Basi wahariri wetu ni bogus kabisa wanakosea toka
Heading: Wabunge waliogongana Richmond warudishwe
Hadi conclusion:Ni kwa sababu hiyo ninaamini wabunge wafuatao warudishwe bungeni
Ngoja na mimi ni conclude, huwa napenda sana kufuatilia vitu na huwa si mvivu wa kutafuta facts popote zilipo ni utamaduni wangu niliojijengea labda kwa vile ni field yangu. Nilikuwa nataka nione stance yako juu ya kura za maoni ni vizuri umesema ziheshimiwe lakini nilipoangalia Makala yako ilikuwa contrary, kwa vile umesema kosa ni la mhariri nitaenda na hilo, na kwa kujiridhisha nimetoa hint hapo juu kwamba inawezekana mhariri alikosea vyote viwili heading na conclusion kitu ambcho ni nadra sana kutokea ili mbeleni nisije kujikuta mjinga kwa kukubali kitu nisichokuwa na uhakika nacho.
Hapana hakukosea Heading; heading ni yangu. Kuna maneno ambayo si yangu: Makala ya awali niliyotuma kwa mhariri ni hii hapa:
WABUNGE WALIOGONGANA SUALA LA RICHMOND WARUDISHWE BUNGENI
Na. M. M. Mwanakijiji
Leo Chama cha Mapinduzi nchini kinapiga kura ili kuweza kuanza mchakato wa kujua ni kina nani watakuwa wagombea wa chama hicho kwenye nafasi za udiwani, uwakilishi na Ubunge kwa kipindi kijacho cha miaka mitano. Mamia ya wana CCM watajitokeza kupiga kura ili kutoa mapendekezo yao katika utaratibu wa kura za maoni ambapo wanachama mbalimbali wamejitokeza kugombea wengine ikiwa ni marudio na wengine ikiwa ni mara ya kwanza.
Tukiondoa taarifa ambazo tumezisikia hasa wiki hii iliyopita hasa mazingaombwe ya TAKUKURU na wale wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa masikio ya wachunguzi wengi wa kisiasa nchini yanabakia katika kundi la watu wachache ndani ya CCM ambao kwa takribani miaka miwili sasa limekuwa katika mgongano mkubwa. Leo kumbe ndiyo ile leo ni leo ya kwenye methali kwa kundi hili. Hili ni ku kundi ambalo lilijikuta linakipasua Chama cha Mapinduzi kufuatia sakatala la kashfa ya Richmond na masuala mengine ya ufisadi.
Kufuatia sakata hilo la Richmond na baadaye suala la Rais Mstaafu Mkapa na mgodi wa Kiwira wana CCM walijikuta wakigawanywa na kuwa na makundi makubwa mawili. Wale ambao wanaamini aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye alijiuzulu kufuatia kuhusishwa na kashfa ya Richmond kuwa alionewa na wale ambao wanaamini kabisa kuwa Kamati Teule ilimwonea Waziri huyo Mkuu kwa kutompa nafasi ya kujitetea. Mpasuko huo ukatiwa nguvu na mpasuko wa kundi la wabunge ambao waliamini kuwa aliyekuwa Rais wa Tanzania Bw. Ben Mkapa alitumia madaraka vibaya pale alipodaiwa kujipatia mgodi wa Kiwira yeye, familia yake na watu wake wengine wa karibu. Suala hilo la kujipatia mgodi kinyemela liliwafanya baadhi ya wabunge wadai kuwa Rais huyo mstaafu avuliwe kinga ili hatimaye aweze kulazimishwa kujibu katika mahakama ya Sheria.
