Ukweli ni kwamba katika Uislam kuna taratibu zilizowekwa katika kuamiliana na watawala. Haifai kuminyamana na watawala. Tumeamrishwa kuwatii watawala katika yasiyo ya haramu na kuwa na subra katika dhulma ya mtawala.
Na haifai kumkosoa mtawala hadharani, anayetaka kumnasihi mtawala amshike mkono au amuandikie kwa siri amnasihi. Umekutana na mtawala uso kwa macho hapo sasa ndio umepata fursa ya kumnasihi, basi mnasihi kwa busara iwapo kama ni kweli unataka kutoa nasaha. Au muandikie. Haifai kumtukana.
Lakini haifai kuwapinga na kuwakosoa hadharani. Sikuambii kuwafanyia uasi ndio kabisa.
Na kuhusu maandamano sijui mapinduzi hayafai. Sisi tumefundishwa kuwa na subra kunako dhulma ya mtawala. Hawawi madhalimu watawala ila kwa sababu ya dhulma za raia.
Dhulma ikidhihiri miongoni mwa watu; kukajaa washirikina wanaoabudu wengine pamoja na Allah au wakawaabudu wengine badala ya Allah, au kukajaa wazinifu, wezi, wadokozi, matapeli, waonevu na wenye kupokonya haki za watu na kadhalika basi Allah atawaoneshea athari ya maovu yao kupitia watawala wao. Watayaona hayo kwa watawala wao. Hivyo wakitaka kuondolewa watawala madhalimu, basi waache wao kwanza dhulma.
Ila migomo, maandamano, uasi na mapinduzi unazidisha shari na uharibifu na kuondoa amani.
Nimeandika haya sio kwa sababu hao "dokta" Sule na Sheikh Mziwanda ni masheikh zangu. Hapana. Allah awaongoze.
Allah atuongoze katika njia iliyonyooka. Allah atengeneze mioyo ya watawala wetu, awaongoze katika njia iliyonyooka, awafanyie wepesi na awape hikma na uadilifu. Allah aidumishe amani tuliyonayo, Yaa Hayyu Yaa Qayyum. Ameen.