Habari zenu Ndugu WanaJamboForum,
Kwanza nianze kwa kusema
Mungu ailaze roho ya Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia Mahala Pema Peponi Amen!
Amina tutakukumbuka kama kijana mtanashati, jasiri, mwerevu, mchangamfu na mjenga hoja! CCM umetuachia pengo kubwa sana katika vijana wetu shupavu kama wewe, lakini kama isemavyo, 'Akitakacho Mungu hashindwi, kwani Dunia ni yake". Rest in Peace!
Okey! On the other side:-
Kwanza nauliza kwanini Serikali haikumpa ulinzi wakati Amina Chifupa alivyosema kwamba atafichua majina ya watu wenye kudeal na madawa ya kulevya na vinginevyo, wakamwacha aende bila ulinzi, na najua Serikali walijua kwamba anajua hao watu, wakamwacha aende hivi hivi bila ulinzi, na wanajua kitu chochote kinaweza kufanyika wakati huo?
Pili kama walijua ugonjwa wa marehemu, kwanini wasingempeleka kuu ya Taifa ya Muhimbili, wakaenda kumweka kwenye hospitali ya Jeshi, Jamani!!
Hospitali ya Jeshi?????????!!!!????.. Na wanakuja na excuse ya Kisukari.... ivi kuna mtu anaweza kufa na kisukari.. embu nielimisheni kama nimekosea, lakini kuna watu wengi wanavisukari lakini hawawafi kwa kuoza mwili na mwili kuwa ganzi, kama sukari imepanda mpaka juu unapewa dawa, na ikiwa chini kuna description unapewa ili iwe wastani.. na ikipita viwango unakufa..
Hii ni sumu kabisa inaonekana... Mimi binafsi na wenzangu tunajaribu kufanya '
invetigation' katika hili swala, na kwa wengine wanaofanya investigation msisite kutueleza hapa kwenye forum and likewise!!
Kitu kinachonisononesha ni Mtoto wake Amina, anakua bila mama! Duh... Mungu awape nguvu famlia na Amina waweze kupita majonzi na uchungu wakati mgumu kama huu..
Pia naona wapinzani, viongozi , wasanii, na watu mbalimbali waliyokuja hapo kwenye nyumba ya marehemu kutoa salamu zao za pole kwa familia ya Chifupa.
Kuna habari hii nimesoma kutoka gazeti la 'Wapinzani wetu' kuhusu kifo cha Amina, Soma Chini Kwa Habari Zaidi!!
Simanzi: Kifo cha Amina Chifupa
Na Happiness Katabazi
KIFO cha Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Chifupa, kilichotokea juzi katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, jijini Dar es Salaam kimelitikisa taifa.
Habari ambazo gazeti hili limezikusanya kutoka sehemu mbalimbali nchini zinaonyesha kwamba msiba wa mwanasiasa huyo kijana umebadili kabisa mwenendo wa mambo kitaifa.
Uamuzi wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kutangaza kuahirishwa kwa Kikao cha Bunge la Bajeti kwa siku nzima jana kwa ajili ya kutoa fursa kwa wabunge kushiriki kumuomboleza mwanasiasa huyo, unatokana na namna tukio hilo lilivyogusa hisia za watu wengi.
Viongozi takriban wote wakuu kitaifa, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Edward Lowassa, viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa, wanasiasa wa vyama mbalimbali vya siasa, wafanyabiashara na wananchi wengine kwa ujumla, kila mmoja kwa wakati wake alionekana akiwa ameguswa na tukio hili kubwa la kwanza la aina yake.
Jijini Dar es Salaam jana, hali ilikuwa ni ya majonzi makubwa na katika maeneo mbalimbali habari kuu iliyokuwa ikizungumzwa ilikuwa ni hiyo ya kifo cha mwanasiasa huyo ambaye tangu alipoingia bungeni Desemba mwaka juzi, alitokea kuwa mjengaji makini wa hoja.
Kikubwa kinachoonekana kuwaumiza vichwa watu wengi ni mazingira ya kifo chake, kila mmoja akiwa hataki kuamini iwapo kweli mwanasiasa huyo alikuwa amekumbwa na maradhi makubwa ambayo hatimaye yamechukua maisha yake.
Nini hasa kimemuua Amina jamani, ni kisukari kweli? Ni kitu gani hasa? ndilo swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Nyumbani kwa baba yake mzazi, Hamisi Gabriel Chifupa, hali ilikuwa ni tete kuanzia usiku ya kuamkia jana na kwa jana nzima maelfu ya watu waliokuwa katika hali ya simanzi na kwikwi za kuomboleza walifika katika eneo hilo kufarijiana.
Vilio vya hapa na pale, huzuni na mshtuko wa kutoamini kilichotokea uliendelea kutawala eneo hilo na hata maneno yaliyozungumzwa na baba mzazi wa Amina na aliyekuwa mumewe, Mohammed Mpakanjia, kwa nyakati tofauti jana, yalikuwa yakionyesha dhahiri hali ya kutoamini au kuelewa vyema ni kitu gani hasa kilikuwa kimemtokea.
