Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
BURIANI RAFIKI NA NDUGU YANGU SALUM ''SLIM'' SHAMTE 1951 - 2020
Nimeingia maktaba yangu ya picha ndani ya photo album natafuta picha moja ya Slim niliyompiga kiasi cha miaka 20 iliyopita mwezi mtukufu wa Ramadhani kwenye futari ambayo kila mwaka alikuwa akitualika nyumbani kwake Bombo.
Kwa kipindi chote nilichoishi Tanga kila Ramadhani kulikuwa na siku Shamte anatualike tunajumuika nyumbani kwake kufuturu pamoja.
Tunaanza kwa kufungua muazini kwa maji, juisi na tende kisha tunasali kwenye bustani yake na baada ya hapo tunafuturu tukimaliza tunaomba dua na kutawanyika.
Futari ya Slim Shamte nyumbani kwake Bombo, Tanga nzima tukiipenda si kwa ajili ya mapochopocho bali futari hii ilikuwa inaukusanya mji mzima wa Tanga nyumbani kwa Shamte.
Slim alikuwa akiwaalika wengi katika jamii ya Tanga
Mamudir yaani wakuu wa vyuo vyote vya Tanga na masheikh wa mji walikuwa wanahudhuria futari hii na utawaona wamekaa pamoja bega kwa bega na raha inakuja pale panapokimiwa ili tusali.
Hapo katika hadhira ile wapo wanazuoni wa juu kabisa katika Afrika ya Mashariki lakini kila mmoja inapokuja kuongoza sala ile ya Maghrib atajirudisha nyuma kutaka mwenzake atangulie.
Tanga ni kati ya miji michache sana katika Afrika ya Mashariki ambayo hawezi mtu kutoka nje akaenda pale kwa nia ya kusomesha.
Allah ameijalia Tanga kuwa mji ambao unajitosheleza kwa elimu ya dini kiasi wanafunzi wanatoka nje ya Tanga kuja pale kusoma iwe TAMTA, Zaharua, Maawa au Shamsi Maarif.
Pale tuliposimama kusubiri ikama ili tuswali Maghrib katika safa hii ya wasomi wapo vijana na wapo wazee na hawa wazee wengine ni walimu waliowasomesha hawa wanazuoni vijana.
Hapa wanazuoni vijana wanajua wazi kuwa kusalisha sala ile basi aula zaidi ni mwalimu wao, kwanza kwa ule ualimu wa kuwasomesha wao anastahili yeye kuwasalisha na pili haiyumkini kuwa mwalimu aongozwe na wamanafunzi wake.
Basi utasikia sheikh anasema, ''Nyote mwakimbia kusalisha hoja yenu ati atangulie mzee sasa mtafanza haya hadi lini? Sasa mswalishe nasi tu hai tukuoneni kama kweli mwapatia.''
Watu wa Tanga ni watu fasaha sana wanapozungumza utapenda kusikiliza.
Sheikh atasema haya maneno kwa maskhara kwa ile lafidh ya Kitanga lakini hatatangulia atamwita mmoja wa vijana wanazuoni kuja kusalisha.
Hapa inakuwa ile itifaki na adabu ya elimu imezingatiwa.
Hii ishakuwa amri na kijana atasogea mbele na kusalisha.
Kuanzia hapa sasa tunapata raha nyingine kwa kusikiliza kile kiraa, yaani usomaji wa Qur'an kwa mazingatio ya hukumu zake zote.
Naam na imam sharti asome vizuri eti kwani nyuma yake anasalisha pamoja na sisi maamuma wenzangu mie, wanazuoni wakubwa.
Siku zote kila mwaka ilikuwa inapofika kipande hiki cha umma kusali pamoja pale nyumbani kwa Shamte kwenye bustani yake yenye maua mazuri nafsi yangu ilikuwa inaburudika sana.
Nitapenda kueleza jambo hapa.
Pamoja na maua mazuri haya na majani, Slim nyumbani kwake kapanda mkonge kuzunguka wigo mzima bila shaka kuufahamisha ulimwengu kuwa yeye ni mtu wa mkonge.
