NJIA PANDA ZA KUZIMU - 2
Akanilipa shilingi mia moja, Mungu wangu eeh yule mtu alikunywa yale maji yanayofanania na damu kabisa, alikunywa huku akinilalamikia kuwa huenda yale maji hayajachemshwa.
Akanywa ule mfuko mmoja akamaliza akaongeza mwingine, nilitamani kusema neno lolote lakini huwezi amini kila nikitaka kusema sauti inakwama kabisa. Na sauti inapokwama yule dada ananigeukia na kunitazama kwa jicho kali sana.
Tulizunguka kule Kariakoo kwa takribani masaa manne kama sikosei tukawa tumemaliza kuuza yale maji ambayo si maji bali uchafu unaofanana na damu.
Hapa naomba niseme kitu mpenzi msomaji, yaani tangu nifanikiwe kuwa huru tena haya maji yanayoitwa ya kandoro siwezi kunywa nipo radhi kubaki na kiu lakini sio kunywa maji yale. Simaanishi na wewe hapo usinywe la hasha lakini wanasema kuwa usiloliona huwezi kuliogopa.
Mwenzenu niliona…
Wale watu ambao mchana walinunua uchafu ule na kunywa kama maji ndio haohao ambao usiku walikuwa wanaletwa kwa ajili ya kulima mashamba. Na walikuwa wanalima kweli.
Kidogo kidogo nikazoeana na yule dada na hapa ndipo nilipoyajua machafu mengi ambayo yananikera hadi leo kwa sababu hayataki kutoka katika kichwa changu.
Kule tulipokuwa hapakuwa na saa hivyo nitakuwa muongo nikielezea tukio kisha niseme ilikuwa saa fulani, yaani ile ilikuwa ni dunia ya wenyewe siku ambayo wa kujiita malikia ambaye bila shaka alikuwa ndiye yule mama mkwe wake Nasra akiamua tu hakuna kulala basi siku hiyo hamtaliona giza. Na siku watu wakimkera analeta giza hata siku tatu.
Kuna siku tulienda kariakoo kuuza yale maji mfanowe damu, tukarejea na maji kama pakiti tano hivi tukamueleza kuwa watu hawajanunua sana maji siku hiyo kuna mvua kubwa ilikuwa imenyesha.
Akatuuliza kwa upole sana ikiwa tunafahamu nini maana ya mvua, tukakubali kuwa tunaifahamu mvua vizuri.
Akacheka kidogo kisha akatuuliza nini maana ya mvua.
Tukabaki kimya tusijue ana maana gani kutuuliza lile swali, tulipokosa jibu akatuambia atatupa jibu baada ya muda mchache.
Akaondoka na kuingia ndani akaufunga mlango wake wa maajabu ambao unaonekana wakati wa kufunguliwa na kufungwa tu. Nyumba haionekani wala vilivyomo ndani. Yule dada aitwaye Adella ambaye ndiye ali9kuwa mwalimu wangu katika maisha yale mapya aliwahi kunieleza kuwa ndani ya ile nyumba kuna vito vingi sana vya thamani na samani zenyewe pia ni nyingi.
Baada ya kuingia ndani anga ilianza kutanda na kuwa nyeusi, tukadhani kuwa kama kawaida alikuwa ametupa adhabu ya kuleta giza siku tatu. Lakini hili halikuwa giza, mara ngurumo zikasikika na hapo mvua kubwa ikaanza kushuka.
Cha kushangaza mvua hii ni kama ilikuwa ikinyesha na kuingia katika beseni, yaani9 kila ilivyokuwa inanyesha maji yalizidi kuongezeka kwa kasi. Na wakati huo ile anga ikisogea taratibu ili ikutane na maji yale, Adella hakuwa vizuri sana katika kuogelea lakini mimi nilikuwa mtaalamu nilijitahidi sana kumsaidia Adella ili asinywe maji yale ambayo yangeweza kumsababishia kifo ikiwa angekunywa sana. Nilijaribu sana lakini baadaye tulikuwa tunaikaribia anga iliyokuwa inatema maji kwa wingi.
