Mimi nadhani Chuo Kikuu cha DSM kimeonesha njia na vingine bado vina mda wa kutosha kuipita. Tukubaliane kwamba UDSM ni baba kama sio babu wa Vyuo Vikuu vyote Tanzania achilia mbali vitivo vya sheria na elimu ya siasa ambavyo mambo ya katiba yanavihusu zaidi. UDSM ina miaka zaidi ya 40 ikisheheni maprofessa na madakitari wenye uzoefu unaliotukuka katika fani zao. Chuo Kikuu cha Mzumbe hakina hata miaka kumi toka kilivyopata hadhi ya chuo kikuu. Lakini kimepiga hatua hakipaswi kupuuziwa. Chuo Kikuu cha Dodoma hakina hata miaka mitano. Ni kitoto kama nikisema. Fani ya sheria haina hata miaka miwili kati chuo hicho. Tukitarajia kifanye makubwa kama UDSM itakuwa ni sawa na kukamua damu toka katika jiwe.
Tukirudi katika kongamano la katiba la jana limetoa muelekeo mzuri sana katika mstakbari wa Taifa kuhusiana na Katiba mpya licha ya mapungufu machache yaliyojitokeza. Wachokoza mada PROF SHIVJ na ULIMWENGU walidodosa mada kwa umahiri mkubwa na bila kuonesha ushabiki wa kisiasa jambo ambalo liliwahamasisha hadhira iliyokuwepo kuweza kuchangia kwa mafanikio. Prof Shivji aliweka wazi umhimu wa kuwa na katiba mpya kwa kujikita zaidi la uhalali wa kisiasa (political legitimacy)wa ya katiba tuliyonayo kwa sasa. Kwa mujibu wa Prof Shivji, Katiba tuliyonayo japo uandikwaji wake haukuwahusisha sana wananchi kuna wakati ilikuwa inapata uhalali wake kutokana na itikadi mbali mbali za kisiasa zilizokuwepo wakati huo. Kubwa zaidi ilikuwa ni itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Baada ya kuzikikwa kwa Azimio la Arusha na Azimio la Zanzibar na kuivusha nchi toka kwenye ujamaa kwenda ubepari, uhalali wa kisiasa wa Katiba yetu, kwa mujibu wa Prof Shivji, ulipoteza muelekeo. Hivyo palikuwa na ulazima kwa serikali kutafuta uhalali mwingine wa kisiasa kwa kuja na katiba mpya itakayoweka misingi mipya ya muelekeo wa nchi katika mfumo mpya wa kisiasa na uchumi.
Kwa mujibu wa Prof Shivji tatizo la Katiba sio sana katika vifungu vya kanuni na maelekezo yaliyomo katika katiba bali ni mfumo mzima wa upatikanaji wa katiba na namna inavyokubalika kwa watu. Kwa hili, Profesa alikuwa anaowanisha katiba kama mwongozo na sheria kuu na kama nyenzo kuu ya uhalalishaji wa matumizi ya mamlaka. Msimamo wa Profesa Shivji uliungwa Mkono na Ulimwengu ambaye alienda hatua mbele zaidi kwa kusisitiza kwamba Katiba kama nyaraka ya kisheria na chimbuko la madaraka na ukomo wa madaraka kwa dola na vyombo vyake haiwezi kuwa na maana yoyote kama hamna maadili ya uongozi na utashi wa dhati wa kuitii. Bila shaka ni kutokana na ukweli huo kwamba nchi kama Uganda ambayo ilikuwa ni ya kwanza kuandika Katiba mpya wakati wa vuguvugu ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi bado haina mafunzo ya maana katika nchi nyingine kuhusiana na demokrasia na utawala wa sheria.
Kwa upande mwingine mh Tundu Lisu alijaribu kutofautiana na Professa Shivji kwa kusema tatizo kubwa katika katiba sio kukosa uhalali wa kisiasa bali ni kutokuwa na uwezo wa kuifikisha Tanzania kesho. Hakutoa ufafanuzi sana kuhalalisha hoja yake pengine kutokana na uchache wa muda aliopewa. Mimi binafsi sikupata bahati ya kupata nafasi ya kuchangia kutokana na watu wengi kutaka nafasi hiyo licha ya uhaba wa muda. Kwa uelewa wangu wa haraka haraka Mh. Lisu alikuwa anamaanisha kwamba Katiba yetu inamapungufu sana katika kanuni na maelekezo yake kiasi kwamba haiwezi kutufikisha kesho. Baadhi ya mapungufu ambayo wachangiaji wengine pamoja na wazungumzaji wakuu waliyoyagusia ni pamoja na madaraka makubwa ya Raisi, kutokuwepo Tume Huru ya Uchaguzi, haki za binaadamu kutolindwa ipasavyo, matatizo ya muungano nk.
