Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA} inapenda kutoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu kampuni inayoitwa Kalynda E-Commerce Limited baada ya kuona na kupokea malalamiko kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa biashara inayofanywa na kampuni hii.
Kampuni ya Kalynda E-Commerce Limited ilisajiliwa tarehe 14 Juni, 2022 na kupewa cheti cha usajili Namba. 156483877. Kwa mujibu wa katiba ya kampuni (Memorandum and Articles of Association) shughuli kuu za kampuni ni pamoja na;
1. Uuzaji wa jumla wa vifaa vya kielectroniki na mawasiliano,
ii. Ufanyaji wa biashara ya kitekinolojia ya kimataifa mtandaoni.
Vilevile, Kalynda E-commerce Limited ilipata Leseni ya Biashara tarehe 21 Juni, 2022 yenye Namba 20000031405 ambayo itaisha muda wake wa matumizi tarehe 20 Juni, 2023. Leseni iliyotolewa ni ya kufanya biashara ya masoko na mauzo ya bidhaa kwa njia ya mtandao pekee (Online Marketing and Sa/es).
Wakati wa uwasilishaji wa maombi ya usajili wa Kampuni na Leseni ya Biashara taarifa zilizowasilishwa zilionesha ofisi ya Kalynda E-commerce Limited zipo Kiwanja Na. 9, Mtaa wa Kaunda, Kata ya Msasani Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa zisizo rasmi zinazoleta taharuki kwenye jamii kuwa Kalynda E-commerce Limited imekuwa ikifanya bias hara ya Upatu "Pyramid Business" ya kukusanya fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kupata faida ndani ya muda fulani kinyume na bidhaa au huduma iliyoombewa na kupata leseni ya biashara.
Leseni ya Biashara ya Kalynda E-commerce Limited inamruhusu kufanya biashara ya masoko na mauzo ya bidhaa kwa njia ya mtandao pekee (Online Marketing and Sa/es). Ufanyaji wa biashara kinyume na leseni iliyotolewa ni kosa la jinai chini ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Leseni za Biashara, Sura Na. 208.
Wakala inapenda kutoa angalizo kwa umma kuwa kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya kibiashara na kampuni yoyote ni vema kupata uthibitisho wa uhalali na uwepo wa kampuni hiyo pamoja na biashara husika kutoka BRELA na Mamlaka nyingine za Serikali. Taarifa zote za Makampuni na Leseni za Biashara Kundi "A" zinapatikana kupitia tovuti
www.brela.go.tz au ofisi za BRELA.
Hivi karibu kumekuwa na matukio ya baadhi ya watu wasio waaminifu kughushi vyeti vya Makampuni, Majina ya Biashara na Leseni za Biashara kwa lengo ovu la kuwatapeli wananchi. Baadhi ya vyeti vilivyogushiwa ni pamoja na Kopa Fasta Company Limited, Champion Investments na Afric. Taarifa zimeshatolewa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya hatua za kijinai.
BRELA inapenda kuukumbusha Umma kutojihusisha na Taasisi zinazofanya baishara za upatu "Pyramid Business" kwani ni kinyume cha sheria za nchi.