CCM yamteua Rwegasira kuwania ubunge Biharamulo
Habari Nyingin
NA JOSEPH BURRA
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemteua Oscar Rwegasira, kuwa mgombea wa kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo wa Biharamulo Magharibi, mkoani Kagera. Rwegasira aliteuliwa katika kikao cha kamati kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa ameteuliwa na mkutano huo kuzindua kampeni za uchaguzi huo, zitakazofanyika Juni 13, mwaka huu. Zitafungwa Julai 4, na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Kamati ilikutana na wagombea sita walioomba kuteuliwa na Chama kuwania uongozi katika jimbo hilo.
Alisema lengo la kukutana nao ni kuweka mshikamano ili kukipatia Chama ushindi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Julai 5, mwaka huu. Rwegasira aliongoza katika kura ya maoni kwa kupata kura 309. Wengine walioomba kuteuliwa kuwania kiti hicho na kura zao kwenye mabano ni Magoha Agricola (120), Balagama Mwajemi (23), Rwabudongo Hassan (14), Matata Mussa (10) na Burchard Ntibihora (5).
Kupitia taarifa hiyo, Kamati Kuu imewaomba wana-CCM, wapenzi na wananchi wa Biharamulo kumuunga mkono Rwegasira ili ushindi upatikane. Uchaguzi huo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Phares Kabuye (TLP), aliyefariki dunia Aprili, mwaka huu kwa ajali ya gari mkoani Morogoro. Wakati huo huo, Angela Sebastian anaripoti kutoka Biharamulo kuwa, vijana wa wilaya ya Biharamulo wamepokea kwa furaha uteuzi wa Rwegasira.
Kutokana na uteuzi huo, vijana hao walifanya maandamano makubwa wakiimba nyimbo za kumpongeza. Vijana hao walisema uteuzi huo ‘umewakuna' na kilichobaki ni kumuunga mkono mteuliwa huyo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, ili aweze kuwa mbunge. Walisema wananchi wa Biharamulo wanahitaji mabadiliko, kwani wamekuwa na wabunge ambao kazi yao ni kwenda bungeni na kupokea posho bila ya kuangalia maslahi ya vijana.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Wilaya ya Ngara, Pantaleon Rumanyika, aliye Biharamulo kwa shughuli za Chama, alisema amepokea kwa furaha uteuzi huo na kwamba, wamejipanga kuhakikisha Chama kinaibuka na ushindi.