Sasa hapo sikuwa na namna yoyote nilifumba macho kukisubiri kifo, Adella naye alikuwa kimya akitumbua macho kuitazama ile anga ilivyokaribiana na uwepo wetu.
Ilikuwa hali ya kutisha sana.
Ghafla yale maji yakaanza kukauka tukaanza kushuka chini kwa kasi.
Tulipotua ardhini palikuwa pakavu kabisa na pembeni alikuwa amesimama yule malkia akiwa na beseni dogo tu.
‘’hiyo ndo maana ya mvua, je imenyesha mvua kubwa na ya kutisha kama hiyo…’’ alituuliza huku akitabasamu na kuondoka zake.
Ndugu msomaji, uchawi upo kama hauamini ni bora uamini tu lakini kamwe usijiingize katika shirki kwa sababu haimpendezi Mungu hata kidogo.
Yaani ardhi ile ilikuwa kavu kabisa na wenzetu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
‘’alituweka kwenye beseni’’ yule dada akaniambia likiwa ni neno lake la kwanza kunieleza kisha akaendelea.
‘’asante sana kwa kuniokoa wewe ni rafiki yangu kuanzia sasa..’’ aliniambia kwa sauti iliyojaa upole.
Na neno lile ndilo lililozua kizaazaa.
Neno lile likaujenga ukaribu zaidi baina yetu akaniahidi kuwa ipo siku tutatoka na kuishi duniani kama mtu na mke wake.
Mapenzi yakanza katika ardhi nisiyoielewa.
Adella alikuwa akinieleza mambo mengi sana ambayo amewahi kuyafanya, yalikuwa ya kutisha sana lakini aliniambia kuwa wanaotakiwa kutishika ni wale ambao wanaishi duniani sio mimi kwa sababu muda wowote ule nitatumwa kufanya kazi. Na nisijidanganye kuwa itakuwa rahisi kutoroka.
‘’Hivi wewe unadhani kwa nini ukiwa kariakoo haukimbii ukatoroka au huwa hauzioni gari za kwenda Temeke zimejaa pale shule ya uhuru… nikupe onyo yaani usije ukathubutu kutoroka kwa njia nyepesi kama hizo utajikuta matatani sana… acha kabisa Martin…’’ alinipa maonyo ya ajabu ajabu.
Ni kama vile alikuwa amenitabiria kuwa kuna kazi naenda kupewa katika siku hizo za karibuni.
Tulikuwa kama pacha vile na yule malkia alionyeshwa kupenda tunavyofanya kazi kwa ushirikiano.
Siku hiyo alituita na kutueleza kuwa kuna sherehe kubwa sana inatarajiwa kufanyika ndani ya siku saba zijazo akatueleza kuwa kila kitu kipo lakini hakuna msanii mzuri ambaye atatumbuiza katika hizo sherehe.
Na hapo akatuagiza kwenda kutafuta msanii ama wasanii wawili ambao watatumbuiza katika hiyo sherehe. Nilistaajabu sana lakini kwa sababu yule ADELLA alikuwa mkongwe hakustaajabu.
Na siku hiyo alinieleza kuwa ukiwa mzembe tu na usiyejishughulisha unaishia kuwa msukule ama unauzwa na ukiuzwa unaweza kuishia kuliwa nyama ama kufanywa kiti.
Maneno ya adella yalinichanganya sana kwa sababu yalikuwa mengi na yalikuwa yanatisha.
Usiku tuliondoka kama kawaida tulipofika mahali akanizaba kibao kikali sana mgongoni na kujikuta tupo katika ukumbi ambao nilikuwa naufahamu vyema na msanii aliyekuwa anatumbuiza pale jukwaani nilikuwa namfahamu, nilishtuka sana kujikuta ndani ya ukumbi ule na nilihisi kuwa muda si muda nitakutana na watu ambao nilikuwa nawafahamu.
Adella aliniacha nikiwa katika kona moja ya ukumbi, akajichanganya na baadaye nikamuona akimtuza yule msanii, alimrushia matawi matawi watu wakawa wanapiga kelele kumpongeza.
