Zitto sasa kama 'upupu' CHADEMA
Habari Zinazoshabihiana
• Hiza, Akwilombe watumika kummaliza Zitto 27.09.2007 [Soma]
• Polisi yachunguza kauli za Mbowe, Kabwe 07.09.2007 [Soma]
• CHADEMA wafadhaishwa na sakata la Kabwe, Amina 11.05.2007 [Soma]
*Kamati Kuu yatabiriwa 'kutofua nazi' Jumamosi
*Akigawa chama katika makundi na aitwa 'fisadi'
Na Mwandishi Wetu
KAMATI Kuu ya CHADEMA ambayo inatarajiwa kukutana Jumamosi ijayo kujadili pamoja na mambo mengine ushiriki wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, katika Kamati ya Kuangalia Upya Mikataba ya Madini nchini, inaweza isibadili msimamo wa Mbunge huyo, imebainika.
Hatua hiyo inatokana na mbunge huyo kusimamia upande wa kutetea maslahi ya Taifa na si yake binafsi, hali ambayo imesababisha mtafaruku ndani ya chama chake na kuzaa kambi mbili, moja ikitetea msimamo wake na nyingine ikiupinga.
Habari zilizopatikana ndani ya chama hicho jana, zilisema wakati muasisi wa chama hicho, Bw. Edwin Mtei, akimtetea Bw. Zitto kuendelea kushiriki ndani ya Kamati hiyo, Mbunge wa Tarime, Bw. Chacha Wangwe, anaonekana kukereka.
"Kibaya zaidi hata kama mlivyoona jana kwenye magazeti sasa Wangwe anahisi kuwa Bw. Zitto amepewa 'kitu kidogo' na CCM ili akubali kuwa ndani ya Kamati hiyo...kosa ni nini kama ndicho tulikuwa tukikipigia kelele hata bungeni?," alihoji Bw. Mathayo Lazaro aliyejitambulisha kuwa mwanachama wa CHADEMA.
Alisema yatakuwa ni maajabu kwa Bw. Zitto kujitoa katika Kamati hiyo wakati ndiye aliyewasilisha hoja binafsi kuhusiana na mikataba ya madini na kuibua suala la Buzwagi.
Ndani ya CHADEMA tayari kuna hisia kuwa CCM ina mpango wa kukisambaratisha chama hicho na ndiyo sababu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, akamwingiza Bw. Zitto katika Kamati hiyo na yeye kukubali na kumpongeza Rais.
Hatua hiyo ilisababisha hasira miongoni mwa viongozi na wanachama wa CHADEMA ambao walieleza kushangazwa kwao na Bw. Zitto kumsifia na kumpongeza kiongozi wa chama tawala.
Akisisitiza msimamo wake wa kutaka kuona Bw. Zitto akiendelea kubaki ndani ya Kamati hiyo, Bw. Mtei alikaririwa akisema hiyo ni fursa nzuri kwa chama chake kufikisha maoni na msimamo wake serikalini.
Watu wa karibu na Bw. Zitto wanaofahamu msimamo wake, walisema Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake cha Jumamosi isipokuwa makini itakuwa imemegua jiwe moja muhimu katika msingi wake.
"Inaonekana Zitto hawamwelewi vizuri ni mtu mwenye msimamo na mbishi constructively (enye manufaa), hawezi kusimamia katika ubishi wa kijinufaisha binafsi, ingawa anaweza kutumiwa na wengine kujinufaisha,wasipomwelewa kama anavyoamini yeye watamkosa," alisema mwana CHADEMA mwandamizi ambaye hakutaka atajwe gazetini.
"Tayari tunaona hivi sasa anahusishwa na ufisadi, huyu ni yule ambaye baada ya kusimamishwa kazi bungeni, alipitishwa mikoani kama Mwenge wa Uhuru...leo anapewa nafasi nzuri ya kulitetea Taifa, anaanza kusakamwa eti kanunuliwa, mbona hatutaeleweka wana CHADEMA?," alihoji mwanachama huyo.
Baadhi ya wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema ingekuwa bora kama CHADEMA ingelichukulia suala hili kwa umakini mzuri kwani kumbadilisha Bw. Zitto kunaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa na hata chama hicho kumeguka.
"Mambo ya siasa huanza hivi hivi, huwezi kujua, mbunge huyu machachari wa CHADEMA anaangalia wapi na ana hisia zipi ndani ya chama chake, alikuwapo Dkt. Walid Kabourou, akiwa na wafuasi wengi tena Kigoma, yuko wapi sasa? Na huyu ni wa huko huko!
"Tumesikia, wazee wa Kigoma wao wanataka aendelee kubaki ndani ya Kamati, sasa hicho kikao cha Jumamosi kitasaidia nini? Kama si cha kubadili msimamo wa Bw. Zitto, sawa kifanyike, lakini kama ni kinyume chake, hatudhani kama Zitto atakubali kuwa kinyonga kwa hili," alisema Bw. Elibariki Ulotu, aliyejitambulisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Wakati huo huo, Reuben Kagaruki, anaripoti kwamba
Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema, amesema hatua ya Rais Kikwete kumteua Bw. Zitto kwenye Kamati huyo kunalenga kuwagombanisha katika umoja wao.
"Kamati aliyounda Rais Kikwete ni ya 'magrini' itatufanya tugombane na kutugawa bure."
Bw. Mrema alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na gazeti hili kwa simu alipoombwa atoe maoni yake kuhusiana na hatua ya Rais Kikwete kumteua mbunge huyo kuwa katika Kamati hiyo.
Bw. Mrema alisema hawezi kumzungumzia, lakini anajua wazi kuwa Kamati hiyo haiwezi kufanya chochote.
Alisema yeye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani hivyo anafahamu mambo mengi.
"Tulipopata misukosuko tulikuwa tunatafuta mbinu za kuzima moto kwa lengo la kuwapoza wananchi, ili jambo lisogezwe mbele," alidai Bw. Mrema.
Alisema mbinu hiyo ndiyo anayotumia Rais Kikwete kumteua Bw.Zitto katika katika Kamati hiyo. Alitolea mfano Tume nyingi zilizoundwa baada ya Serikali kupata misukosuso lakini baada ya mambo kupoa, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alitaja baadhi ya tume hizo kuwa ni pamoja na ya Jaji Nyalali,ya Jaji Warioba na ya Jaji Kisanga. Alisema mbali na tume hizo, zipo tano zilizoundwa kwa ajili ya kushughulia mambo ya madini, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Alisema kamati hiyo haiwezi kubadili chochote kwenye mikataba ya madini kwani mingi iliyosainiwa ni ya muda mrefu. "Mikataba ambayo Serikali imesaini ni ya miaka mingi hatuwezi kuibadili kwa sasa, labda Yesu arudi," alisema Bw. Mrema.
Alisema endapo Rais Kikwete atachukua hatua ya kuvunja mikataba iliyosainiwa, wahusika wanaweza kushitaki kwenye Mahakama ya Kimataifa na kuifanya Tanzania ikumbwe na yale yanayotokea Zimbabwe.
Bw. Mrema alisema kama Rais Kikwete anataka kutunga sheria ya mikataba ya madini hilo ni jambo rahisi. "Ni kiasi cha kuweka sheria kuwa mwekezaji akija atapata asilimia 49 na sisi (Watanzania) tutapata 51 ya mapato hakuna haja ya kuunda kamati," alisema Bw. Mrema na kuongeza kuwa kuunda kamati za aina hiyo, ni sawa na kuwachezea Watanzania.