Mdondoaji, ulivyoanza nimedhani niko ndani ya Bunge Maalum La Katiba! Huko ndipo watu badala ya kujadili hoja kama zilivyowasilishwa mbele yao na Tume, wamejikita katika mipasho, kejeli na matusi. Naomba na mimi nikuuulize; ni wapi pahala muafaka unadhani haya maswali yako yangefaa yaulizwe na majibu kutolewa? Nitakujibu; ni ndani ya Bunge Maalum La Katiba. Je ni kwa nini hili halikutokea? Nitakusaidia tena; ni kwa sababu hilo bunge limetekwa nyara na watu ambao lengo lao kubwa ni kuhakikisha maoni ya wananchi kupitia Tume yanapuuzwa, watu ambao kwa mtizamo wao rasimu imewatia hofu na watu ambao usalama wa maslahi yao yanalindwa ndani ya mfumo wa serikali mbili.
Mdondoaji, kusema kweli wengi wanaounga mkono rasimu kama ilivyotolewa na Tume ni watu ambao mwanzoni walikuwa na imani kubwa kuwa siku moja tutafanikiwa kuwa na Muungano wa kweli,
wa nchi moja, Tanzania. Tuliamini kuwa iko siku tutaweza kusahau tofauti zetu na kutanguliza utaifa wetu (Utanzania) na kwamba mfumo wa serikali mbili ulikuwa ni wa mpito tu kuelekea serikali moja. Waasisi waliweka msingi na tuliamini kwa pamoja tutaendeleza ujenzi, tofali kwa tofali, hadi nyumba ikamilike! Ambacho hatukujua ni kwamba
in reality we were living a lie kwani ingawa nyufa zilianza kuonekeana toka mapema kabisa, tuliziba macho...
wishing them to go away and they never did!
Mdondoaji, siku zilivyosogea ndivyo na nyufa zilivyozidi kujitokeza bila jitihada zozote za dhati kufanyika kurekebisha hali hiyo zaidi ya kuzipaka rangi zionekane kama vile zimeboreshwa. Mwaka 2010 upande moja katika Muungano ukaamua kuubomoa msingi wa Muungano kwa kuanzisha nchi ndani ya nchi, kitendo ambacho hakikubaliki kabisa katika nchi inayoendeshwa kwa kufuata sheria. Kwa miaka karibu mitano tuna chama tawala kimoja, serikali mbili
na nchi mbili; nchi moja inaitwa
Tanzania na nchi nyingine inaitwa
Zanzibar. Ingawa nchi mbili zilizoungana mwaka 1964 ni
Tanganyika na
Zanzibar, ajabu ni kwamba kwa sasa tunazo nchi mbili,
Tanzania na
Zanzibar!
Mdondoaji, Tume ilitembea nchi nzima ikikusanya maoni ya wananchi na hakuna ushahidi wowote kwamba wana CCM ama walibaguliwa au maoni yao hayakuzingatiwa. Je huu msimamo wa CCM kuhusu serikali mbili ulipatikanaje? Na wao waliunda tume yao ama ni viongozi wachache tu walijifungia wakatunga rasimu mbadala?
Akizindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiunda yeye mwenyewe siku ya
Ijumaa, Aprili 6 mwaka 2012 , Raisi Kikwete aliitaka Tume kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya mchakato wa kuunda Katiba mpya. Lakini siku akizindua Bunge Maalum La Katiba baada ya Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha rasimu, Raisi huyo huyo alishambulia mapendekezo ya Tume akiapa serikali tatu haitawezekana
"under his watch!"
Swali linalojitokeza hapa ni
kwa nini Tume iliundwa? Hili swali nalo linazua swali,
kwa nini Bunge Maalum La Katiba nalo liliundwa? Ningetegemea kwamba kazi ambayo ilitakiwa ifanywe na Bunge hili ni kujadili rasimu na kutafuta ufafanuzi pale ambapo kuna maswali kama haya uliyouliza
Mdondoaji! Mtu au watu wa kutoa ufafanuzi ni wale waliohoji wananchi na kupata maoni yao nao ni
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini kwa unafiki, wajumbe wa BMLK kutoka CCM, wameamua kuunga mkono msimamo wa Raisi badala ya msimamo wa wananchi. Nachelea kusema kuwa kama Raisi angeunga mkono rasimu, hao hao wanaombeza Jaji Warioba leo wangekuwa wanampigia makofi wakimsifia.
Mdondoaji, kuna sehemu umetoa eti unazoita takwimu kuhusu gharama za kuendesha serikali kwa kuzingatia bajeti zetu za sasa, My God! Ubadhirifu uliomo na unaodhihirika siku hadi siku ndani ya uendeshaji wa serikali naweza kusema bila kumung'unya maneno kwamba ni matokeo ya mkanganyiko uliotanda katika utekelezaji. Mfumo wa serikali mbili umeruhusu na kusababisha ubadhirifu mkubwa kwa ukosefu wa uwajibikaji; nani anamsimamia nani ndani ya serikali ya Tanganyika (Tanzania bara) iliyojivika koti la Muungano? Kwa mtindo huu ufanisi utawezekanaje? Mfano mzuri tu ni bajeti ya Waziri Mkuu, ni wapi mambo ya Muungano yanapoishia na yale yasiyo ya Muungano yanapoanzia?
Namalizia kwa kusema laiti Bunge Maalum la Katiba lingekuwa na nia njema ya kutupatia katiba mpya, lingejikita katika kujadili mapendekezo yaliyotolewa na Tume na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa wahusika inapobidi. Lakini kwa kutanguliza maslahi ya chama mbele ya Taifa, CCM haitutakii mema sisi wananchi tuliotoa maoni kupitia tume ambayo kwa bahati mbaya CCM wanaiita Tume ya Warioba. Tume hii ama ilitakiwa iwe sehemu ya hili Bunge Maalum la Katiba au iwe tayari kuitwa kwa mahojiano wakati wowote utata unapojitokeza kuhusu mapendekezo waliyoyatoa. Kumsulubu Warioba bila kumpa nafasi ya kujitetea ndani ya BMLK ni njama za kuteka haki ya wananchi.