Huku Serikali ikidaiwa matrilioni, CCM yapanga hila kushinda uchaguzi 2015!
Na Sylivester Hanga
Toleo la 378
5 Nov 2014
KAMA ingekuwa nchi inaendeshwa kwa itikadi za kidini, ningethubutu kusema kuwa angalau siku hizi Mbunge wa Iramba (CCM) na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, "ameokoka".
Kauli yake ya wiki iliyopita kukiri kuwa Serikali inadaiwa na kuwa italipa zaidi ya shilingi trilioni 4 na ile ya mwanzo kuwa angetamani Bunge Maalumu la Katiba lisimame ili kuokoa fedha, zinamfanya aonekane anabadilika japo katika siasa watu hubadilika kila uchao.
Mwigulu alikuwa akizungumzia madeni lukuki yanayoikabili Serikali kiasi cha kufifisha huduma za afya na sekta nyingine za kijamii. Tatizo lake hasemi ni nini hasa kimekwamisha ulipaji wa madeni hayo, na jinsi fedha za makusanyo ya kodi zilivyotumiwa na zinavyotumiwa na watawala.
Tatizo sio kukopa kwenye mabenki ya kibiashara na mifuko ya jamii – japo hilo nalo ni kasoro kubwa kwa serikali inayojigamba kuwa uchumi unakua; bali tatizo ni namna fedha zilizokopwa zilivyotumika na zinavyotumika. Katika hili, Serikali imefeli; maana ufisadi umepamba moto kila kona, na kote zinazolengwa kuchotwa ni fedha za umma za makusanyo ya kodi.
Na tunavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, hali itakuwa mbaya zaidi. Kwa mambo yanavyokwenda hivi sasa serikalini, wananchi watarajie kupanda zaidi kwa ugumu wa maisha kuelekea mwaka wa uchaguzi wa 2015.
Kwa nini? Kwa sababu ni kawaida kwa wanasiasa wanaoutaka urais kutumia kila hila na ghiliba kuchota mapesa ya umma kwa ajili ya kuwania ubunge na urais; hata kama wanajua kuwa baada ya miaka 9 kupita ndani ya Ikulu watasema; "nimechoka natamani siku ziende upesi" (rejea kauli ya Kikwete ya hivi karibuni).
Huku kukiwa na mahitaji ya zaidi ya shilingi bilioni 270 kwa ajili ya kuboresha daftari la wapiga kura, uendeshaji wa kura ya maoni kuhusu Katiba Pendekezwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ufisadi ndani ya serikali ndiyo kwanza umepamba moto.
Ukiacha kashfa ya hivi karibuni ya Bunge kutumia vibaya fedha za umma kwa malipo yanayotia shaka, kashfa nyingine za ufisadi bado zinalitafuna taifa na kuzidi kuwachanganya wananchi.
Hivi karibuni, Zitto Kabwe na kamati yake ya Bunge anayoiongoza alimtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutoa taarifa kuhusu zilivyochotwa zaidi ya Sh. bilioni 200 kupitia akaunti ya Tegeta Escrow ya IPTL.
Hivi sasa Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama TAKUKURU na CAG wataitoa ripoti hiyo kwa wakati, na kama ripoti yenyewe itakuwa na tija kwa Watanzania au tija kwa mafisadi wachache ‘wanaokingiwa kifua' na Serikali kwa makusudi. Shaka ya wengi ni kwamba itakuwa sawa na ripoti nyingine zilizoishia kwenye makabati ya maofisi ya watawala wetu!
Wakati gharama za malipo ya kitanda katika hospitali kuu ya rufaa nchini ya Muhimbili zikitangazwa kupandishwa wiki iliyopita (na bila shaka huduma nyingine nazo zitapanda) kuna madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajiandaa kukijaza mapesa chama kipya cha siasa kilichoanzishwa hivi karibuni ili kiweze kuvuruga jitihada za vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) visifurukute na viondokewe na maelfu ya wanachama.
Hapo ndipo Tanzania yetu ya sasa ilipofikia. Yaani mahospitalini hakuna dawa, shuleni wanafunzi wanakaa chini, maabara hakuna na walimu hawana nyumba - bila kusahau akina mama wanaotembea Kilomita 10 kusaka maji, lakini bado chama tawala kinapanga mbinu ya kuchota fedha za walipakodi serikalini ili kufadhili chama kimoja kipya cha siasa kivuruge muungano wa vyama vya upinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao. Yaani CCM kinapanga hivyo kwa lengo la kukiwezesha tu kubaki madarakani milele na milele!
