Baraza la Mawaziri: Moshi mweupe sasa kuonekana Jumanne
* Yadaiwa atapunguza mawaziri 20
* Tetesi za kuteua Zitto, Mdee zaenea
* Wapinzani wasema hawana habari
Na Muhibu Said
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuzima shauku kubwa na ya muda mrefu ya Watanzania kwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri, mjini Dodoma Jumanne baada ya kuahirishwa Jumatatu
Shughuli hiyo ambayo awali ilitarajiwa kufanyika saa 11:00 jioni, itafanyika Jumanne saa 4:00 asubuhi, katika Ikulu Ndogo ya Chamwino, mjini hapa.
Mwandishi Msaidizi wa Rais, Premy Kibanga amethibitisha suala hilo kupitia taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
"Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kutangaza Baraza la Mawaziri kesho (leo) Jumanne
(12/02/2008) saa 4.00 asubuhi katika Ikulu Ndogo ya Chamwino, Dodoma," alisema Kibanga na kuwataka wahariri, waandishi, wapiga picha kuwasili katika eneo hilo saa 3.00 asubuhi, ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Rais kuvunja Baraza la Mawaziri wiki iliyopita kutokana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa huo kufuatia kuhusishwa kwenye kashfa ya upendeleo katika zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond Development ya Marekani.
Kutokana na hatua hiyo, Alhamisi wiki iliyopita, Rais Kikwete alimteua aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu mpya.
Pinda ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mashariki (CCM), aliapishwa kushika wadhifa huo siku iliyofuatia.
Ijumaa wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Samwel Sitta aliliambia Bunge kuwa alikuwa na fununu kwamba, Rais Kikwete angetangaza baraza hilo jana.
Taarifa hiyo ambayo jana ilitawaliwa karibu vyombo vyote vya habari, iliwafanya Watanzania kusubiri suala hilo kwa hamu na shauku kubwa, kabla ya Ikulu kutoa taarifa rasmi jana mchana kuuarifu umma kwamba, shughuli hiyo itafanyika leo.
Hata hivyo, Sitta alikaririwa na kipindi cha Harakati kinachorushwa hewani na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) jana jioni akisisitiza kuwa taarifa za kutangazwa kwa Baraza jipya la Mawaziri jana, zilitolewa na Ikulu na kwamba uamuzi wa kuahirisha hadi leo, uko nje ya mamlaka yake.
"Ni Ikulu ndio waliosema, sasa kama kuna kuahirishwa, jambo hilo si letu, na mimi sina uwezo wa kumpangia Rais siku ya kutangaza," alisema Sitta kupitia kipindi hicho.
Hata hivyo habari zilizopatikana jana zinadai kuwa, awali, Baraza jipya la Mawaziri lilitarajiwa kutangazwa jana.
Lakini shughuli hiyo ikaahirishwa baada ya Kambi ya Upinzani kukataa uteuzi wa baadhi ya wabunge wao kuingizwa katika baraza hilo kwa madai kwamba hawakushirikishwa katika mchakato huo.
Baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani wanaodaiwa kuingizwa katika baraza hilo, ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Halima Mdee, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Zitto alipoulizwa na mwandishi wa Mwananchi jana, alikiri kupigiwa simu na watu wa kada mbalimbali za kumpongeza kwa kuteuliwa kuwamo katika Baraza jipya la Mawaziri, lakini akasema hajapata taarifa za uteuzi huo.
Nao Mdee na Hamad walipoulizwa kwa nyakati tofauti jana, walisema hawajapata taarifa zozote kuhusiana na uvumi huo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alipoulizwa alisema hajapata taarifa za kuteuliwa kwa mbunge wao yeyote, lakini akasisitiza msimamo wa chama chake kwamba, hawatakubaliana na uteuzi huo.
"Lazima kuwapo na majadiliano na makubaliano kabla ya kuamua uteuzi huo na siyo jambo hilo zito lifanywe kwa mtu mmoja mmoja pekee, ndivyo inavyofanyika duniani kote," alisema Dk Slaa ambaye pia ni Mbunge wa Karatu (Chadema).
Habari zilizopatikana jana zinafahamisha kuwa, Baraza jipya la Mawaziri limefanyiwa mabadiliko makubwa kwa kupunguza idadi ya mawaziri na manaibu wake.
Imeelezwa kuwa, katika mabadiliko hayo, idadi ya mawaziri imepunguzwa kutoka mawaziri 29 waliokuwapo zamani hadi kufikia mawaziri 25 wa sasa.
Pia, idadi ya manaibu mawaziri imepunguzwa kutoka 31 wa zamani hadi kufikia manaibu mawaziri 15 wa sasa.