MDHAMINI wa Yanga Yusuf Manji ameahidi kuwanunulia tiketi ya kushuhudia mechi ya kirafiki kati ya timu ya soka ya Taifa Taifa Stars na Brazil inayotarajiwa kuchezwa Juni 7 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Manji aliahidi hayo jana kwenye barua yake kwenda kwa Katibu wa Yanga Lawrence Mwalusako kuhusu kusaidia mkutano mkuu wa wanachama unaotarajiwa kufanyika Juni 6 kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi Osyterbay.
Hata hivyo katika barua yake hiyo Manji alisema wanachama watakaopewa tiketi ni wale watakaohudhuria mkutano huo tu.
Manji alikuwa akijibu barua aliyoandikiwa na uongozi wa Yanga kumuomba kugharamia mkutano huo wa kupitisha rasimu ya Katiba.
Manji alisema kwa vile Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewaomba wananchi kusaidia gharama za kuileta Brazil nchini kwa njia ya viingilio, hana budi kama mdau kufanya hilo kwa kuwalipia wanachama wa Yanga.
Rejea barua yako ya Mei 27 2010 yenye kumbukumbu namba YASC/165/LPM ikinikumbusha barua niliyopokea mapema mwaka huu kutoka kwa Mwenyekiti Iman Madega akiniomba kugharamia mkutano barua ilikuwa ya Machi 16, 2010 kumbukumbu namba YANGA/CM/10/010.
Sasa nimefahamishwa juu ya mkutano huo na nitagharamia yafuatayo, nitalipia ukumbi, nitagharamia usafiri wa wanachama kutoka klabu mpaka eneo la mkutano na kuwarudisha, kwa hiyo nitaandaa mabasi ambayo yatakuwa klabuni asubuhi kuchukua wanachama, nitalipa posho kwa maofisa wa serikali watakaokuwepo kwa ajili ya mkutano huo
Pia nitanunua tiketi kwa wanachama wote wa Yanga watakaohudhuria mkutano huo kushuhudia mechi ya kihistoria kati ya Taifa Stars na Brazil, ilisema sehemu ya barua hiyo.
Brazil inatarajiwa kuwasili nchini Juni 6 usiku na baada ya mechi yake ya Jumatatu itaondoka kurejea Afrika Kusini inakojiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia inayotarajiwa kuanza Juni 11.
Brazil ipo Kundi G katika michuano ya Kombe la Dunia ikiwa na timu za Jamhuri ya Watu wa Korea, Ivory Coast na Ureno.
Itarusha kete yake ya kwanza Juni 15 dhidi ya Korea kwenye Uwanja wa Ellis Park Johannesburg.
Tanzania itakuwa imepata ugeni mzito kwa mara ya pili katika soka wa kwanza ulikuwa ni ule wa Ivory Coast iliyokuwa Januari ikielekea Angola kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika.
Chanzo: Habari leo