Allien
JF-Expert Member
- Jul 6, 2008
- 5,546
- 1,861
Haya . . . Kanyaga twende . . . .
Source: UPL-Homepage
Source: UPL-Homepage
Oscar Mukasa: Kijana anayedhamiria kutumia
NA EPSON LUHWAGO
KUNA msemo unenao kuwa mjenga nchi ni mwananchi. Msemo huo ambao umezoeleka miongoni mwa watu una busara ya namna ya kipekee na una maana kwamba aendeleo yatatokana na wananchi wenyewe katika jamii husika kwa kutumia nyenzo na rasilimali zilizopo wakiwemo watu. Ni msemo ambao umekuwa ukitoa changamoto ya aina yake kwa Watanzania kutaka kutumia juhudi, maarifa na uwezo wao katika kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.
Kutokana na ukweli huo, kuna Watanzania lukuki wanaosoma ndani na nje ya nchi ama kwa gharama zao au za serikali ili pindi wanapomaliza watumie elimu yao katika maendeleo ya taifa. Pamoja na ukweli huo, ni Watanzania wachache ambao wamekuwa na mtazamo chanya katika kushiriki kwao kutoa mchango wao kuendeleza jamii zao ili kuondokana na umasikini unaowakabili.
Oscar Mukasa, ameamua kuvunja ukimya na kuwa mfano kwa vijana wengine wasomi wa Tanzania katika kushiriki kwa vitendo kutumia elimu na maarifa yake kuisaidia jamii katika maendeleo. Akizungumza na mwandishi wa makala hii ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam, juzi, Mukasa alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na kuguswa na kuamini kuwa yeye ni sehemu ya jamii, hivyo anahusika moja kwa moja kuibadilisha na kuwa na maendeleo endelevu.
"Matatizo ya nyumba hayamalizwi bila juhudi binafsi za wenye nyumba. Kadhalika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, haziwezi kutoka kwenye kundi la dunia ya tatu wala kuondokana na umasikini, ujinga na maradhi, isipokuwa kwa juhudi za watanzania wenyewe, kwa nafasi zao, taaluma zao, na dhamira zao njema," alisema.
Mukasa, mwenye umri wa miaka 38 na mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano katika afya na utabibu, alisema hiyo ndiyo inayomgusa zaidi katika kujitoa kwake kushiriki katika mapambano dhidi ya matatizo yanayoikabili jamii.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa akiwaza nini hasa suluhisho la kupunguza matatizo yanayowakabili wananchi wengi hasa wa vijijini huku Watanzania wengi waliosoma wakiyapa kisogo matatizo hayo.
Mukasa, mwenye shahada ya uzamili katika teknolojia ya habari na mawasiliano, alitoa mfano wa sehemu anakotoka, wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kwamba wananchi wanaishi katika hali ngumu licha ya kuwa na rasilimali lukuki.
"Inaumiza kuona miaka nenda miaka rudi, jamii iliyotulea inagubikwa na matatizo mengi mno. Nadhani wakati umefika sasa wa kushiriki kuyatatua kwani ni sehemu ya jamii ile," alisema.
Mukasa, ambaye hivi karibuni anatarajia kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) nchini Uswisi, aliongeza: "Sisi kama vijana taaluma na nafasi zetu zitakuwa na maana zaidi kama zinatoa mchango moja kwa moja katika kutatua matatizo ya jamii tunazotoka."
Alisema wapo vijana wengi wasomi fani mbalimbali kama vile afya, elimu na uhandisi hivyo wanatakiwa kupata fursa kushiriki katika kuiletea jamii maisha bora, kwa kutumia taaluma zao.
Kwa mujibu wa Mukasa, matatizo ya maji, upungufu wa walimu katika shule za sekondari na msingi, na upungufu wa watumishi wa afya ni baadhi ya mambo yanayohitaji msukumo wa kutosha ili kuyapatia ufumbuzi.
"Panapokuwa na ubunifu ufumbuzi wa masuala haya unawezekana kwa kiasi kikubwa sana. Kinachohitajika ni kuhakikisha unakuwepo uwakilishi mzuri katika vyombo vya maamuzi," alisema.
Anaamini kwamba elimu, ambayo kwa dunia ya sasa ni silaha muhimu katika kuongoza mpambano dhidi ya umasikini, hivyo Watanzania wasomi hawana budi kuitumia ipasavyo katika kushughulikia matatizo hayo.
Kuhusu njia atakazotumia kutimiza malengo yake ya kupambana na umasikini kwa maeneo ya Tanzania yaliyonyuma, alisema jambo kubwa ni elimu yake na uzoefu alio nao.
