Baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, wametangaza msimamo wa kutoshiriki mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, John Heche, unaotarajiwa kufanyika jimboni humo.
Wanachama hao wameweka sharti kuwa Heche anapaswa kwanza kutoa ufafanuzi wa kina na kuomba radhi kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kabla ya kufanya mkutano wowote jimboni hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari, aliyetambulishwa kama Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jimbo la Hai, Humphrey Munisi, alisema kutoridhishwa kwao kunatokana na kauli anazodai zilitolewa na Heche hivi karibuni wakati akizungumzia masuala ya maridhiano ya kisiasa.
Kwa mujibu wa Munisi, kauli hizo zimeibua maswali mazito na taharuki miongoni mwa wanachama kuhusu heshima na thamani inayogawiwa kwa viongozi waandamizi waliotangulia na waliokipigania chama hicho kwa miaka mingi.
Amesisitiza kuwa tofauti za kimawazo ndani ya chama zinapaswa kutatuliwa kwa hoja na mazungumzo, badala ya kutumia lugha zinazoweza kudhalilisha viongozi au kuongeza mgawanyiko miongoni mwa wanachama.
Aidha, Munisi amemtaka Heche kufafanua kauli inayolalamikiwa na kuomba radhi kwa Mbowe kabla ya kutarajia kuungwa mkono na w anachama wenye msimamo kama wake, akieleza kuwa heshima kwa viongozi ni sehemu muhimu ya kulinda mshikamano wa chama.
Ameongeza kuwa CHADEMA ni taasisi inayopaswa kujengwa kwa misingi, nidhamu na hoja, huku akimtaka Heche kukemea makundi yanayotumia lugha za matusi dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Hata hivyo, haijabainishwa iwapo msimamo huo unawakilisha viongozi na wanachama wote wa CHADEMA Jimbo la Hai au ni msimamo wa Munisi na baadhi ya wanachama wanaounga mkono hoja zake.
Vilevile, ufafanuzi wa John Heche kuhusu kauli inayolalamikiwa, pamoja na msimamo wake kuhusu wito wa kuomba radhi, unahitajika ili kutoa nafasi kwa upande wake kueleza hoja zake kabla ya mkutano huo kufanyika.
Hata hivyo banana fm imeendelea kuwatafuta viongozi wa Chadema Hai kupata ufafanuzi zaidi wa madai hayo huku
@hechejohn akitarajiwa kufanya mkutano Mkubwa wa hadhara Mjini Bomang'ombe Hai Kilimanjaro Kesho Jumapili Oktoba 18, 2026.
Chanzo :Banana fmtz