SoC02 Biashara ya nafaka (mahindi) nje ya nchi ni fursa muhimu, kuzuia ni kuikataa fursa ambayo ni adimu kuipata

SoC02 Biashara ya nafaka (mahindi) nje ya nchi ni fursa muhimu, kuzuia ni kuikataa fursa ambayo ni adimu kuipata

Stories of Change - 2022 Competition

Keryo

New Member
Joined
Sep 2, 2022
Posts
2
Reaction score
4
MAANA YA NAFAKA.
Nafaka ni mbegu zinazotokana na mimea aina ya nyasi zilimwazo mashambani kama mahindi, mtama, mpunga, ngano na hutumika kama chakula kwa ajili ya binadamu na hata mifugo.

Kumekua na kasumba ya mara kwa mara ya serikali ya Tanzania kupiga marufuku nafaka hasa mahindi kuuzwa nje ya nchi kwa ajili ya usalama wa chakula kwa wananchi wake jambo ambalo linaumiza wakulima na kuinyima serikali mapato.

Hii tabia ifike mwisho na tuangalie biashara ya mahindi nje ya nchi kama fursa ya kuchangamkia.

Ni aibu na fedheha kwa nchi kama Tanzania iliyobarikiwa na ardhi ya kilimo hekta 29.6 milioni lakini mpaka ilipofika mwaka 2012 ina eneo lisilotumika kwa kilimo la hekta 336,169 (Chanzo: World data Atlas). Tutumie ardhi vizuri kwa matokeo makubwa zaidi kwani ardhi ni mali.

Tanzania haijabarikiwa ardhi pekee; imebarikiwa ardhi yenye rutuba, misimu ya mvua miwili na mmoja kwa baadhi ya maeneo, mito na maziwa yenye maji ya kutosha. Swali ni Je? Ni nini kinatuzuia kuzalisha mahindi kwa ajili ya kula na biashara?

Hebu tuiangalie nchi ya kijangwa kama Libya ilivyoweza kubadili jangwa kuwa sehemu ya kilimo.

Libya iliwekeza kwenye mradi wa kuchimba maji ya kale (fossil water) kwa ajili ya kilimo wa dola za kimarekani bilioni 20 na kusambaza mtandao wa mipira ya kumwagilia kwa maili 2333 ili kuweza kumwangalia hekta 160,000. (Topol, S.A, The Christian Science Monitor: Tripoli, Libya 2010).

Swali ni Je? Kama Libya iliweza kufanya hivyo jangwani je Sisi Tanzania wenye kila kitu kizuri tunakwama wapi? Kupanga ni kuchagua; basi serikali inapaswa kuchagua kilimo kama sekta mama kwa vitendo kwani imeajiri watanzania wengi zaidi ambapo ikiinuka na watanzania watakua wameinuka.

HASARA INAYOTOKANA NA KUZUIA NAFAKA(MAHINDI) KUUZWA NJE YA NCHI.
a)Kuporomoka kwa bei
Mahindi yanapozuiwa kuuzwa nje ya nchi bei hushuka kwa sababu ya uhitaji (Mzunguko) wa biashara kuwa mdogo.

b)Mahindi mengine huharibika kwa kuwekwa stoo muda mrefu na kumsababoshia mkulima hasara.

_20220905_123645.JPG

Malori ya mahindi yaliyokwama mpakani Namanga baada ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Tanzania na Kenya Machi 2021 (Chanzo: DW 2021)

FAIDA INAYOTOKANA NA KUUZA MAHINDI NJE YA NCHI
a)Kuchangamsha shughuli za kiuchumi.
Wafanyabiashara wanapoenda kununua mahindi watalala nyumba za wageni, watakula mgahawani na kuongeza mzunguko wa fedha eneo husika.

b)Hutoa ajira kwa wengi
Mahindi yanapouzwa pikipiki, guta na magari hubeba mahindi na kuwapatia ajira watu wengi. Si hivyo tu madalali hunufaika sehemu ya kununulia na sehemu ya kuuzia mahindi.

