Kama mtavyoona kwenye article hii. Siri kali yetu kila kitu ni siri. Mikataba ta madini ni siri hata wabunge hawaruhusiwi kuiona na kuijadili. Wabunge bungeni wafunge midomo yao. Wale wataojifanya wajuaji watapewa onyo kali kama hawatasikia basi WATAWAKOLIMBA kama walivyomkolimba Amina, Sokoine na Kolimba. Kashfa ya Richmond ambayo inamhusu kingunge wa juu kabisa, aliwaomba wabunge wasiijadili. Nchi yetu inakwenda wapi!!!?
~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+~+
TAARIFA kuwa serikali imewaonya wabunge wa CCM kuwa makini wakati wakichangia hoja bungeni, zimetushangaza.
Zimekuwa ni habari za kushangaza kwetu, kwa sababu uamuzi wa kuwaonya ulifikiwa wakati wabunge hao walipokutana kama kamati ya chama kufanya tathimini ya namna walivyoshiriki katika kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti na ile ya mwelekeo wa uchumi wa taifa.
Moja ya michango iliyotolewa na wabunge wa CCM ni dhahiri kwamba, ilikuwa ikiiweka katika wakati mgumu serikali, kwa kuzingatia kwamba, iliyowaahidi wananchi imeshindwa kuyatekeleza, na hicho ndio chanzo cha kelele za wabunge.
Mmoja wa wabunge waliokuwa mbogo kwa serikali ni Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM) aliyetishia kukwamisha bajeti za wizara tatu, ikiwamo ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa muda mrefu.
Tunapenda kuikumbusha serikali kwamba, wabunge ni wawakilishi wa wananchi, na wameingia bungeni kwa kupigiwa kura na wananchi, hivyo kitendo cha kuwaita kwenye kikao cha faragha na kuwakaripia kinakiuka misingi ya utawala bora.
Tumefikia uamuzi huu wa kuikumbusha serikali jambo hili kwa sababu si mara ya kwanza kwa serikali kuwatisha wabunge wa chama tawala, ambao wamekuwa wakitofautiana na baadhi ya maamuzi yake, hasa yale yenye athari mbaya kwa wananchi.
Jambo kubwa tunalojiuliza kila serikali inapowaita wabunge wa CCM na kuwaonya ni kwamba, iko madarakani kwa maslahi ya nani kama haitaki kushauriwa na wawakilishi wa watu inaowatawala?
Hatutaki kueleweka vibaya, kwa kueleza msimamo wetu kuhusu jambo hili, kwamba tumelazimika kulisema hili kwa sababu tunadhani wakati wa kuwa na wabunge ambao akili na mawazo yao yameshikiliwa na serikali sasa umepitwa na wakati.
Watanzania wanataka maendeleo, yanayopatikana kwa kila mwananchi kutimiza wajibu wake inavyostahili, hivyo anapotokea mtu au chombo chochote kukwamisha jitihada hizo, ni lazima mtu au chombo hicho kikemewe mapema.
Kusema hivi hatuna maana kwamba tunakusudia kuikemea serikali, bali tunaishauri iepuke tabia ya kuziba mdomo wawakilishi wa wananchi wanapokuwa wakitetea maslahi ya hao waliwaochagua kuwatetea.
Na kwa viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwashambulia wabunge wanaoikosoa serikali katika baadhi ya mambo inayoonekana kufanya kwa makosa, tunapenda kuwakumbusha kwamba, wanachokifanya ni usaliti kwa Watanzania.
Watambue kuwa wabunge, sehemu yao ya kuzungumza ukweli ni bungeni, hivyo kuwanyima uhuru huo ni kuwabana na kuwafanya wasitekeleze majukumu yao kama inavyotakiwa.
Tuwakumbushe viongozi wa aina hii kwamba wakati wa Watanzania kuendelea kuburuzwa unazidi kupungua. Hivyo kitendo chochote chenye mwelekeo wa kuziba sauti za wawakilishi wa wananchi, ni chenye nia ya kutaka kuwaburuza wananchi kwa sababu sauti inakuwa haisikiki katika chombo muhimu kabisa kinachohusika na kutunga sheria za taifa letu.