Nimesema kuwa nilikuwa natafuta picha moja ya Slim niliyompiga zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Bahati mbaya sana kwangu picha hii sikuipata.
Nitaeleza kwa nini picha hii mimi nilitaka niiweke hapa muione.
Abdallah Mgambo amemtangulia Salum Shamte kwa siku moja kufariki.
Picha hii yupo Abdallah Mgambo na Slim nimewapiga mwezi wa Ramadhani Mkonge Hotel kwenye futari ya Shamte.
Iweje kiwanja tumebadili hatufuturu nyumbani tumehamia Mkonge Hotel, moja ya hotel za kupendeza mjini Tanga?
Siku ile mvua kubwa ilinyesha kuanzia asubuhi.
Mimi nikiishi si mbali na nyumbani kwake Shamte na mkewe Bi. Mariam.
Nikampigia simu Slim kumuuliza itakuwaje futari na mvua ile nikitambua fika kuwa ndani ya nyumba yake tusingeweza kuenea hata kidogo lau kama nyumba yake haikuwa kibanda.
Slim akanijibu kwa namna yake ambayo marafiki zake tukijua, anazungumza huku anacheka, ''Sidney tutafuturu In Shaa Allah.''
Sikupata kumuona Slim kaweka uso wa jiwe hata siku moja yeye saa zote ni mtu wa tabasamu.
Futari ya mwaka ule tulifuturu Mkonge Hotel na kwa hakika mwaka ule Shamte alitustarehesha juu ya kuwa baadhi yetu tulilowa.
Hapa Mkonge Hotel siku ile nilipiga picha nyingi katika hali ya mvua ile na wingu lile.
Abdallah Mgambo ambae kama nilivyoelza awali kuwa alimtangulia Shamte kufariki kwa siku moja alikuwa amenitembelea nikamwambia kuwa kaja na mguu mzuri kwani siku ile tutafuturu kwa Shamte.
Abdallah Mgambo na Shamte wote niliwanasa katika camera yangu.
Nimesikitika sana kutoiona picha hii kwani kwangu ni kumbukumbu nzuri sana.
Shamte alikuwa akikualikeni futari yeye hali kwa utulivu muda wote anatoa maelekezo au kachukua hiki mwenyewe kampelekea yule mara wameingia wageni wamechelewa ataelekeza wawekwe wapi kukaa na nani akae na nani nk. nk.
Chakula kinashuka vizuri ikiwa unakula pamoja na marafiki zako.
Shamte alikuwa na rafiki yake kipenzi Sheikh Balhassan.
Sheikh Balhassan alikuwa miongoni mwa masheikh wanaoheshimika sana pale mjini.
Kila mwaka baada ya kufuturu Shamte atamuomba Sheikh Balhassan aombe dua.
Sayyid Muhammad Hashim kutoka Tanga kabla ya maziko aliposimama kutoa rambirambi alisema kuwa watu wa Tanga wamejiinamia kwa majonzi kama tulivyoijiinamia sisi watu Dar es Salaam pale nyumbani kwa Shamte, Mbweni.
Hakuna madrasa Tanga ambayo Shamte hakupata kuinyooshea mkono.
Hujapata wewe kumuona mtu karim kama Shamte.
Slim alikuwa mtu karim mlango wa nyumba yake ulikuwa wazi kwa kila muhitaji na hakujua kumnyanyapaa mtu.
Hakuna ambae mbae alikuwa hamjui Shamte Tanga kuanzia mjini hadi vijijini achilia vile vijiji ambavyo kuna mashamba ya mkonge.
Nimepata kuwa na ''great moments,'' na Shamte nyingi tu baadhi za kuchekesha na nyingine za kuogofya na kusikitisha.
Huenda wengine wasifahamu yale ya ndani ambayo Shamte alipata kukutananayo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Katani Limited.
Mti wenye matunda ndiyo unaopopolewa.
Kuna walioona katika viongozi kuwa wana haki zaidi ya Shamte ya kutia vidole vyao katika yale aliyokuwanayo Slim na wanaona hiyo ni haki yao kwa sababu ya nafasi zao.
