BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeonyesha kusikitishwa na kutochukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wabadhirifu wa Sh63.4 bilioni katika utoaji wa tuzo ya zabuni za uboreshaji wa Bandari ya Tanga kwa Kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) Ltd.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge, kuhusu mapendekezo ya Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/2021.
Kaboyoka amesema azimio hilo halijatekelezwa kama Bunge lilivyoagiza kwa kuwa imepita muda mrefu bila hatua za kisheria kuchukuliwa kwa suala la ubadhirifu katika zabuni ya upanuzi wa bandari ya Tanga.
Amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamepokea taarifa ya ukaguzi maalumu kwa takribani miezi saba iliyopita hivyo walitakiwa kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.
“Serikali imeliwasilisha suala hili Takukuru kwa ajili ya hatua za Kisheria. Ili kujua hatua iliyofikiwa, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imefuatilia Takukuru na kuelezwa kuwa suala hili linaendelea kufanyiwa kazi na Ofisi hiyo,”amesema.
Amesema kamati hiyo ilifahamishwa kuwa na CAG kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Juni 2021 aliomba kufanyika ukaguzi wa kiuchunguzi na kuainisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka uliofanywa na watumishi wa TPA katika utoaji wa tuzo ya zabuni za uboreshaji wa Bandari ya Tanga kwa Kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) Ltd.
Amesema ukaguzi huo ulikamilika na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma takribani Sh64.30 bilioni ambayo ni hasara kwa Serikali.
Amesema Takukuru walipewa matokeo ya ukaguzi huo na hivyo Bunge liliazimia Serikali ichukue hatua za kisheria kwa makampuni na watumishi wote wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) waliotajwa katika taarifa ya ukaguzi huo maalum.
MWANANCHI