Timu ya Taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars leo saa 6.30 mchana inashuka kwenye Uwanja wa Mandela ulioko kitongoji cha Nambole mjini hapa kukwaana na timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati inayoendelea.
Kilimanjaro Stars inacheza nusu fainali hiyo baada ya kushika nafasi ya pili katika Kundi A, huku Kenya wakiibuka vinara wa Kundi B. Mchezo unaotarajiwa kuonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha kulipia cha GTV kupitia chaneli yake ya G Sport 1.
Mchezo wa pili wa nusu fainali utachezwa saa 9.30 alasiri kati ya mabingwa mara tisa Uganda na Burundi. Kocha wa Kilimanjaro Stars, Marcio Maximo amesema litakuwa pambano gumu lakini la kupendeza litakalohitaji mbinu za hali ya juu na wachezaji kutekeleza majukumu yao sawasawa, ili kuweza kucheza fainali hapo Jumanne Januari 13.Mwamuzi wa mchezo huo ni Hassan Haile wa Somalia akisaidiwa na Felicien Kabanda wa Rwanda na Hussein Bugembe wa Uganda.
Kenya ni wazuri wanagongeana vema hasa sehemu ya kiungo kwa ajili ya kujenga mashambulizi, lazima kuwadhibiti kwa kutumia mbinu sahihi, alisema Maximo wakati akizungumzia mchezo huo wa leo. Sehemu ya kiungo ya Harambee Stars inao wachezaji wazuri akiwemo mchezaji mpya wa Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Osbone Monday huku sehemu ya ushambuliaji ikiongozwa na mchezaji mpya pia wa Azam, Francis Ouma.
Kocha Maximo anatarajiwa kuwakosa wachezaji wake wawili katika safu ya ulinzi ambao wamekuwa wakicheza vizuri katika michezo ya makundi. Wachezaji hao ni Kevin Yondan aliyeonyeshwa kadi nyekundu wakati wa mchezo dhidi ya Uganda na Shadrack Nsajigwa ambaye ana kadi mbili za njano alizozipata katika michezo dhidi ya Rwanda na Uganda.
Hali hiyo na ikizingatiwa mlinzi mwingine wa kati Meshack Abel bado anakabiliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, kocha Maximo amemteua kiungo Henry Joseph kucheza sehemu ya ulinzi wa kati pamoja na Salum Sued, mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za kimataifa (43) katika kikosi cha Maximo. Shaban Nditi ndiye atacheza nafasi ya kiungo iliyoachwa wazi na Henry.
Pia Nurdin Bakari ambaye amekuwa akitumiwa na Maximo katika sehemu ya kiungo ndiye amepewa jukumu la kuziba nafasi ya Nsajigwa. Shaban Dihile ana uwezekano mkubwa wa kurejea langoni baada ya kukosa michezo miwili dhidi ya Rwanda na Uganda, ambayo mlinda mlango namba mbili Deogratius Munishi Dida mwenye umri wa miaka 19 alitekeleza majukumu yake vilivyo licha ya kufungwa magoli mawili na Waganda.
Hakuna mabadiliko zaidi yanayotarajiwa katika kikosi cha Maximo. Hivyo iwapo hakutakuwa na dharura ya dakika za mwisho sehemu ya ulinzi kushoto itaendelea kudhibitiwa na Juma Jabu, Geofrey Bony ataendelea na majukumu yake sehemu ya kiungo, Athuman Idd atacheza pembeni kushoto, winga ya kulia Mrisho Ngasa, washambuliaji wa kati ni Danny Mrwanda na Haruna Moshi.
Pambano la Tanzania Bara na Kenya linatarajiwa kuwa na upinzani wa aina yake kutokana na historia ya timu mbili hizo zinapokutana hususan katika michuano ya Chalenji.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania na Kenya kukutana katika hatua ya nusu fainali ya michuano hii tangu ilipopewa jina jipya la Senior Challenge Cup mwaka 1973. Mara ya kwanza na mwisho ilikuwa mwaka 1975 wakati michuano hiyo ilipofanyika Zambia. Kenya ilishinda mchezo huo kwa magoli 2-1.
Mchezo huo unakumbukwa sana kutokana na vituko vilivyokuwa vikifanywa na wachezaji wa Kenya dhidi ya washambuliaji hatari wa Tanzania Bara, Kitwana Manara na Gibson Sembuli huku lango likilindwa vilivyo na Athuman Mambosasa.
Lakini Watanzania watakuwa wanakumbuka kwa machungu zaidi michezo miwili ya fainali ya Chalenji iliyofanyika katika ardhi ya Tanzania na Kenya kutoroka na kombe huku Watanzania wakiwa hawaamini.
Hiyo ilikuwa mwaka 1981 wakati goli la James Ouma Jakaranda lilipowazima Watanzania kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Kikosi cha Kenya wakati huo kilikuwa na wakali kadhaa wakiwemo Mahmoud Abbas, JJ Masiga na Bob Ogora.
Na mwaka 2002 Kenya ikarejea kile ilichokifanya miaka 21 iliyokuwa imetangulia kwa kuifunga Kilimanjaro Stars magoli 3-2 kweye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza uliofurika mashabiki waliokuwa na matarajio makubwa na timu yao hasa baada ya kuwafunga Kenya goli 1-0 katika mchezo wa ufunguzi.
Goli la ushindi la Kenya lilitiwa kimiani na mshambuliaji kinda wa Mathare United wakati huo Denis Oriech ambaye sasa anakipiga katika klabu ya Auxerre huko Ufaransa.
Tanzania Bara imetwaa ubingwa wa Chalenji mara mbili, (1974 na 1994) na kupoteza michezo ya fainali mara tano (1973, 1980, 1981, 1992 na 2002) haijawahi kufuzu kucheza nusu fainali tangu mashindano hayo ya mwaka 2002 huku mara mbili (2006 na 2007) ikitolewa katika hatua ya robo fainali.
Mungu Ibariki Tanzania...