Hatimaye yule msanii akamuamuru adella apande jukwaani.
Adella akageukia upande niliokuwa nimesimama na kunifanyia ishara ya dole gumba, yule msanii alimkumbatia adella huku mapigo ya muziki yakiendelea.
Sijui ni mimi pekee niliyeliona tukio lile ama kila mtu aliona, huenda niliona mimi mwenyewe maana wangeona watu wengine lazima wangepiga kelele tu.
Wakati anamkumbatia adella alimfunga msanii yule kitu kama hirizi nyekundu kiunoni. Walipoachana akabaki na ile hirizi.
Akili zangu ni kama zilikuwa zinarejea hivi, nikajiona mjanja sana kuwa siwezi kuendelea kuishi maisha yale.
Nikajichanganya na kutoka nje ya ukumbi, huko nikaanza kuzubaa ni wapi nielekee kwa sababu sikuwa na nauli na pale nilipokuwa paliwa ni umbali mrefu sana hadi kufika nyumbani.
Siku hii ndipo nilizidi nkukiri kuwa ikiwa wewe ni mjanja basi kuna mjanja zaidi yako.
Nilizurura hapa na pale naingia hapa natokea kule na kujikuta nikiwa palle nilipoanzia awali.
Muda ulizidi kwenda hadi pakakucha, naziona gari najishauri kupanda lakini sipandi, natembea hadi huko na kurudi palepale,.
Kama ni adhabu basi ile ilikuwa ni adhabu kubwa sana, nawaona watu ninaowafahamu nikiwaona nakimbia na kujificha wakiondoka najishangaa ni kwanini sikiwakimbilia na kuwaeleza yote yaliyonitokea.
Hatimaye njaa ikaanza kuniuma, mchana jua kali akili inakuwa nzito kufanya maamuzi. Ilikuwa baada ya siku mbili nikiwa naishi kama kivuli nazurura huku na kule na hakuna anayenijali. Hatimaye baada ya siku mbili nikapata mwanamke wa kwanza kabisda kunisaidia.
Huyu alinichukua na kuniuliza nilikuwa nina matatizo gani, alikuwa ni mama mtu mzima anayejiheshimu, alinieleza kuwa amekuwa akiniona pale kwa siku mbili. Akanipeleka hadi nyumbani kwake, nikasema kuwa hatimaye nilikuwa nimepata msaada thabiti, alinipatia nguo nikabadilisha na kisha akanipatia chakula, baadaye akanieleza kuwa yeye ni mjane na watoto wake wote wameenda shule hivyo kwa wakati huo alikuwa akiishi mwenyewe.
Nilimpa pole na kumsihi kuwa anisaidie nauli niende nyumbani kwetu akaniahidi kuwa siku inayofuata nitaenda nyumbaji. Nyumba yake ilikuwa nzuri ya kupendeza sana hakika alikuwa amejipanga mama yule.
Usiku alinionyesha chumba ambacho ningelala ili siku ifuatayo niende nyumbani.
Nikaingia na kujifungia nikasinzia.
Baadaye usiku mnene nikahisi joto kali sana, nikatoa shuka, bado joto kali, nikatoa nguo nikaona si vibaya nikilala mtupu.
Ndugu msomaji katika hili uwe makini, hali kama hii ikikutokea usiku muite MUNGU wako akusimamie. Mimi nilichukulia kuwa hali hii ilikuwa ya kawaida sana kumbe nilikuwa nawekewa lile joto ili nivue nguo kwa hiari.
Nilipobaki mtupu nikasinzia, eti bila sababu nikaanza kumuota yule mama aliyenisaidia, nikamuona akinikumbatia huku akiwa yu uchi wa mnyama, nikawa naifurahia hali ile joto nalo likazidi. Baadaye nikajikuta nipo katika kuzini na mama yule.
Nilipokuja kushtuka nilihisi kuna harufu kali ya marashi pale chumbani. Na nilikuwa natokwa jasho haswa…..
Nilitapatapa huku na kule kisha nikalala tena hoi.