Amefariki
alianza kuugua tangu Mei 8, alikuwa na homa kali na baadaye ikajulikana alikuwa na kisukari ambacho sijui kilitokea wapi kwa kuwa sisi tulikuwa hatujui. Wataalamu wamejaribu sana kuokoa maisha yake lakini imeshindikana, alisema mzee Chifupa.
Kwa upande wake, Mpakanjia jana alasiri akizungumza huku akibubujikwa machozi alikaririwa akisema; alikutwa akiwa na kisukari ambacho jitihada za madaktari kujaribu kushusha kiwango cha sukari yake waliyokuwa wakiielezea kuwa haikuwa ya kawaida kwa mtu aliye hai zilishindikana.
Vilio na simanzi viliongezeka majira ya saa 7:57 mchana wakati mwili wa Amina ulipowasili nyumbani kwa wazazi wake, Mikocheni.
Ni hakika watu wengi walikuwa hawaamini kifo cha Amina lakini baada ya kuwasili kwa jeneza hilo baadhi ya wananchi walisikika wakisema wameamini kufariki kwa Amina baada ya kuona jeneza hilo.
Jeneza hilo baada ya kuingizwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo, ulisomewa dua iliyoongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaban bin Simba kwa muda wa dakika tano, kisha likaingizwa sebuleni ambapo mwili huo unalala hapo hadi leo asubuhi kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Lupembe-Ihenjo, wilayani Njombe kwa mazishi.
Baba wa marehemu alisema uamuzi wa kumzika huko unatokana na uamuzi wa Amina mwenyewe ambaye alipata kueleza miaka mingi nyuma kwamba alitaka atakapokufa azikwe huko.
Mama yake Amina alisikika akilia huku akisema: Alipata ujauzito nikampeleka Hospitali ya Mwananyamala akajifungua salama, hivi karibuni ameugua tukampeleka Hospitali ya Lugalo kumbe mwanangu ndiyo anakufa.
Binafsi yangu yanasema kifo cha Mbunge Chifupa, nakihusisha na masuala ya kishirikina kabisa na kama nitakuwa natenda dhambi Mungu anisamehe, alisema muombolezaji mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, baba wa marehemu alisema hausishi kifo cha mwanae na imani za kishirikina wala mapambano yake dhidi ya dawa za kulevya, bali anaamini ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kuwataka vijana waendelee alipoishia.
Kwa upande wake, Mpakanjia alisema haamini kilichotokea, ila kikubwa kinachomsikitisha ni mwanawe ambaye bado anahitaji mapenzi ya mama yake na kuongeza kwamba amemwacha katika wakati mgumu.
Ilipotimia saa 10:34 jioni, ujumbe wa wabunge 32 waliomwakilisha Waziri Mkuu na wabunge wengine uliwasili nyumbani kwa mzee Chifupa ukiongozwa na Spika, Samuel Sitta.
Sitta, alisema Bunge lililazimika kuahirisha kikao chake kwa ajili ya kuomboleza kifo hicho.
Alisema ujumbe huo umekuja na ujumbe wa simanzi kutoka kwa wabunge wote na Waziri Mkuu na kusema kwamba, hakika Bunge limepata pigo kubwa kwa kumpoteza mbunge huyo.
Aidha, alisema Mbunge wa Singida Kusini, Mohamed Misanga, ndiye atakayeongoza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo kwenye msafara wa mazishi kijijini Lupembe.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya serikali, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, alisema serikali imepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo cha mbunge huyo aliyekuwa mstari wa mbele kupambana na mambo mbalimbali hususan yaliyowahusu vijana.
Njia pekee ya kumuenzi marehemu ni kutekeleza kwa vitendo yale yote aliyoyapigania..tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi, alisema Mwapachu ambaye alitoa ubani wa sh milioni moja kwa niaba ya serikali.
Aidha, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kwa niaba ya Baraza Kuu la umoja huo amesikitishwa na msiba huo na kumtaka Mpakanjia na mzee Chifupa, kukubali kwamba ni kazi ya Mungu ambayo haina makosa, hivyo wakubaliane na hali halisi.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed, alisema kambi yake ilipata faraja kuona mbunge wa
CCM kijana shujaa akiingia bungeni na kuiomba familia iwe na moyo wa uvumilivu.
Kila kifo kina upya wake na uchungu wake. Nasema kifo hiki ni kipya kwa sisi wahusika wa taifa hili, kilichobaki sote pamoja tuige na kuendeleza yale yote mazuri aliyoyaacha, alisema Hamad Rashid.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria msiba huo ni Waziri Mkuu mstaafu, Rashid Kawawa, Dk. Salim Ahmed Salim, John Cheyo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mama Maria Nyerere na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali (Taarifa zaidi zimo ndani).