Ndiyo maana waliomtazama Katibu wa Propaganda wa CCM, Nape Nnauye, siku moja tu baada ya UKAWA kuweka msimamo wa kushirikiana kwenye uchaguzi mkuu ujao, walibaini kuwa ndani ya sakafu ya moyo wake alitambua kuwa jambo hilo litaikwaza CCM kwenye uchaguzi ujao, na hiyo ndiyo asili ya kutafuta mbinu ya kuuvuruga muungano huo mapema.
Kama habari za CCM kujipanga kukijaza mapesa chama hicho kipya cha siasa ni za kweli (ni dhahiri wahusika watakanusha tu), basi Watanzania wasitarajie kupungua kwa gharama za maisha katika sekta muhimu hadi baada ya mwaka 2015.
Nasema hivyo maana; chama hicho kipya kitapewa mamilioni ya fedha zilizochotwa kijanja serikalini (kama ilivyokuwa kwa EPA) ili ‘kukinunua' chama hicho kipya cha siasa kiuvuruge muungano huo wa UKAWA.
Si hivyo tu, mapesa hayo yatatumika pia ‘kuwanunua' wananchi wenye njaa, wasioweza kulipia kitanda hospitalini, wasioweza kulipa michango ya shule kwa watoto wao na wale wanaopenda sana kunywa pombe na kuvaa sare na leso za CCM ili wajiunge nacho.
Kwa kufanya hivyo, taarifa zinasema watakuwa wamepunguza nguvu za vyama vya upinzani; hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na CUF vinavyolengwa zaidi kufifishwa.
Ushauri wangu kwa hao watakaorubuniwa kwa fedha hizo chafu za CCM na serikali yake ni kuwa, kama hawawezi kuzikataa, basi wafuate ushauri wa Mzee Ndesa (Ndesamburo) kupitia kauli yake ile ya "pesa zao chukueni, kura kwa mwingine".
Na ndiyo maana tunaposema CCM kimepoteza dira yake, hatukionei; maana, kusema kweli, hivyo ndivyo kinavyoiendesha nchi tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, afariki Oktoba 14, 1999 – yaani kihila hila. Angelikuwepo hai Baba wa Taifa wanajua asingekubali mambo haya ya kupanga njama za kushinda uchaguzi kihila.
Vyovyote vile, itakuwa ni jukumu la wananchi wenyewe kuamua kupokea fedha hizo chafu ili wavibomoe vyama vya upinzani lakini baadaye waendelee kulipia gharama mpya za tiba, shule nk ama wazikatae, na hivyo kutoa fursa ya kuiondoa CCM madarakani mwaka 2015 na kuleta mageuzi ya kweli nchini.
Wakati mwingine huwa nawauliza vijana na wale wanaotetea mifumo isiyowasaidia wananchi wengi kuondokana na shida kuwa wanapata faida gani kwa kukumbatia yale yale na watu wale wale na chama kile kile (CCM) wakati dukani bei ya sukari, saruji, mabati, maharage, sabuni nk hupanda kila siku?
Na hiyo haijalishi kama wewe ni CCM, CHADEMA, CUF au TLP. Kama kungekuwa na utofauti wa bei kwa msingi wa uanachama wa vyama vya siasa, ningeelewa; lakini walio ndani ya vyama na wasio na vyama wote wanapigwa na bei zile zile kali zisizoendana na vipato vyao.
Nimalizie kwa kusema kuwa, wakati Serikali ikidaiwa matrilioni ya pesa na mifuko ya jamii karibu yote nchini, na pia wafanya biashara wanaotoa huduma mbalimbali, inasikitisha kuwa upande wa pili inashindwa kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuchagua vipaumbele stahiki.
Busara inahitajika hivi sasa kuamua nini kinatangulia. Ni kuandaa daftari la wapiga kura kwanza, kufanya chaguzi za serikali za mitaa, na kisha baadaye uchaguzi mkuu au kura ya maoni kuhusu Katiba Pendekezwa itangulie kabla ya Uchaguzi Mkuu au kura hiyo isubiri mwaka 2016 ili kwanza hospitali zipate madawa na shule zitoe huduma stahili?
Kura ya maoni kuhusu Katiba tata inayopendekezwa inawezaje kuwa ndiyo kipaumbele cha matumizi ya fedha za umma katika nchi ambayo karibu mahospitali yote nchini (ikiwemo hospitali kuu ya Muhimbili) hayana madawa na watu wanakufa kila siku?
- See more at:
Raia Mwema - Huku Serikali ikidaiwa matrilioni, CCM yapanga hila kushinda uchaguzi 2015!