Asubuhi na mapema nilimsikia yule mama akiniita, nikavaa nguo zangu na kutoka nje hadi alipokuwa.
Alinipokea kwa tabasamu zito kisha akanieleza kuwa yeye alikuwa anataka kutoka akanipatia nauli na kunieleza kuwa nikifika nyumbani nimsalimie mama yangu.
Nikaipokea nauli, akanifungulia mlango nikatoka nje.
Ebwana eee, ukisikia wabaya watu wanyama wanasingiziwa ndo hii.
Nilijikuta nipo katika ardhi ileile ya maajabu.
‘’ulienda kwa huyo mama kufanya nini siku mbili zote hizi..’’ ilikuwa sauti ya adella akiniuliza kwa hasira kali. Nilikuwa nimepigwa na bumbuwazi nisijue ni kitu gani cha kujibu.
Yaani akili haikuwepo kabisa, yaani kumbe kumuamini kote kule yule mama alikuwa ndo yule malikia.
Nilitamani kusema neno lakini kabla sijaongea lolote adella aliita jina la kitu nisichokijua, kisha yeye akaondoka zake.
Mama yangu, akaja yule fisi mtu alikuwa amevimba kwa hasira.
Kumbe adella alimwamrisha aje kunisulubu.
Fisi akafanya kweli, safari hii haikuwa kama mwanzo, sikuona jiwe wala fimbo ya kumchapia.
Fisi akanirukia na kupitisha meno yake kwenye paja langu… maumivu makali yakanipitia.
Nilipagawa sana………
Akanifuata tena na kuniangusha chini kisha akanibamiza na kichwa chake katika mbavu zangu.
Nikashindwa kupumua vizuri.
Yule fisi akarudi nyuma tena kisha akanifuata kwa nguvu sana, nikajua kuwa kwqa namna yoyote ile alikuwa anakuja kunimalizia…
Nikafumba macho huku nikiuma meno kwa nguvu..
NIKIWA nimetulia pale nikikisubiri kifo changu mara nilisikia kilio kikali sana cha mwanaume ambaye alikuwa katika maumivu makali sana. Nikajikuta nikifumbua jicho langu kutazama. Nilimuona yule fisi mtu akigalagala chini huku akijitupa huku na kule.
Na baada ya hapo akatulia tuli huku akianza kuvimba kwa kasi kubwa na kelele kubwa zikiendelea kupigwa na yule fisi mtu.
Uvimbe ule ukaanza kuisababisha ngozi yake ianze kutatuka kana kwamba hapo awali ilikuwa imeshonwa na uzi wa kawaida.
Ilitatuka na baadaye kikasikika kishindo kikubwa sana wakati fisi yule akipasuka na kusambaratika vibaya mno.
Matone mazito ya damu ya moto kabisa yalinirukia, na hapo nikasikia tena mluzi mkali sana ukipigwa.
Ghalfa zikasikika shwangwe na hapo ukawa uwanja wa kugombania vilivyogombaniwa, misukule wale wachafu kabisa wakaingia katika ukumbi wa kuwania mabaki ya kupasuka fisi yule.
Walifika kwanza kwangu na kunigombania huku wakinilamba zile damu kwa matamanio, kucha zao zilikuwa zinaniumiza lakini nilitulia tuli kwa sababu sikujua naweza vipi kujiokoa kutoka katika hali ile.
Niliwaona misukule wengine wakigombania utumbo, wengine waligawana ngozi. Na baadaye msukule mmoja ukapita na kichwa cha yule fisi, kichwa ambacho kilikuwa na sura ya mtu kabisa.
Nikiwa nimeganda pale kama barafu mara alifika mbele yangu yule mama mweusi ambaye alikuwa akiitwa kwa cheo cha malikia.
‘’hicho kisichana chako kinachojifanya kukupenda kilitaka ufe leo nimekuokoa naomba utambue hilo….’’ Alizungumza vile kisha akatoweka.
Dakika mbili mbele ADELLA akasimama mbele yangu akitokea anapojua yeye mwenyewe.
