Mfahamu walau kwa ufupi Bernard Kamilius Membe, aliyepata kuwa waziri wa mambo ya nje katika awamu ya 4.
1. Bernard Kamilius Membe alizaliwa tarehe 9 Novemba, 1953, Rondo, Chiponda, katika Mkoa wa Lindi, akiwa ni mtoto wa pili kati wa watoto saba (7) waliozaliwa katika familia ya Mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe.
2. Kwa kabila, Bernard Membe ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya Wamwera, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama. Hivyo watoto wote saba wa familia hii ya Mzee Kamillius wamekuwa wanatumia jina la upande wa mama yao, Cecilia, yaani Membe.
3. Huyu ni mseminari kwelikweli kwani kwa asilimia kubwa alipata elimu yake huko Seminarini kama ifuatavyo
1962 – 1968: Elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Chiponda, Lindi.
1969 – 1972: Elimu ya Sekondari, (O-level) Namupa Seminary, Lindi
1973 – 1974: Kidato cha tano na sita (A-level) Itaga Seminary, Tabora.
4. Mwaka 1975 akiwa na miaka 22 tu aliajiriwa serikalini katika idara ya Usalama wa Taifa. Kutokana na kazi hii ndipo jina la Jasusi Mbobezi wakati akiingia kwenye siasa likaibuka.
5. Ukisikia wanamuita Mwana diplomasia basi ujue Membe ni kweli amepiga shule kuhusu masuala ya mahusiano ya Kimataifa. Elimu yake ni kama ifuatavyo;
1981 – 1984: Alipata Shahada ya kwanza katika tasnia ya Sayansi katika maswala ya Siasa na mahusiano ya kimataifa (Bachelor Political Science and International Relations)
1985 – 1989: Aliendelea na ajira yake serikalini katika katika ofisi ya rais
1990 – 1992: Alipata Stashada ya Uchumi, Mahusiano ya Kimataifa na Sheria za Kimataifa (Masters- Economics, International Relations and International Law)
1993 – 1994: Alirudi serikalini kuendelea na kazi kama mchambuzi za mambo ya ulinzi na usalama
6. Ni miongoni mwa wanausalama mahiri kuwahi kuwa nao nchini. Amepitia kozi mbalimbali za kijasusi ndani na nje ya nchi. Kwa kifupi ni jasusi msomi. Mwaka 1978, Ndugu Membe alipata Mafunzo ya sheria za Jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza.
7. Mwaka 2000, aliingia Bungeni baada ya kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Mtama, kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
8. Mwaka 2005, Bernard Membe alichaguliwa tena na wananchi wa Jimbo la Mtama kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Tofauti na kipindi cha nyuma, Bernard Membe alianza muhula wa pili wa Ubunge, Januari 2006, kama ‘front bencher’ baada ya kuteuliwa na rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.
9. Hata hivyo miezi michache baadae, yaani January 2007, rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua Bernard Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa baada ya aliyakuwa anashikilia wadhifa huo - Dr Asha Rose Migiro - kuteuliwa na Katibu Mkuu Baraza la Umoja wa Kimataifa na kuwa Naibu Katibu mkuu wa baraza hilo. Bernard Membe amehudu katika nafasi hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tangu 2007 hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika Wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.
10. Mwaka 2015 alichukua fomu za kugombea Urais lakini alishindwa na John Pombe Magufuli.
Mwaka 2020 aligombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ACT Wazalendo baada ya kufukuzwa CCM lakini hakufua dafu. Baadae alirejea tena CCM.
Bernard Membe enzi za Uhai wake alibahatika kuwa na watoto watatu tu ambao ni; Cecilia, Richard na Denis.