TAARIFA KWA UMMA
Maoni yangu Binafsi kuhusu Kamati ya Madini iliyoteuliwa na Rais Kikwete
Napinga Muundo, Mfumo na Mamlaka ya Kamati; nahoji dhamira ya Rais Kikwete
Sijawahi kupinga, sipingi na sitapinga Zitto Kabwe kuteuliwa kwenye Kamati
Zitto aingie kwenye Kamati kuendelea kuhoji na kutuwakilisha
Kupinga Kamati si maslahi binafsi, ni maslahi ya Taifa- kupinga kwa nia ya kitaifa ni uzalendo.
Gazeti la Mtanzania na Rai nipeni haki ya kunisikiliza; chukueni maoni yangu toka kwangu mwenyewe kuondoa kupotosha na kunichafulia jina.
Toka Rais Kikwete aunde Kamati ya Madini Novemba 13 na kumteua Zitto Kabwe kama mmoja wa wajumbe, sijawahi kujitokeza hadharani kutoa maoni yangu kuhusu suala hilo hata nilipotakiwa kufanya hivyo na vyombo kadhaa vya habari. Nilikwepa kutoa maoni yangu kutokana na sababu mbili: Mosi, tayari nilishatoa maoni yangu kuhusu kamati hii ya Rais toka Novemba 4 mara baada ya Kauli ya Rais katika mkutano mkuu wa CCM. Pili; Mara baada ya Novemba 14 Viongozi mbalimbali wa CHADEMA walikuwa wametoa maoni yao kuhusu suala hili na kwa kiasi wengine maoni yalitofautiana na baadhi ya vyombo vya habari vikatafsiri kuwa ni mgogoro- hivyo sikutaka kuongeza jina langu katika orodha ya watoa maoni kuepusha kuendeleza hisia za kwamba tunamgogoro-nilinyamaza kimya na kuyawasilisha maoni yangu katika vikao vya chama chetu. Hata Novemba 17 ambapo Kurugenzi ya Vijana tuliandaa Kongamano la Wasomi ambapo suala la Kamati hii pia lilijadiliwa, sikutoa maoni yangu yoyote kuhusu hii kamati kwa sababu ambazo nimezieleza.
Hata hivyo, nalazimika kwa shingo upande kuyatoa maoni yangu kwa umma. Sababu mbili zimenisukuma nitoe kauli yangu leo. Mosi, habari za gazeti la Mtanzania ambalo katika matoleo kadhaa ya wiki hii limekuwa likinitaja na mara moja ukurasa wa mbele kwamba napinga Zitto Kabwe kuwepo kwenye Kamati(gazeti limewasilisha kwa niaba yangu kitu ambacho sijakisema) na Gazeti la Rai toleo la Jana(22/11/2007) ambalo si tu limerudia maoni ya gazeti lake dada kwa niaba yangu- bali pia limenihukumu natunguliza mbele maslahi yangu binafsi badala ya maslahi ya Taifa. Katika hali hii ya kutolewa maoni kwa wiki nzima, nikinyamaza wasomaji na watanzania wenzangu wanaweza kudhani kwamba hayo ndiyo maoni yangu. Nimeamua nitoe taarifa hii kutoa wazi maoni yangu. Pili; kikao cha Kamati kuu ya CHADEMA kinakaa kesho Jumamosi 24/11/2007- kwa vyovyote vile, katika kikao hicho chama kitatoka na msimamo mmoja wa chama baada ya kupokea maoni mbalimbali, hivyo baada ya kikao hicho mimi kama kiongozi zitaweza tena kuwa na fursa ya kuwasilisha maoni yangu binafsi kuhusu suala hili. Nitawasilisha msimamo wa chama kama sehemu ya uwajibikaji wa pamoja hivyo sitapata wasaa tena wa kukanusha na kutoa maoni yangu binafsi tofauti na yale yaliyoandikwa na magazeti ya Mtanzania na Rai. Napaswa kusema sasa, ama ninyamaze milele.