Kati ya masuala hayo mawili yakaibuka masuala mengine yatokanayo na hayo hasa pale ambapo vyombo mbalimbali vya habari vilipojikuta vinalazimishwa kuchukua upande aidha kwa sababu za kiitikadi au vikiwa vinasukumwa na wamiliki wake au na watu wenye maslahi ya kifedha na vyombo hivyo kiasi kwamba mgongano wa kisiasa ulivuka mipaka na kuwa mgongano wa binafsi katika ya makundi mbalimbali ya waandishi wa habari, wanasiasa, wafanyabiashara na kulazimisha jamii vile vile kuwa na pande mbili kuhusiana na masuala hayo.
Kinyume na ambavyo ilitarajiwa kwamba hatimaye mpasuko huo wa kimaslahi ndani ya CCM ungesababisha kundi moja kujitoa hali halisi ni kuwa siku ya leo imefika huku makundi yote mawili yakiwa na mashabiki na wapambe wake yakiwa yameshikana mapembe kama ngombe wagombanao na hakuna aliye tayari kumuachia mwingine. Ukiondoa kujiondoa kwa mmoja wa kundi hilo Bw. Fred Mpendazoe ambaye alijiunga na CCJ na baadaye Chadema, makundi yote mawili yameonekana kujitokeza kugombea tena nafasi za ubunge.
Katika kipindi hiki kilichopita kundi moja lile linalojulikana kuwa la wapiganaji CCM limekuwa likilalamika kuwa kundi jingine la mafisadi limekuwa likijaribu likitumia mbinu mbalimbali ili kufanya wanachama hao wa kundi la kwanza kushindwa katika chaguzi za ndani za CCM na kuwa wasipate nafasi ya kuweza kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Hapo awali kauli hizo zimekuwa zikipuuzwa na vyombo vya dola na hakuna hata mtu mmoja ambaye ameweza kuonesha ushahidi wowote kuwa kumekuwa na mchezo mchagu kwenye majimbo mbalimbali zaidi ya tuhuma tu. Hata pale ambapo baadhi ya watu wametuhumiwa kuwa wametumwa na mafisadi kugombea ukweli unabakia kuwa hakuna ushahidi wowote aidha wa maandishi, picha, sauti, au vielelezo vingine ambao umeweza kutolewa kushawishi jamii kuwa kumekuwa na mchezo mchafu.
Japo hakuna ushahidi wa hilo haina maana jambo hilo halikuwepo. Tukichukulia taarifa za watu mbalimbali kukamatwa katika matukio mbalimbali yanayotajwa kuwa na mazingira ya rushwa wiki iliyopita ni wazi kuwa aidha kuna mtu anachezea akili za taifa zima au tuna vyombo vibovu kabisa vya kusimamia sheria. Inashangaza kuwa baada ya taarifa ya kamata kamata ya wiki iliyopita hadi leo siku ya uchaguzi hakuna mtu HATA MMOJA ambaye amefikishwa mahakamani kwa kosa lolote la kutoa au kupokea rushwa na wote wameachwa (hata wale tulioambiwa wamehojiwa usiku kucha) kushiriki uchaguzi.
Hivyo basi, kama TAKUKURU, Polisi na wale wenye kuwaamuru wameona kuwa makosa yote ambayo yamefanyika hayakuwa na ushahidi mzito wa kumpeleka mtu yeyote mahakamani na hivyo kuwaacha wagombea wagombee na kupigiwa kura basi ni budi niseme kwamba jaribio lolote la kuleta mashtaka baada ya kura za maoni ni upotoshaji mkubwa wa demokrasia na ni kuchezea utawala wa sheria. Ninachosema ni kuwa TAKUKURU na Polisi wasiwachezee Watanzania kwa kujaribu kuvuruga mchakato wa kuwapata wagombea ndani ya CCM hasa kwa kutoa taarifa kwa kamati mbalimbali za CCM kuwa fulani na fulani alifanya hivi na vile wakati wa kura za maoni.