‘’Martin nina ujauzito wako….’’ Alinieleza. Nikatumbua macho na kujiuliza ni lini mimi nilishiriki zinaa na binti yule. Lakini hakuonekana kutania kabisa alikaa akisubiri nijibu alipoona kimya akaendelea.
‘’Tambua kuwa mimi ni mzazi mwenzako…na utaniona Martin utake usitake…’’ alimaliza kusema hayo akaondoka zake. Akarejea alipotambua yeye mwenyewe.
Nilibaki kustaajabu ni kitu gani kile, huyu mama anadai kuwa ameniokoa yeye Adella alitaka nife sasa anakuja Adella anasema ana ujauzito wangu na anaenda mbali zaidi na kusema iwe isiwe lazima tutaoana. Niliduwaa sana.
Baada ya hali ya hewa kutulia, aliagizwa mtu kuja kunipa majukumu na hili jukumu la sasa nilitakiwa kwenda nikiwa mwenyewe bila kuambatana na Adella.
Niliagizwa kwenda kumpa motisha yule msanii wa mziki ili aweze kuhudhuria tamasha katika siku ile maalumu ambayo ilitajwa bila mimi kuitambua.
Alikuwa yule msanii ambaye Adella alianza kumwandaa tayari.
Nilijiuliza nitaanzia wapi bila adella lakini ilikuwa na sikutegemea nikapewa masharti yote ya kufuata. Niliona kuwa ni masharti magumu. Lakini nilipopigwa kibao na kujikuta natokea nyumbani kwa yule msanii ndipo niligundua kuwa mwanadamu ni kiumbe hatari sana, ishi na Mungu kila wakati ili kupambana na mambo haya, lakini bila nguvu zake jamani huko majumbani kwetu kuna mengi sana yanatokea.
Nilifika nyumbani kwa yule msanii, sijui nilikuwa naendeshwa na akili ya nani jamani. Haikuwa akili yangu kabisa, nilikuwa ninalo dumu lililokuwa na maji yale yanayofanania na damu. Nilifika kama nilivyoagizwa nikaliendea jokofu na kulifungua kisha nikaweka lile dumu ndani yake.
Nilikuwa nahofia sana yule mwandishi akisimama itakuwaje. Nilidhani ataniona lakini nilihakikishia kuwa hataamka mpaka nitakapoamua….
Baada ya kuweka maji yale kwenye jokofu nikawasha jani fulani hivi likafuka moshio kidogo kisha nikalizima.
Hivi umewahi kupatwa na kiu kikali sana usiku, ukakurupuka na kwenda kunywa maji.
Binafsi sijui kama ni kila tukio la aina hii linakuwa na maana mbaya ama la lakini naelezea ambacho nilishuhudia tu.
Baada ya moshi ule yule msanii alianza kuhangaika, wakati huo nimesimama nyuma ya mlango ambapo mimi namuona na yeye hanioni. Alisimama na kwenda katika jokofu, akachagua lile dumu langu.
Akafungua na kuweka katika glasi na kugida kwa fujo maji yale yafananayo na damu. Aligida kwa wingi mno, kisha akarejea kulala. Nikaliendea jokofu na kuchukua dumu lile likiwa limesalia na damu ile kiasi.
Kisha nikatoka nje nikapokelewa na fisi mtu mwingine, safari hii sikuuliza nikapanda mgongoni nikamshika masikio tukaondoka kwa kasi hadi kambini.
Na huko nikakuta nimeandaliwa sherehe fupi kwa kufanikiwa zoezi lile.
Nilipokuwa na adella nilikuwa nakula ugali na mboga za majani lakini siku hii nilikaribishwa chakula ambacho kwao wanakiita chakula bora sana.
Zilikuwa nyama nisizozielewa kabisa, na pia palikuwa na maji yafananayo na damu.
Nilikaribishwa kwa shangwe lakini sikuweza kula. Zile sura zilikuwa ngeni kabisa machoni pangu sikuwa na yeyote niliyekuwa namfahamu.
Mara bila mimi kusema neno lolote walianza kucheka kwa sauti ya juu na kisha mmoja wao akawanyamazisha wenzake na kuanza kuzungumza na mimi.
