Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga ametambulishwa mbele ya waandishi wa Habari leo Septemba 27, 2023 na kuelezea kuhusu mipango ya shirika hilo na kugusia kuhusu changamoto ya umeme.
Kuhusu changamoto ya umeme Nchini, amesema “Tunatarajia hadi kufikia mwishoni mwa Machi 2024 tatizo hilo litakuwa limekwisha kwa kuwa tunatarajiwa kuwa tumekamilisha matengenezo yanayoendelea ya mitambo pamoja na visima vinavyotoa gesi asilia.
“Tunayo matarajio kuwa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakapoanza kuzalisha umeme matataizo haya yatakuwa yamekwisha kabisa.”
Amesema Shirika linaendelea kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 ambao mpaka sasa umefikia 92%.
Ameeleza pindi mradi huu utakapokamilika na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa utachangia kuimarika kwa hali ya umeme nchini kwa kiasi kikubwa
============= ===============
TAARIFA KAMILI YA TANESCO KUHUSU UPUNGUFU WA UMEME
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linautaarifu umma kuhusu changamoto ya upungufu wa umeme katika vituo vyetu vya uzalishaji umeme nchini. Upungufu huo unachangiwa na ongezeko la mahitaji ya umeme kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi, upungufu wa maji kwenye vituo vya kufua umeme unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na matengenezo yanaoendelea kwenye visima vya gesi asilia na mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia. Kufuatia hali hiyo, baadhi ya maeneo nchini yamekua yanakosa huduma ya umeme kwa nyakati tofauti.
Shirika limepokea na tayari limeanza kutekeleza maagizo yaliotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati na tayari jitihada mahususi za ukelazaji za kukabiliana na changamoto hii zimeanza, kwa kuharakisha matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme na matengenezo ya visima vya gesi asilia kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Ni matarajio yetu kuwa ndani ya mwezi oktoba kukamilika kwa matengenezo hayo kutawezesha kupata nafuu ya makali ya upungufu wa umeme na ndani ya miezi sita kuhakikisha tunaondokana na kadhia hii ya upungufu wa umeme.
Vilevile, Shirika linaendelea kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115 ambao mpaka sasa umefikia asilimia 92. Pindi mradi huu utakapokamilika na kuingizwa kwenye gridi ya taifa utachangia kuimarika kwa hali ya umeme nchini kwa kiasi kikubwa.
Shirika linawashukuru wateja wake na kuwa omba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito na kwamba shirika litaendelea kutoa taarifa za upatikanaji wa umeme kwa kadri hali itavyozidi kuimarika. Taarifa hizi zitatolewa kupitia vyombo vya habari mbalimbali, mitandao yetu ya kijamii, tovuti rasmi ya Shirika na Ofisi zetu zilizopo katika Mikoa na Wilaya nchini.
Imetolewa Na;
OFISI YA KURUGENZI MTENDAJI TANESCO- MAKAO MAKUU. DODOMA
OFISI YA KURUGENZI MTENDAJI TANESCO- MAKAO MAKUU. DODOMA