Suala la kujiuliza ni kwanini kilio cha katiba mpya kimepata kasi zaidi kuanzia kipindi tulipokwenda vyama vingi na mfumo wa kibebari? Kwa nini hayakujitokeza katika kipindi cha Mwalimu kipindi ambacho "kicontents" katiba ilikuwa na mapungufu mengi ya msingi kuliko sasa?. Kwa mfano, katiba yetu haikuwa na vifungu vinavyolinda haki za binaadamu na mamlaka ya Raisi na wanasiasa yalikuwa makubwa zaidi. Mimi nadhani Professa Shivji yuko sahihi katika hili japo pia kuna mambo mengi ya kihistria yanayoweza kusemwa kuhusiana na uhalalishaji wa matumizi ya mamlaka kipindi cha ujamaa na kujitegemea.
Jambo lingine la msingi, ambalo hata mimi nimeshalizungumzia huko nyuma, ni namna mchakato wa katiba mpya unavyopasa kuanza. Prof. aliunga mkono Raisi kuunda Tume na kuwataka wananchi kupiga kelele kuhakikisha kwamba Tume hiyo inakuwa huru na inawakilisha makundi yote mhimu ya kijamii. Prof aliainisha hatari ya mchakato huo wa awali kuanzia Bungeni.
Mapungufu madogo madogo yaliyojitokeza ni pamoja na hili ambalo linatukabiri katika Forum yetu la wachangiaji kuwa na jazba na kukosa uvumilivu wa hoja zinazopingana nao. Baadhi ya wanakongamano walionekana kuwazomea wale wanaotoa hoja tofauti na misimamo yao bila hata kujali umri na heshima zao. Ikubalike kwamba panapoitishwa kongamano la watu mbali mbali tofauti za kimitizamo zinatarajiwa na washiriki wanapaswa kuvumiliana na kuheshimiana katika toafuti zao. Tatizo la ushabiki kwa baadhi ya wachangiaji toka katika hadhira pia lilikuwepo.
Mchangiaji mmoja raia wa Kenya aliikosoa Katiba kwa kudai kwamba inamruhusu ofisa wa polisi kumupiga raia risasi na kufafanua jinsi ambavyo hakuridhishwa na Mh. Kikwete kuwa Raisi. Alieleza zaidi kwamba yeye mwenyewe ni muathirika wa mapungufu haya lakini hakufafanua zaidi ilikuaje. Raia wa nje mwenye busara na kujua mipaka yake ya kuwa katika nchi za watu asingetarajiwa kusema hayo. Kenya jeshi la polisi mara kadhaa limepiga risasi raia wake lakini sidhani kwamba walikuwa wanatekeleza haki yao ya kikatiba. Askari polisi waliouwa huko Arusha katika maandamano hawakuwa wanatekeleza haki yoyote katika katiba. Ifahamike kwamba chini ya Katiba na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai polisi hawaruhusiwi kuuwa raia. Uhali wa kuuwa katika nchi zote unakuwepo katika mazingira ya dhalula (necessity) pale kuuwa kunakuwa lazima kwaajili ya kulinda maisha ya watu wengine zaidi au maisha ya askari wenyewe. Kama kwenye sakata la Arusha mazingira hayo ya dhalura yalikuwepo au la hilo ni suala la kimantiki na ukweli wa mambo. Kwa hivi sasa kuna madai kinzani toka Jeshi la Polisi na Chadema huku kila mmoja akimsukumia mwingine lawana. Hoja ya Chadema sio kwamba polisi hawaruhusiwi kutumia silaha za moto katika mazingira yoyote bali ni kwamba hayakuwepo mazingira yaliyohalalisha matumizi ya risasi za moto. Kwa kuwa suala hili liko Mahakamani ni sheria za nchi zinaruhusu maofisa wa jeshi la polisi kushitakiwa kama walikiuka sheria tuache hatua za kisheria zichukuliwe.