TAARIFA KWA UMMA
DONDOO ZA MAAZIMIO YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA CHADEMA
Taarifa hii ni kuwajulisha wanachama wa CHADEMA na watanzania kwa ujumla kuwa Baraza Kuu la CHADEMA lilifanya kikao chake katika kawaida cha kila mwaka siku ya jumanne tarehe 18 Disemba 2007 katika ukumbi wa Hoteli ya Land Mark Dar es salaam.
Ajenda katika kikao hicho zilikuwa: Kuthibitisha Muktasari wa kikao cha Baraza Kuu cha tarehe 12 Agosti 2006 na yatokanayo na muktasari huo; Taarifa ya Katibu Mkuu; Taarifa ya Fedha; Mpango Kazi na Bajeti; Kanuni za Umoja wa Madiwani; Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa CHADEMA mwaka 2008; Taarifa ya Ushirikiano wa Vyama na Kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti(Bara).
Zifuatazo ni dondoo za msingi kuhusu maazimio yaliyofikiwa na kikao cha Baraza Kuu kuhusu ajenda mbalimbali zilizojadiliwa:
Baraza kuu limepokea, kujadili na kupitisha taarifa ya Katibu Mkuu
Taarifa hii kwa pamoja na mambo mengine imejumuisha kazi mbalimbali ambazo CHADEMA imezifanya katika mwaka 2007. Taarifa hii imehusisha pia taarifa za kurugenzi mbalimbali za makao makuu ya CHADEMA. Baraza kuu limesikitishwa na taarifa potofu za magazeti zenye kulenga kujenga taswira kwamba kuna mgogoro. Baraza kuu limepokea na kutathmini Ziara ya helikopta ya kushukuru wananchi, kuhamasisha uwajibakaji wa serikali na kujenga chama na kubaini manufaa yaliyopatikana kutokana na ziara hiyo kwa CHADEMA na kwa taifa.
Baraza kuu imejadili na kupokea taarifa ya fedha ya CHADEMA
Taarifa hii imehusisha mapato na matumizi ya CHADEMA katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Baraza kuu limetafakari gharama za ziara za helikopta na kuwianisha na ziara nyingine na kuazimia kwa kauli moja kuendelea na kutumia helikopta katika za awamu nyingine za CHADEMA kama ambavyo iliazimiwa pia na Mkutano Mkuu wa CHADEMA mwaka 2006.
Baraza Kuu limepokea, kujadili na kupitisha Mpango Kazi na Bajeti kwa mwaka 2008:
Mpango Kazi na Bajeti unajumuisha Shughuli mbalimbali ambazo zimepangwa kufanya katika mwaka 2008 pamoja na bajeti ya kutekeleza mpango huo. Mpango Kazi huo utahusisha shughuli ambazo zitafanywa pia na kurugenzi mbalimbali za chama katika masuala ya utawala, uenezi, habari, sheria, bunge, halmashauri,vijana, wanawake, wazee, rasilimali, oganizesheni, mafunzo, mahusiano ya kimataifa nk.
Baraza Kuu limepokea, kujadili na kuthibitisha Taratibu Umoja wa Madiwani wa CHADEMA
Mwongozo wa Umoja wa Madiwani wa CHADEMA(UMC) unajumuisha madhumuni, uanachama, muundo na masuala mengine muhimu yanayohusu taratibu za umoja wa madiwani wa CHADEMA umeridhiwa. Umoja huu ambao wanachama wake ni kila diwani wa CHADEMA utawaunganisha madiwani wa CHADEMA vizuri zaidi katika kutekeleza wajibu wao katika maeneo wanayowakilisha na kwa chama kwa ujumla.
Baraza kuu limepokea na kujadili taarifa ya ushirikiano wa vyama
Taarifa ya ushirikiano ilijumuisha makubaliano na kazi mbalimbali ambazo zimefanywa na ushirikiano wa vyama vya siasa vya upinzani vya CHADEMA, CUF, TLP na NCCR Mageuzi imepokelewa. Baraza kuu limeazimia kuwa CHADEMA iendelee na ushirikiano wa vyama kwa lengo la kudumisha demokrasia nchini, kuunganisha nguvu katika kutetea maendeleo na hatimaye upinzani kuweza kuchukua dola.
Baraza kuu limepokea, kujadili na kupitisha Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa CHADEMA mwaka 2008:
Ratiba ya uchaguzi mkuu wa CHADEMA imepitishwa rasmi ambapo uchaguzi utafanyika mwaka 2008. Baraza Kuu lilipitisha azimio la kutangaza ratiba ya uchaguzi(Ratiba hiyo imeambatanishwa pamoja na Taarifa hii kwa umma, maelekezo zaidi kuhusu uchaguzi huo yatatolewa baadaye).
Baraza Kuu limefanya uchaguzi na kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti(Bara).
Baraza kuu lilifanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti(Bara). Wagombea wa nafasi hiyo walikuwa: Chacha Zakaya Wangwe(Mb) aliyepata kura-56. Na Said Amour Arfi(Mb) aliyepata kura:- 38 na hakuna kura ambayo iliharibika. Hivyo kwa matokeo hayo Chacha Wangwe(Mb) alitangazwa rasmi kuwa Makamu Mwenyekiti(Bara).
Taarifa hii imetolewa 20/12/2007 na:
Freeman Mbowe
Mwenyekiti Taifa