja ujanja na za kitapeli ambazo zilitumika kufanikisha wizi huo.
Ukaguzi uliofanywa na kampuni za ukaguzi wa hesabu zinazoheshimika; Ernst & Young na Delloite & Touche ndio uliogundua kuwepo kwa uozo huo wa kudidimiza uchumi na neema ya Watanzania baada ya kupewa kazi hiyo na serikali ya Rais Kikwete.
Kiasi hicho cha fedha bilioni 133/- kingetosha kujenga shule za sekondari 266 zenye madarasa maabara na samani za kisasa. Kiasi hicho pia kingeweza kuendesha wizara kama ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka 15 bila nyongeza ya bajeti yake ya sasa.
Wathamini wa majengo wanaeleza kuwa kiasi hicho cha fedha pia kingeweza kujenga majengo ya ghorofa zote yaliyoko Kariakoo, Mnazi Mmoja, na katikati ya jiji la Dar es Salaam na fedha nyingine kujenga barabara, kwa kiwango cha lami kuunganisha majengo hayo.
Hakuna ubishi kuwa kaka hawezi kufanya jambo la kijinga namna ile, hana tamaa na wala siyo mwizi, ndiyo maana amekuwa akiaminiwa na taasisi kubwa za fedha za kimataifa ambako analipwa vizuri kwa kazi za ushauri, iweje leo azuliwe uongo na kuchafuliwa jina, lazima atasema kuukanusha, alisema mdogo wake huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini kwa sasa.
Mdogo huyo wa Ballali ambaye mwaka jana alikuwa hapa nchini amesema mshahara wa kaka yake unamtosha kufanya mambo makubwa na ya maendeleo bila hata kuiba mali ya umma.
Huwezi kuamini, kaka Daudi hapendi mtu anayepindisha sheria, na huo ndio umekuwa msimamo wake mara zote katika maisha yake na hata kumfikisha hapo alipo, ni mwaminifu sana. Hizo pesa kama zimeibwa BoT, basi yeye siyo mfaidi, bali zimewafaidisha wengine, aliongeza kwa sauti ya kushangaa na kusikitika wakati akizungumza na gazeti hili.
Inaelezwa kuwa mshahara wa Ballali, pamoja na kuwa na magari mawili ya serikali aliyokuwa akitumia nyumbani na ofisini, kupewa nyumba iliyo na samani zote na wafanyakazi, alikuwa akilipwa mshahara wa milioni 25/- kila mwezi.
Ballali amefanya kazi Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa zaidi ya miaka 25 akiwa Washington, Marekani.
Mbali na kufanya kazi IMF na Benki ya Dunia, Ballali anasifika kwa kushauri na kufanikisha uimara wa uchumi wa baadhi ya nchi za dunia ya tatu, ikiwemo Ghana ambayo inangara kwa uimara wa uchumi wake.
Kufuatia wasiwasi wa usalama wa maisha yake, mdogo wa Ballali amesema kaka yake amelazimika kuishi katika makazi ambayo hayafahamiki kwa wengi kwani wanaompakazia wanaweza kumdhuru kwa lengo la kuficha kile atakachokieleza kwa umma.
Hivi sasa, kaka anapumzika mahali wanakokujua wachache, kwani kuna hatari ya kudhuriwa na watu wanaoendelea kumpakazia huku wakiutambua ukweli kuwa walikuwa wahusika wakuu wa kutolewa kwa fedha hizo za BoT kwa njia ambazo sasa hata yeye anatambua hazikuwa halali, amesema mdogo huyo wa Ballali.
Hata hivyo, hakuwa tayari kueleza ni lini Ballali atarejea nchini kwa ajili ya kuweka bayana kile anachoamini ni ukweli wa shauri hilo ambalo limekuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania, nchi yenye idadi kubwa ya watu masikini, wengi wakishindwa hata kumudu mlo wa siku moja.
Ballali aliteuliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kushika wadhifa huo kwa mkataba wa miaka 10 na kurithishwa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alimfukuza kazi bada ya kupata taarifa ya ukaguzi uliogundua kuibwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.
Katika kipindi hicho, akiwa amedumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka tisa, Ballali alikuwa akiripoti kwa Basil Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha wakati wa Mkapa na Zakhia Meghji ambaye ni Waziri wa Fedha wa sasa.