‘’NDUGU mwandishi, yaani ukakosa vitu vyote vya kuandika katika ulimwengu wenu mchafu huo ukaona uanze kutupekua na sisi ili utuandike…. Unajiamini kitu gani wewe kijana….’’ Alinipiga piga begani. Na hapo akaendelea.
‘’ukaona kutuandika haitoshi umekuja huku hata mwezi mmoja bado umempachika mimba binti yetu mchapakazi, hizo gharama za kule mtoto utaziweza mwandishi… ama una uwezo wa kumlipia mahari……’’ alinisanifu na wala hakuwa ameniuliza, akaendelea kunitazama machoni huku akichukua pande la nyama, ni hapo nikaliona lilikuwa limeambatana na sikio la mwanadamu, akarusha lote mdomoni huku akijilamba mikono yake akatafuna na kumeza kisha akatabasamu na kuendelea.
‘’unaotuona hapa sisi ni wazee wa huu ufalme na tumezipata taarifa kuwa umemjaza mimba malikia mtarajiwa wa ufalme huu…. Kwa hiyo wewe umetoka zako huko duniani na ghafla unataka uwe mfalme huku usipopajua.. una jeuri gani wewe……’’ akacheka kidogo na kuendelea, ‘’tumeipanga zawadi yako kwa hiki ulichoamua kufuata huku, tunataka tukupe zawadi ya mengi ya kushuhudia ili ukirejea huko ulimwengu dhaifu uwaandikie na wao wayasome na kutambua kuwa hawawezi kukabiliana na sisi ikiwa wataendelea na huo udhaifu…… kazi uliyoianza ni nzuri sana lakini kuna ugumu fulani, yule msanii amegoma kuja kwenye tamasha letu. Tunahitaji umlete kinguvu sasa maana tumejaribu kistaarabu imeshindikana…… tunahitaji umtumie mama yake mzazi…… na shughuli hiyo ifanyike ndani ya siku nne utuletee majibu, tunakurudisha duniani kwa siku hizo nne kwa ajili ya kuifanya hiyo kazi.. usijidanganye kuwa utatutoroka kwa sababu ulimwengu wenu dhaifu upo katika mikono yetu, ni wapi utakimbilia. Pia tutakuwa nawe kwa ajili ya kukupa maelekezo, sherehe yetu haitanoga bila kuwa na msanii. Ukimaliza hili tutafikiria namna ya kukupunguzia adhabu kwa sababu tangu uje huku haujaadhibiwa ujue… hebu’’ akasita na kisha akazungumza kabila nisilolijua. Na hapo akaletwa bwana mmoja asiyekuwa na mikono na mguu mmoja. Nilikuwa namfahamu kabisa sura yake haikuwa ngeni, aliwahi kuwa mwanasiasa maarufu.
‘’huyu hapa tumekula mguu na mkono na tutamla hadi amalizike kwa sababu alijifanya mbishi na mjanja mjanja’’ alinieleza. Halafu akaletwa mwanamke.
‘’unamuona huyu na mimba yake, hii mimba ina miezi thelathini hadi sasa, hatutamuachia kirahisi azae anajua alichotufanyia, ataumwa uchungu lakini hatajifungua…..’’ alinieleza na kisha akarejea tena katika mazungumzo.
‘’tunakuagiza kuifanya kazi, kaifanye kazi na hautakuwa na ugomvi na sisi lakini ukileta kujua sana hakika utateseka sana na huo si mkwara tupo makini na tunachokifanya.. tunakurudisha duniani uende kwa mama mzazi wa huyo msanii, ni kipi utamfanya ama kipi utatakiwa kufanya ukifika duniani tutakutumia majibu…. Simama ‘’ aliniamrisha nikasimama………
Kama nilidhani mambo magumu yalikuwa kumuona mwanadamu akimla mwanadamu mwenzake, nilikuwa najiongopea kuna mengine magumu zaidi yaliyokuwa yakinisubiri.