Zaidi ya miaka 20 iliyopita katika mazungumzo alipata kunihadithia dhiki alizokuwa anapata kutoka kwa kiongozi mmoja aliyedhani kuwa yeye yuko juu ya kila mtu katika mkoa ule.
Shamte alikuwa akimstahamilia na kufanya staha kwa kuheshimu ule umri wa huyu bwana.
Slim alishukuru bwana yule alipoondoka Tanga.
Naamini pale nyumbani kwake Mbweni kabla ya maziko ulipokuwa unasomwa wasifu wake wengi walistaajabishwa na yale ambayo Shamte aliyafanya katika umri wake katika biashara na ujasiriamali.
Neno hili, ''ujasiriamali,'' mimi kwa mara ya kwanza nililisikia kutoka kwa Shamte.
Nimebahatika pia kuwepo kwenye shughuli zake nyingi kuanzia mkutano ya kimataifa kuhusu mkonge uliofanyika Tanga, uzinduzi wa bidhaa mpya aliofanya Golden Tulip, Dar es Salaam kwa kutaja machache.
Lakini katika miradi hii yote hakuna mradi ulionivutia kama mradi wa Hale wa kufua umeme kutoka kwenye gesi.
Kila siku akinisisitizia niende kuutazama.
Nilifika Hale na nilishangazwa kuona jinsi makapi ya mkonge yalivyokuwa yakitoa gesi iliyogeuzwa kuwa umeme na umeme ule ukawasha ukatumika kiwandani na katika nyumba za jirani.
Msomaji wa wasifu wa Shamte alisahau kitu kimoja kuwaeleza waombolezaji.
Salum Shamte alikuwa ''super intelligent.''
Mtihani wa Cambridge ''O'' Level alipata credit 9 ndani yake sijui ziko ''Distinction,'' ngapi.
Nini maana yake kupasi namna hii?
Maana yake Shamte angeliweza kusoma chochote na narudia chochote katika mgongo huu wa ardhi.
Pasi hizi ndizo zilizomuingiza Chuo Kikuu cha Nairobi.
Lakini kuna wengi sana ambao haya wala hawakuyajua walimtazama Shamte kama Mswahili mmoja,
Ramadhani Madabida alisimama kuzungumza kwa niaba ya familia ya Shamte.
Hakuweza kuzungumza aliishia kutoa salamu na kumswalia Mtume akaangua kilio cha kwiki na ilibidi aondolewe akakae chini apumzike.
Vipi Madabida ataweza kumzungumza mpenzi wake, rafiki yake ndugu yake, shemeji yake aliyemuoza dada yake Bi. Zarina bint Juma na kupata watoto wema mmoja wa kiume Abdulwahab Madabida yeye pale aliposimama kuzungumza anamuona Abdulwahab akipita akishughulika katika msiba wa mjomba wake?
Vipi utamtegemea Madabida aweze kueleza kote alimopita na Slim kuanzia Pugu Sekondari wakiwa vijana wadogo hadi alipomuoa dada ya rafiki yake kipenzi?
Madabida alitueleza yote ya hisani baina yao katika lile chozi lake.
Haya ni katika yale ambayo watengenezaji filamu kama David Lean hutengeneza senema zinazoitwa, ''Block Blaster.''
Sayyid Muhammad Hashim aliwaambia watu wa Dar es Salaam kuwa, ''Nyinyi mnamjua Shamte kwa mambo ya mkonge, sisi Tanga tunamjua Shamte kama kiongozi wa dini.''
Tunakuomba Mola wetu Wewe uliye Hakim Muadilifu muamulie ndugu yetu Shamte kwa haki katika yale yaliyomsibu katika siku zake za mwisho hapa duniani.
Amin
PICHA:
Slim wa kwanza kulia Mohamed Said, Mohamed Bhinda, Salum Matimbwa, Abdallah Tambaza na Abdallah Shamte mazikoni makaburi ya Msasani Februari 2020.
Sheikh Balhassan siku ya harusi ya mtoto wa Shamte, Juma ambaye ni huyo wa kwanza kulia.
Salum Shamte ni huyo wa tatu kushoto na wa kwanza ni Sayyid Muhammad Hashim hapo ni harusini Tanga miaka mingi iliyopita.