CHADEMA MATATANI BIHARAMULO
Imeandikwa na Neophitius Kyaruzi, Biharamulo
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeingia matatani katika kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Biharamulo Magharibi baada ya kukiuka taratibu za kampeni, kwa kupotosha habari kwa kutumia kibonzo kinachoonesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewakashifu wananchi wa jimbo hilo. Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Vijana wa Chadema, Mwita Waitara anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusu tukio hilo ambalo linadaiwa kuwa na nia ya kuvuruga taratibu za kampeni kwa kutoa ujumbe ambao si wa kweli.
Kamanda wa Operesheni ya Upelelezi ambaye pia ni Mkuu wa Polisi wa Kuzuia Ghasia Tanzania (FFU), Tresphory Anaclet alithibitisha kukamatwa kwa Waitara na kuhojiwa. Viongozi wa Chadema wilayani hapa, wanatuhumiwa kushirikiana na kuondoa maelezo halisi ya kibonzo kilichotolewa katika gazeti la Sauti Huru toleo namba 34, na kuweka maelezo yao yanayoidhalilisha CCM, kukashifu wapiga kura kisha kudurufu maelezo hayo waliyopotosha na kuyasambaza katika mji wa Biharamulo na maeneo mengine.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mnyika alikiri kupata taarifa hizo na kukamatwa kwa Waitara na kisha kuhojiwa na polisi, lakini alikana Chadema kuhusiana na tuhuma hizo huku akidai kuwa hizo ni fitina zilizotengenezwa na CCM ili kukidhalilisha chama hicho.
Sisi ni chama makini na tunajua taratibu za uchaguzi na sheria zinazotuongoza hatuwezi kufanya upuuzi kama huo, jambo hilo litakuwa limepandikizwa na CCM ili kutudhalilisha, alisema Mnyika. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kupitia mahojiano na wananchi mbalimbali, unaonesha kwamba magari ya kampeni ya Chadema yamekuwa yakipita mitaani na kusambaza nakala zilizodurufiwa zinazoonyesha ujumbe uliopotoshwa katika gazeti hilo.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara maarufu mjini hapo, John Rwegasira ambaye pia ni mhamasishaji wa Kampeni wa CCM, takribani siku ya tatu sasa Chadema kimekuwa kikikodi waendesha pikipiki na kupeleka nakala za maelezo ya upotoshaji katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo. Alisema kwamba baada ya CCM kupata taarifa na kushuhudia nakala hizo, ilipeleka taarifa katika vyombo vya usalama ili suala hilo lishughulikiwe.
Naye Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alidai kuwa fitina hiyo ya Chadema ni dalili za kutojiamini kwao katika uchaguzi huo baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Busanda uliofanyika hivi karibuni na CCM kupata ushindi. Alisema Chadema sasa kimejaa ubinafsi na ubabaishaji ndio maana ilifikia hatua ya kutangaza chama chake cha TLP kutosimamisha mgombea wakati si kweli.
Nataka niwaambie wananchi wa Biharamulo na Watanzania wote kwamba Chadema ni chama kilichojaa ubinafsi na ubabaishaji wa hali ya juu kwani kinataka kujifanya kiranja wa vyama vingine vya upinzani wakati kinajua wazi kimepoteza mwelekeo, alisema Mrema. Alisema kwa mwenendo unaoonekana sasa, Chadema haina uwezo wa kushindana na CCM na kunyakua majimbo, lakini imeendelea kuvishawishi vyama vingine vijitoe wakati havina uwezo na baada ya kushindwa ni ushahidi tosha. (tamati).
CCM yafanya kampeni kwa mbwembwe Biharamulo
Frederick Katulanda, Biharamulo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) juzi jioni kilifanya kampeni zake huku Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho, Mfaume Kizigo akitangaza kuwa vijana wake wako tayari kuwashughulikia watu watakaoleta vurugu kwenye jimbo hilo.
Mkutano huo wa kampeni za CCM ni wa kwanza kufanyika katika mji wa Biharamulo mjini tangu Juni 10 mwaka huu, kampeni zilipoanza ambapo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndicho kilikuwa cha kwanza kufungua kampeni zake katika mji huo, wakati CCM ilizindulia katika mji wa Nyakanazi.
CCM ilifanya mkutano huo siku moja baada ya Chadema kuitisha mkutano wa wandishi wa habari katika ofisi yake ambapo ilikilalamikia Chama Cha Mapinduzi na polisi kwa tuhuma za kuuhujumu uchaguzi huo.
