Wafanya biashara wa maduka ya rejareja, akija mama/baba na chupa iliyofungwa, akakupatia umpimie mafuta ya kula, usiifungue hiyo chupa, mrudishie huyo mama/baba aifungue yeye mwenyewe. Ukimrudishia hiyo chupa kama ni salama ataifungua, la sivyo atalalamika sana, mara hoo vijana wa siku hizi heshima hawana, mara hili na lile, ukweli ni kuwa hawezi kabisa kuifungua hiyo chupa, akianza kulalamika atakuwa anaondoka akisema maduka yapo mengi unafikiri ni wewe peke yako tu mwenye duka. Kumbuka siyo aina yoyote ya chupa, lazima iwe chupa ya kioo yenye mfuniko wa kujizungusha kama chupa zinazowekwa pombe kali.
Chupa za plastiki hizo hazina matatizo. Wachawi wa nchi wanatumia uchawi wao kupata pesa kwa njia za wizi, aina hii ya wizi wa kutumia majini huitwa chuma ulete. Majini haya huyatengeneza wao wenyewe, zipo aina ya majani na vitu vingi huchanganya pamoja na damu ya mnyama, huo mchanganyiko ukifikia hali fulani husomwa dua mbalimbali na machangiko huo hupatiwa jina kama Jumatatu, na kila siku mchawi anaita jina hilo mara tatu au nne akiwa karibu na huo mchanganyiko.
Baadaye hutumika aina mbalimbali za ubani na dua na ule mchanganyiko huwa ni pepo kamili, pepo hilo huingizwa ndani ya chupa kama moshi, ambao siyo rahisi kuona. Anapokupa hiyo chupa kuifungua, kawaida unapofungua chupa, unaiweka mbele karibu na uso wako, hivyo ule moshi ulio ndani ya chupa hutoka na kuingia ndani ya mwili wako.
Jumatatu akishaingia ndani ya mwili wako, mchawi akitaka kitu chochote dukani kwako atakichukua kirahisi sana. Anachofanya akifika dukani anaita tu jina la Jumatatu, lile pepo aliloliweka ndani yako huitika na kupanda, pepo likipanda wewe mwenye duka fahamu zinakutoka, analiangiza sasa nipimie mchele kilo 4, sukari kilo 1, unga kilo 5 akishapimiwa huondoka, na wewe mwenye duka huzinduka bila kujua chochote kilichofanyika, mara nyingine anaweza kuja na kuita Jumatatu nipe shilingi alfu ishirini, Jumatatu hupanda na kumpatia hizo pesa.
Hilo pepo linapanda linapoitwa na mchawi aliyelitengeneza peke yake, akija mtu mwingine na kuita Jumatatu pepo hilo halipandi kwani halimtambui.