Hilo likishaeleweka hatuna kukubali jambo jingine ambalo ni muhimu kuwa wale wabunge wote ambao waligongana Bungeni kwenye masuala ya Richmond, Mkapa na Kiwira wana CCM wataona ni bora wawarudishe tena Bungeni. Ninaamini kabisa kuwa itakuwa ni makosa makubwa kwa wana CCM kutowarudisha wabunge hao wote kwani kwa kufanya hivyo kutawapa ushindi kundi moja nje ya Bunge.
Binafsi sipendi ushindi wa mezani. Kwa vile CCM imeshindwa kutafuta suluhu ya makundi haya licha ya kuundwa kwa kamati ya Mzee Mwinyi basi kujaribu kutafuta suluhu nje ya Bunge litakuwa ni kosa kubwa zaidi. Fikiria kwamba Bunge lijalo linakuja halafu Mwakyembe na Selelii wametupwa nje huku Rostam na Lowassa wakiwa wameingia tena (kama inavyotarajiwa) je hawatotumia nafasi zao Bungeni kuhakikisha wabaya wao wanashughulikiwa na hata kutumia mtindo wa Kamati Teule kuweza kujisafisha zaidi? Japo hilo ni jambo zuri kwa upande mmoja mimi ninaamini tusiwaachie haya makundi mawili yakwepane.
Wana CCM wanajukumu la kuwarudisha wabunge wote waliohusika na masuala haya Bungeni ili wakamalizane Bungeni kwani hakuna atakayepewa ushindi wa chee. Sitaki tufike mahali Rostam na Lowassa wapoteze Ubunge halafu kina Mwakyembe na Selelii wakirudi Bungeni waamue kuwamaliza kabisa bila ya wao kupata nafasi ya kujitetea.
Kwa vile suala hili lilianzia Bungeni ni lazima liishie Bungeni na hakuna ujanja wa njia za mkato. Ninaamini wale wagombea wengine waliojitokeza katika majimbo ya wabunge hawa watakuwa ni wasindikizaji wazuri na wametoa changamoto nzuri lakini wana CCM watatambua kuwa kinachogombaniwa ni zaidi ya majimbo ya kisiasa. Wananchi katika majimbo yote yenye wabunge hawa wapambani na wale wenye kulaumiwa watatambua kuwa suala ambalo limelikabili taifa kwa miaka hii miwili ni kubwa mno kiasi kwamba kama ingekuwa ni mechi ya soka basi ningeweza kusema kilichopita ni kipindi cha kwanza tu. Katika kipindi hicho timu moja imefungwa magoli mawili.
Wana CCM kwenye kura za maoni watafanya makosa makubwa endapo wataamua kuondoa wachezeaji uwanjani badala ya kuja na kumaliza kipindi cha pili ati kwa vile wameonewa na kufungwa mabao mawili. Timu yenye akili ni ile inayokuja kwenye kipindi cha pili kwa nguvu zaidi na mbinu mpya ili kujibu mashambulizi huku ile timu nyingine nayo ikijipanga vizuri zaidi kulinda magoli yao na ikibidi kuongeza mengine.
Ni kwa sababu hiyo ninaamini wabunge wafuatao warudishwe Bungeni ili wakamalizie mechi yao kwani katika Tanzania ya leo, hakuna ushindi wa chee au wa kubebwa.
Edward Lowassa (Monduli)
Rostam Aziz (Igunga)
Peter Serukamba (Kigoma Mjini)
Anne Kilango Malecela (Same Mashariki)
Dr. Harrison Mwakyembe (Kyela)
Lucas Selelii (Nzega)
Aloyce Kimaro (Vunjo)
Said Juma Nkumba (Sikonge)
Wana CCM wafanyie taifa hisani kwa kurudisha kundi hili zima Bungeni ili wakamalizie mechi waliyoianzisha. Jaribio lolote la taratibu za kichama kumwengue yeyote hapo ni kujaribu kuipatia timu moja ushindi wa mezani. Tuwaache wote hawa warudi wakagongane tena huko Bungeni au wakapatane. Ushindi wa chee hakuna.
Niandikie:
Mwanakijiji@jamiiforums.com