Hata hivyo juzi hiyo, vijana wa CCM walianza hamasa saa 12: 15 aubuhi , baada ya kundi la vijana wapatao 35 kupita katika kona za mji huo wakikimbia mchakamchaka na kuimba nyimbo za mafunzo ya mgambo huku wakiwa wamevalia sare za CCM.
Ilipotimu saa 6:20 mchana, kundi lingine la vijana 20 likiwa na bendera ya Chama hicho, lilianza kupita tena, likikimbia mchakamchaka, huku likiimba nyimbo zenye maneno mengi ya kuchekesha yakiwemo ya "Tutawashughulikia wapinzani mpaka wakione cha moto na mgombea wake apandwe presha ama aharishe.
Wakati kundi hilo likiendelea, mkuu wa kitengo cha propaganda Tambwe Hiza yeye alikuwa akisaidiana na baadhi ya vijana wengine wa chama hicho kugawa
Magazeti ya 'Sauti huru na Nyundo' ambayo yalichapishwa habari nyingi za kuviponda vyama vya upinzani.
Mkutano wa CCM ulianza saa 9:30 ambapo wa kwanza kupanda jukwaani alikuwa Kizigo ambaye alisimama na kusema kuwa yeye kama mkuu wa vijana wa chama hicho hayuko tayari kuiacha Tanzania huru na Biharamulo ikichafuliwa amani na vijana wa Chadema na hivyo kusema vijana wa chama chake wamejipanga kikamilifu.
Alisema Jana Chadema wamefanya mkutano hapa wakasema kuwa tunawamwagia tindikali, tuna mapanga na tunatembea na magobole, sasa nataka kuwaeleza kuwa CCM ni chama cha amani lakini hatuko tayari kuona vurugu na vijana wangu watawashughulikia wakianza vurugu, alifafanua.
Naye mbunge wa Bukoba Mjini Balozi Hamisi Kagasheki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, alisema CCM imekuja kwa heri kugombea katika jimbo la Biharamulo na kuwataka wananchi kuepuka vurugu na matusi ambayo alidai kuwa yamekuwa yakitolewa na vyama vya upinzani kwa kumchagua mgombea wa CCM.
Mkiona watu wanakuja kwa shari na matusi mjue kuwa hao wameishiwa sera na wamefilisika, mimi nimekuja kwa niaba ya wabunge wote wa CCM mkoa wa Kagera kuwaomba mtuchagulie mgombea Oscar ili tuweze kuwaletea maendeleo, alieleza.
Kagasheki alisema yeye alimfahamu mgombea huyo tokea akiwa nchini Holland alikokuwa akisoma na kwamba ndiye aliyemshauri kurudi Biharamulo kugombea na kumwelezea kuwa ni kijana makini na msikivu ambaye anapaswa kuwa mbunge.
Akizungumza kumnadi mgombea wa chama chake Naibu Katibu Mkuu wa CCM George Mkuchika, alisema mgombea wake amekuwa tishio kwa Chadema, jambo ambalo liliwafanya kumsingizia kuwa siyo raia ya Tanzania ili aenguliwe uwanja wa uchaguzi kwa kumhofia kuwa atawashinda.
Naye mgombea wa CCM, Oscar Rwegasira Mukasa akijinadi kwa wapiga kura alieleza kuwa jimbo la biharamulo kwa sasa linahitaji mbunge kutoka CCM kwa vile kwa muda limekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na kuwa na mbunge wa upinzani na hivyo kuwaomba wananchi wamchague yeye kwa vile amedhamiria kuwaletea maendeleo kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa CCM mkoani Kagera.
Alisema iwapo watamchagua yeye ataanza kushughulikia suala la maendeleo kwa kusimamia mpango wa maendeleo wa Halmashauri ya wilaya ikiwa ni pamoja na kukutana na walimu wa shule ambao alidai kuwa wamekuwa wakifundisha katika mazingira magumu..
Alisema mbali na suala la walimu atahakikisha kuwa vijana wanapata fursa ya kukopa katika taasisi za mikopo kwa kushirikiana na wizara husika na kuwasihi wananchi kuhakikisha wanamchagua yeye kwa vile ni mgombea wa CCM yenye ilani ya uchaguzi inayotekelezeka.
Mkutano huo wa CCM ulihitimishwa kwa maandamano ambapo viongozi wa CCM waliwatangazia wananchi kuwa baada ya mkutano huo wananchi wamsindikize mgombea wao ambaye atatembea kwa mguu kuelekea ofisi za chama.
Source:
Mwananchi Read News