richard amuonya latoya
MSHINDI wa shindano la Big Brother II mwaka jana, Richard Bezuidenhout, ametoa ushauri wa bure kwa mwakilishi wa Tanzania katika shindano la mwaka huu BBA 3, Latoya Lyakurya, kuwa mwangalifu na kubadili tabia yake endapo anataka kuendelea kukaa katika jumba hilo.
Akizungumza kwenye kipindi cha Jambo Afrika, kinachorushwa na Televisheni ya TBC 1, juzi, Richard alisema kwamba mshiriki huyo amezidi kuwa mapepe, hivyo apunguze.
Jambo jingine analolifanya ni kutudhalilisha Watanzania, hivyo aelewe kwamba ukiwa machachari sana, watu huchoshwa na wewe, hivyo wanaweza kukupigia kura za kukutoa kwenye jumba, alisema Richard.
Latoya ambaye amepigiwa kura za kutolewa kwenye shindano hilo, pamoja na mshiriki mwingine Tayana hatima yao iko mikononi mwa mashabiki wa nchi wanazotoka, hivyo wameombwa wawapigie kura ili kuwanusuru.
Katika hali isiyo na kificho, hatima ya Latoya kubaki BBA3 iko mikononi mwa Watanzania, hivyo wamnusuru kwa kumpigia kura kwa njia ya ujumbe mfupi, alisema Richard.
Jumapili iliyopita, Latoya na Tawana walitolewa kwenye jumba hilo na kuweka kwenye shimo la taka, ambako mmoja kati ya wawili hao atatoka na mwingine kurejea jumbani Jumapili ijayo.
Aidha watazamaji wa shindano la BBA 3, linalofanyika Johannesburg, Afrika Kusini juzi walianza kupiga kura ya kuchagua mshiriki atakayerudishwa kwenye jumba hilo kutoka katika shimo la taka, ambako wametenganishwa huku wakishuhudia kila kitu kinachoendelea kwenye jumba hilo.