Wiston Mogha
Senior Member
- Feb 13, 2014
- 168
- 141
Salaam Mama Rais Samia.
Wakati yalipoanza matukio ya utekaji kipindi cha Serikali ya awamu ya 5; yalikuwa ni matukio mageni. Walakini kama vile hayataki yakawa mazoea kabla ya kuota mizizi.
Pengine isingekuwa hofu sana kama ungekuwa ni utekaji tu, ila watekaji wenyewe kuwa WATU WASIOJULIKANA na huku waathirika wake kuwa wakosoaji wakubwa wa Serikali; kulileta mashaka makubwa. Mbaya zaidi katika kipindi hicho, JESHI LA POLISI na IDARA YA USALAMA WA TAIFA wamekuwa wakituhumiwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine.
Mheshimiwa Rais.
Kwa siku kadhaa Sativa255 alipotea; labda sahihi zaidi niseme alipotezwa iwapo si kutekwa. Kwa mujibu wa maelezo yake, watekaji walimpeleka Polisi Osterbay kabla ya kwenda kumaliza unyama wao huko Katavi.
Kutajwa kwa Jeshi la Polisi ndiko hasa kulikonisukuma kukuchukulia ujiti, wino na karatasi. Zaidi wakati nayafikiria haya ninayokwandikia, kichwani mwangu kulijaa jazanda ya sura yako; sura nzuri yenye macho ya huruma. Sura inayonishurutisha kuchagua na kuteua maneno ya kuikabili. Japo una sura namna hiyo, lakini yapo ya kweli ambayo hata wewe mwenyewe huna ubavu wa kuyapinga. Ndiyo! Hunao hata kama ungataka.
Mosi
Mheshimiwa Rais.
Jeshi la Polisi la Awamu ya Sita ndilo lilelile la awamu zilizopita; Jeshi la Polisi ambalo limekuwa likituhumiwa kwa utekaji, kubambikia watu kesi na kushughulikia wakosoaji wa Serikali. Jeshi ambalo kwa sheria na vitendo vyake, limekuwa jeshi la mabavu badala ya kuwa jeshi la huduma.
Pili.
Mheshimiwa Rais.
Idara ya Usalama wa Taifa ya Awamu ya Sita ndiyo ileile ya awamu zilizopita. Idara ambayo pamoja na kwamba kisheria hairuhusiwi kukamata watu, walakini imekuwa ikituhumiwa kukamata na kutesa watu; hasa wakosoaji wa Serikali.
Tatu.
Mheshimiwa Rais.
Sheria kandamizi zilizotajwa na tume mbalimbali(miongoni mwa Tume hizo, Tume ya Jaji Nyalali) sheria hizo zingalipo hata sasa katika awamu yako, kama zilivyokuwepo katika awamu zilizopita. Sheria hizi zimekuwa zikitumiwa na Serikali kufanya uhalifu dhidi ya Vyombo vya Habari, Vyama vya Upinzani, Wanaharakati, na Wakosoaji wa Serikali.
Nne.
Mheshimiwa Rais.
Katiba iliyoko sasa, ndio ileile iliyokuwako katika awamu zilizopita. Katiba ambayo imezaa Mfumo wa Nchi ulioshindwa kumlinda Akwilina, Ulimboka, Ben Saanane, Tundu Lissu, Azory Gwanda, Tito Magoti, Babu Duni, Ismail Jussa, Mazrui Nassor, Kabendera, Alfonsi Mawazo, Abdul Nondo na hata mimi Dotto Rangimoto Mfumo wa Nchi ulishindwa kunilinda mwaka 2020 dhidi ya Utawala wa mkono wa chuma wa Rais Magufuli. Orodha ya watu waliokosa hifadhi na Mfumo wetu ni ndefu na inaanzia tangu enzi za Mwalimu Nyerere. Aidha ukiyashufu mambo kwa kina utagundua kuwa kushindwa kwa mfumo kuna sura nyingi; na kushindwa kulinda Uwakili wa Fatma Karume ni moja miongoni mwa sura zake.
Nini nataka kusema hapa?
Mheshimiwa Rais. Unaweza kuwa mtu nadhifu sana, walakini kwa uchafu wa mambo hayo manne uliyoyarithi, fanya utakavyo fanya—midhali yapo, nawe utachafuka tu. Hutakuwa nadhifu kamwe! Kwa kuwa mambo haya yananuka, nawe hutakosa kutuzi kila wendako!
Mheshimiwa Rais.
Baadhi yetu tuna silika ya kujipendekeza kwa viongozi na watawala. Kwa hivyo wapo wanaojipendekeza kwako; na kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wengi watajipendekeza. Wengine katika kujipendekeza wanaweza kujipa kazi ya kushughulikia watu. Kama Mfumo wa Nchi utakuwa huuhuu, ni dhahiri shahiri tutakosa ulinzi dhidi ya watu hao na pengine pia tutakosa ulinzi dhidi yako endapo nawe ukibariki kushughulikiwa kwetu.
Kwa hivyo kama kweli una nia ya dhati na 4R zako, basi hakikisha mfumo wa sasa UNAVUNJWA; na njia ya pekee ya kuuvunja ni kuandika Katiba Mpya. Katiba itakayounda Miimiri ya Dola inayochungana, na si miimiri ya sasa inayolindana. Katiba itakayounda Taasisi Imara za Haki Jinai. Katiba ambayo haitatupatia Rais Mungu. Katiba ambayo haitamwacha Rais Mhalifu atambe Ikulu atakavyo pasi na kicho wala kificho.
Dotto Rangimoto
Mshairi na Mwandishi wa Riwaya