Kuna jambo moja tu msomaji nilikuwa nalisahau kila siku, nilikuwa namsahau ama sikuwahi kumtegemea Mungu. Ni vile sikukuzwa katia misingi hi indo maana niliteseka sana, na huenda haya yalinitokea ili nije kukuandikia wewe usome kisha ujifunze……
Katika kipengele kimojawapo katika masimulizi haya nilisema kuwa wabaya watu jama wanyama kama paka na fisi hawa wanatumwa tu hawana ubaya wowote.
Na hawa watu wabaya hawazaliwi na roho mbaya bali mazingira na matukio yanayowatokea maishani husababisha wawe na roho mbaya.
Mimi nilishiriki kutimiza matakwa ya watu hawa wenye roho mbaya.
Nilifungwa akili jamani, hadi sasa hivi sijui ilikuwaje hadi nikashindwa kabisa kutoroka. Acha niamini kuwa nilifungwa akili katika kiwango cha juu sana…
Nilitupwa duniani, nikajikuta nipo katika chumba kimoja kilichokuwa na meza na viti viwili huku pia pakiwa na kitanda na godoro.
Kwa kifupi kilikuwa ni chumba ambacho angeweza kuishi kijana ambaye bado hajaoa. Sikuwa nafanya kazi yoyote, lakini kila siku nilikuwa nakuta chakula pale ndani, kilikuwa chakula kizuri sana kwa kutazama, wakati mwingine kuku, pilau, nyama ya mbuzi na kadhalika.
Ilikuwa baadaye sana nilipoambiwa kuwa zile hazikuwa nyama za kuku wala mbuzi bali nilikuwa nalishwa mizoga ya fisi na wakati mwingine nyama za watu ili niwe na roho mbaya.
Naam, ile roho ikajipandikiza na nikajikuta nayazoea maisha yale kwa juma moja tu.
Na hapo nikaingia kazini.
Mama wa yule msanii alikuwa ni mjamzito, ujauzito ule ulikuwa una miezi ipatayo nane na nusu. Muda wowote ule alitakiwa kujifungua.
Ni hapo ndipo nilipofanya nilichoagizwa, nilimfuatilia yule mama alipokuwa akifanya maozezi ya kutembea, nikapishana naye na kisha nikachota mchanga katika hatua alizoacha barabarani. Nikaenda na ule mchanga ndani kwangu, usiku wakaja wazee kuuchukua huku wakiniambia kuwa nimefanya kazi nzuri.
Ni hapo yalifuata mateso makali kwa yule mama, wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi, sasa jiulize ule uchungu unakuja lakini mtoto hatoki.
Walimwengu wana mapana jama.
Niliagizwa niende kumshaurti yule msanii ambaye alikuwa ni mtoto mkubwa wa mama yule. Niliamriwa nimshawishi aende kwa waganga kwa sababu hospitali pekee haitoshi.
Kweli nikaenda kumsalimia yule mama pale hospitali nikijifanya mimi ni jirani mwema, baadaye nikamvuta yule bwana na kisha nikamuelezea kuwa hata mimi mama yangu aliwahi kupatwa na tatizo kama lile, nikamsihi sana kuwa lile si tatizo la kawaida na asipokuwa makini basi mama yake ataaga duniani.
Nani kama mama……. Kusikia kuwa mama atapotea akanishika mkono na kuniuliza ni kipi anatakiwa kufanya.
Kitendo cha kunishika mkono likawa ni kosa kubwa sana kwake.
Akajikuta akinisikiliza kila nilichokuwa nasema.
Hatimaye baada ya siku mbili nikamfikisha kwa mganga ambaye alikuwa mwenzetu pia.
Akamchanganyia madawa, akampa na maelekezo.
Ile tunarudi hospitali mama alikuwa amejifungua tayari mtoto wa kike.
Yule msanii akanishukuru sana lakini nikamwambia kuwa aende kumshukuru yule mganga.
Kweli akaenda na huo ukawa mwisho wake kuishi duniani.
Niliumia sana mpenzi msomaji, kwani nilikuwa duniani wakati wakitangaza kuwa msanii yule amekutwa akiwa amekufa kitandani kwake bila kuwa na kovu hata moja.