Bongo fleva ina miaka 30? Kulikuwa na kwanza unit ya akina D knob na Niga one

Bongo fleva ina miaka 30? Kulikuwa na kwanza unit ya akina D knob na Niga one

Fahari ya kusini

JF-Expert Member
Joined
Nov 26, 2022
Posts
545
Reaction score
1,908
HAPO ZAMANI
_______________

Vichwa viwili muhimu katika historia ya muziki wa Hip Hop nchini ambapo chimbuko lake ndilo lililozaa muziki wa Bongo fleva, Adili Kumbuka (Nigga One) na Robert Mwingira (D-Rob). Wakali hawa walikuwa Marapa wa kundi la Kwanza Unit, na wawili wote kwa sasa ni marehemu.

Wakati Adili akifariki dunia kwa ajali ya gari mwaka 1993, Miaka 8 baadae Rapa D Rob naye akafariki dunia kwa kuugua. Matukio haya mawili ya vifo vya Adili na D Rob yameendelea kuwa pigo kubwa katika historia ya kundi la Kwanza Unit na historia ya muziki wa Hip Hop nchini.

ADILI

Adili ndiye "Baba" wa Kwanza Unit, akichagiza kuundwa kundi hilo kutoka kwenye makundi mengine kadhaa ili kutengeneza kundi moja litakalokuwa na nguvu na kufanya mapinduzi ya kuupeleka mbele muziki na utamaduni wa Hip Hop ambao ndiyo kwanza ulikuwa umeanza kuchipua.

Akiwa kwenye kilele cha mafanikio kutokana kuwa mmoja wa washindi wa mashindano ya "Yo Rap Bonanza", Adili aliyekuwa Rapa wa kundi la "Raider's Posse" alikutana na wakali kutoka makundi mengine ya "Villain Gangsters", "Rapports", na "Tribe X" kisha kuvunja makundi hayo na kuunda kundi moja liitwalo "Kwanza Unit"

Kwa bahati mbaya, Adili alifariki dunia kabla ya Kwanza Unit kurekodi wimbo wake wowote, na hivyo sauti yake na uwezo wake kubahatika kuonwa na wale tu waliowahi kumshuhudia akichana 'live' kupitia matamasha mbalimbali ya Rap ya wakati huo. Aendelee kupumzika kwa amani Rapa Adili Kumbuka (Nigga One).🙏

***************

Wakati Kwanza wakiianza safari mpya bila ya Adili, haikuweza kuwa rahisi kubaini kama kundi hilo limepata pengo kufuatia kifo cha mtu muhimu kwao. Hii ni kutokana na ukali wa Marapa waliokuwa wakiunda kundi hilo kuwa mahiri tangu walipokuwa kwenye makundi yao ya awali.

Kwanza Unit iliundwa na Marapa Ramadhan Mponjika (Chief Rhymson), Kibacha Singo (KBC), Robert Mwingira (D-Rob), Bernard Mloka Luanda (Easy B), Godfrey Koshuma (Fresh G), na Yunus Lameck Mligiliche (Y-Thang). Hii ndiyo Kwanza iliyosimama imara baada ya kifo cha Adili.

Lakini Kwanza halikuwa kundi la Marapa tu, bali ilikuwa na familia iliyounganisha vichwa vingine nje ya jukwaa ikijulikana kama "Kwanza Foundation". Familia hiyo ilijumuisha vichwa kama Khalid na Mahadia Kumbuka ambao ni ndugu wa damu wa marehemu Adili Kumbuka (Nigga One).

Wengine ni pamoja na Edward Magaye (Bugs Malone), ML Chris, Ndoti Mwingira, Abbas Maunda, Makanga Lugoe (Papa Sav), Baraka, Gaddy, na wengineo wengi ambao waliifanya Kwanza kuwa "Supreme" haswa katika nyakati ambazo hakuna kundi lililothubutu kutia pua mbele yao.

*****************

D ROB

Kifo cha Rapa Robert Mwingira (D-Rob) kilikuwa ni tukio la pili la huzuni kuwahi kulikumba kundi hilo katika historia yake. D Rob alikuwa moja ya nguzo imara za Kwanza Unit akishiriki hatua zote muhimu za historia ya kundi hilo kuanzia albamu yao ya kwanza iitwayo "Kwanza Unit" ya pili "Tropical Technique" na ya mwisho "Kwanzaniaz".

Sauti yake ya mwisho kusikika ni katika wimbo wa Lady Jaydee uitwao "Mpenzi Wangu" ambao marehemu D-Rob amechana kwa umahiri mkubwa katika ubeti wa mwisho wa wimbo huo na hivyo kuwa moja ya kumbukumbu za mwisho sauti ya mmoja kati ya Marapa bora kuwahi kutokea Tanzania.

Wimbo wa "Msafiri" ni moja kati tungo mahiri ambazo D Rob amechana kwa ubora wa hali ya juu katika verse ya pili, akimpokea Chief Rhymson baada ya kumaliza verse ya kwanza. Tungo kama "Nakuja", "Kwanzaniaz ", "Beyond Belief", "So Why?" na nyingine nyingi zinadhihirisha ukali wa mwamba huyu aliyefariki dunia mwaka 2001.

Mpaka leo katika historia ya Kwanza Unit, vifo vya Adili Kumbuka (Nigga One) na Robert Mwingira (D-Rob) vimeendelea kubaki kama moja ya kumbukizi za kuumiza sana kuwahi kulikumba kundi hilo katika historia yake.

Continues to Rest in Heaven, Adili & D-Rob. 🌹
Ahsante sana Rapa Joseph Osmund Mbilinyi (Sugu) kwa dedication yako kwa Legends hawa kupitia kibao chako hiki cha "Zamani". Hakika tutaendelea kuwakumbuka ni historia haitoweza kuwasahau daima.
 
Back
Top Bottom