"Nina uzoefu wa kuandika na kusimamia miradi ya maendeleo katika nyanja za afya. Ni suala la kutumia ujuzi na uzoefu huo kwa kupanua wigo wa fikra," alisisitiza.
Alisema hivi sasa anashirikiana na rafiki zake wa Italia, Canada na Singapore kuandika miradi maalumu katika nyanja tofauti, hivyo lengo lake kuelekeza nguvu hizo katika maeneo yanayohitaji miradi hiyo, Biharamulo ikiwemo.
"Tayari tumekuwa na mazungumzo na wafadhili mbalimbali ambao wameonesha nia ya dhati kufadhili miradi hii. Tutakapokuwa tayari hivi karibuni nitaiweka hadharani ili umma uelewe," aliongeza.
Katika kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa, mpango shirikishi baina yake na wananchi wa wilaya ya Biharamulo utakuwa dira kuu ya mafanikio.
Kwa mujibu wa Mukasa, wilaya hiyo ina vijana wengi waliosoma hivyo kinachohitajika ni kuwakusanya pamoja na kutumia elimu na taaluma zao katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi hao.
ALIKOTOKA
Mukasa aliyezaliwa Julai 1970, ni mtoto wa tano kati ya 10 katika familia ya Mzee William Mukasa na Mama Apolonia Mukasa. Alizaliwa katika kijiji cha Rukaragata kilichopo takriban kilometa tatu kutoka mji Biharamulo, barabara ya kwenda wilayani Ngara.
Baba yake ni mtumishi wa umma mstaafu ambaye amewahi kuwa Ofisa Afya wa wilaya ya Biharamulo kati ya mwaka 1977 na mwaka 1987 kabla ya kuwa Ofisa Afya wa mkoa wa Kagera kati ya mwaka 1987 na 1992 alipostaafu kwa mujibu wa sheria. Kabla ya hapo, aliwahi kuwa mtumishi wa umma sehemu mbalimbali nchini.
Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Biharamulo kuanzia mwaka 1978 mpaka 1984 na baada ya hapo alichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Nyakato iliyopo nje kidogo ya mji wa Bukoba.
Mwaka 1989 alichaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari ya Pugu, Dar es Salaam katika masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati.
Mwaka 1991/1992, alitumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria katika kambi za Ruvu mkoani Pwani na Maramba, Tanga.
Baada ya hapo, mwaka 1993 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya shahada ya kwanza ya sayansi katika hisabati na takwimu.
Hakuishia hapo kwani baada ya kufanya kazi kwa muda katika Kituo cha Utafiti na Maendeleo ya Afya cha Ifakara, alikwenda Uholanzi kwa masomo ya shahada ya uzamili ya sayansi katika Teknolojia ya Mawasiliano na Habari katika tiba (MSc in Medical Informatics) kwenye Taasisi ya Sayansi za Afya. Alihitimu shahada hiyo mwaka 2001.
Hivi sasa ni mwanafunzi wa masomo ya shahada ya uzamivu katika teknolojia ya habari na mawasiliani kwenye fani ya afya katika chuo kikuu cha Basel, Uswisi.
Mfumo wa masomo anayosomea ni ya mazoezi ya vitendo na ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya masomo. Alisema mfumo huo unamwezesha mwanafunzi kuendelea na kazi pia na unatoa nafasi ya kuoanisha masomo ya nadharia na vitendo.
Licha ya kuwa mtaalamu aliyebobea katika fani ya TEKNOHAMA, Mukasa ni kijana mwenye uelewa mpana kutokana na bahati aliyoipata katika kutembelea sehemu mbalimbali duniani.
Baadhi ya nchi alizotembelea kutokana na masomo, warsha na ziara za kikazi ni ndani na nje ya bara la Afrika, Kenya, Uganda, Ghana, Afrika ya Kusini, Uholanzi, Scotland, Uingereza, Ethiopia, Canada, Italia, Uswisi na Vietnam.
Vile vile amekwishafanya machapisho ya kisayansi 10 na kuongoza, kusimamaia, au kuandika miradi takriban 13 ya kitaalamu iliyostahili na kupata ufadhili mkubwa wa fedha.
Mukasa hayuko mbali sana kijamii kwani ni mjumbe wa kamati ya usimamizi na tathmini ya masuala ya kitaalamu ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Vile vile ni mwakilishi wa umoja wa kimataifa wa wanataaluma wa sayansi na teknolojia ya habari na mawasilino katika afya kanda ya Tanzania.
Hatua aliyoichukua Mukasa ni ya kuigwa na vijana wengine wa Tanzania waliobahatika kupata elimu. Changamoto kwa vijana na wasomi wengine nchini ni kushiriki kikamilifu katika kutatua matatizo yanayozikabili jamii kwa kuwa na wao ni sehemu ya matatizo hayo.