NINI KIFANYIKE ILI KUONDOKANA NA MARUFUKU ZA MARA KWA MARA KUZUIA MAHINDI KUUZWA NJE YA NCHI

Kwanza nimpongeze waziri wa kilimo Mh Hussein Bashe kwa kutoa tamko kwamba hakutakua na marufuku ya kuzuia mahindi kuuzwa nje ya nchi kwani ametambua kilimo ni biashara na biashara ni fursa na mkulima anatakiwa kuneemeka na si kupata hasara.

Utazuiaje mahindi kuuzwa nje hali ambayo hushusha bei na pengine mkulima alichukua mkopo benki ili alime apate faida kinyume chake anaangukia kwenye hasara na deni lisilolipika? Hii haikubaliki kwa mtu yeyote mwenye akili.

a)Tuthamini kilimo cha umwagiliaji
Tanzania ina eneo lenye miundombinu ya umwagiliaji hekta 694,715 ilipofika 2019/2020
(Wizara ya kilimo, 2020, ukurasa wa 48);

Kati ya hekta hizo ni hekta 289,386 pekee zilimwagiliwa (Matokeo ya sensa ya kilimo 2019/2020). Juhudi zinahitaji ili kuongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji.
Kitaalamu tunaweza kufanya kilimo cha umwagiliaji na kuongeza mavuno ya uhakika kwa kutumia njia zifuatazo:

i)Maji ya mito na maziwa
Tuma mito na maziwa ambayo yangeweza kusaidia katika kilimo cha umwagiliaji, ni kitendo cha kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya kilimo cha kisasa.

ii)Kuchimba maji ardhini na kusambaza kwa mipira ili kunyeshea kwa matone. (Drip Irrigation).

Hii inaweza kufanyika maeneo yale kame kama Dodoma, Singida na itazuia upotevu wa maji wakati wa umwagiliaji kutokana na ukame uliopo na joto kali. Libya iliweza kua na mito iliyojengwa na binadamu jangwani ili kusaidia umwagiliaji; sisi ni nini kitatuzuia?

iii)Kuelekeza maji ya mvua yanayotiririka kwenye makorongo kwenda kwenye mabwawa maalumu ili kusaidia katika umwagiliaji.

Mara nyingi mazao hukosa maji kidogo ya kusaidiana na mvua ili kuwezesha mazao kukomaa; kwa hiyo serikali inatakiwa kujenga mabwawa ili kumsaidia mkulima kuweza kumwangalia kipindi ambapo mvua zinakua chache.

b)Serikali kutoa ruzuku kwa wakulima
Serikali inatakiwa kumwezesha mkulima kupata pembejeo za kilimo kama mbegu, mbolea na dawa ili kumwezesha kuzalisha zaidi na kwa tija.

HITIMISHO
Kwa kutambua fursa ni bahati na haitakiwi kuchezewa bali kukumbatiwa kwa nguvu zote; serikali kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wanaweza kuwezesha mbinu bora na za kisasa za kilimo ili kuweza kuzalisha zaidi kwa ajili matumizi ya ndani na biashara nje ya nchi bila kumuathiri mkulima na mlaji wa Tanzania. Hii itakuza pato la taifa na kuongeza ajira kwa watu wengi kwani hutegemea kilimo.

Kwa mujibu wa wizara ya kilimo 2019/2020 hekta 4,946,799 zilipandwa mahindi na kuzalisha tani 6,536,324. Kwa kuzingatia fursa na kuingia katika uzalishaji wenye tija tutazalisha zaidi ya hizo tani za mahindi na marufuku ya kuuza mahindi nje itabaki kua historia.
 
Upvote 4
Karibu kwa mjadala wadau na naomba kura yako ili andiko lifikie watu wengi na kubadili mtazamo wa watu wanaofikiri kuuza mahindi nje ya nchi ni kumuongezea mtanzania maisha magumu kwa maana ya mahindi kupanda bei badala yake waone ni fursa ya kuchangamkia na kulima zaidi. Asante.
 
Siyo vema katika Dunia ya solo huria kumpangia mtu wapi auze na wapi asiuze ili mradi tu havunji sheria na kanuni za nchi. Wangeacha biashara ifanyike bila wao kuingilia.
 
Back
Top Bottom