Novemba 4, 2007 nilitoa msimamo wangu pale tu Rais alipotangaza kuunda kamati hii- kwa ujumla katika msimamo huo nilihoji dhamira ya Rais kuunda kamati mpya wakati ya Masha aliyoiunda pindi alipoingia madarakani na ikatangazwa kuwa imempatia ripoti yake Septemba 2006 hatujaelezwa ilibaini nini na imeshindwa kubaini nini ili iwe sababu ya kuundwa kwa kamati nyingine. Pia nilisema wazi kwamba wapinzani hawapaswi kunyamaza kwa kuwa tu watahusishwa kwenye kamati, wapinzani wanapaswa kuendelea kutetea maslahi ya taifa popote walipo na umma wa watanzania unapaswa kuendelea na mjadala kuhusu madini na rasilimali zingine za taifa. Na kwa ujumla nilieleza kwamba katika mazingira hayo suala sio kuundwa kwa kamati, suala ni kutekeleza matokeo ya kamati, na suala hili linahitaji kitu kimoja tu- Dhamira ya kisiasa ya kuchukua hatua. Huu ni msimamo wangu ambao sikuhitaji tena kuutolea maoni baada ya Rais kuunda kamati mpya Novemba 13, 2007.
Mara baada ya Rais kuunda Kamati ya Madini na kumteua Zitto Kabwe Novemba 13, (narudia tena)- sijawahi kutoa msimamo wangu kwa chombo chochote cha habari.Kwa waraka huu; nawasilisha rasmi maoni yangu kwa umma kuhusu Rais kuunda Kamati ya madini:
Napinga Muundo, Mfumo na Mamlaka ya Kamati na nahoji dhamira ya Rais Kikwete katika kuunda kamati yenye muundo, mfumo na mamlaka kama kamati hii chini ya Mwenyekiti Jaji Msaafu Mark Bomani. Baadhi ya masuala ya kujiuliza yaliyopelekea niwe na maoni haya nimeyadokeza kwenye ujumbe wangu niliowapatia baadhi ya wahariri Novemba 19 mwaka 2007. Sijawahi kupinga, sipingi na sitapinga Zitto Kabwe kuteuliwa kwenye Kamati. Zitto aingie kwenye Kamati kuendelea kuhoji na kutuwakilisha. Kupinga Kamati si maslahi binafsi, ni maslahi ya Taifa- kupinga kwa nia ya kitaifa ni uzalendo. Gazeti la Mtanzania na Rai nipeni haki ya kunisikiliza; chukueni maoni yangu toka kwangu kuondoa kupotosha na kunichafulia jina.
Kwa maoni yangu: Muundo wa Kamati unazua mjadala- Rais aliahidi kwenye mkutano Mkuu wa CCM kwamba angeunda kamati itakayoshirikisha jamii kwa upana zaidi ikiwemo asasi za kiraia-lakini kamati iliyoundwa imejaa watendaji wa serikali na makada wa chama tawala huku asasi za kiraia zikiwa hazina mwakilishi hata mmoja tofauti na ahadi ya Rais. Katika hotuba yake Rais alizungumzia uwakilishi-lakini katika uteuzi wake Rais amefanya uteuzi wa watu binafsi ingawa wanatoka katika taasisi mbalimbali ikiwemo vyama vya upinzani. Katika Lakini hili ni suala dogo. Kubwa zaidi katika muundo wenyewe ni Rais kuwahusisha baadhi ya wajumbe wenye tuhuma za ufisadi ambazo Rais alikuwa anazifahamu kabisa toka wakati akiwa Waziri katika serikali na wengine wanamgongano wa kimaslahi ambao uko bayana. Kama aliwahujua watu hawa, nini dhamira ya kuwateua? Je, hakuna watanzania wengine ikiwemo toka katika chama chao ambao uadilifu wao hautiliwi mashaka ya kiasi hicho?
Mfumo wa Kamati unazua mjadala-Hadidu rejea za kamati zimetogezwa lakini katika hadidu rejea zilizotajwa masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya migodi na ya uchafuzi wa mazingira hayajaguswa. Nini cha pekee ambacho kamati hii itafanya ambacho Kamati ya Masha iliyokamilisha kazi yake mwaka jana haijafanya? Imani yangu ni kuwa suala hili litatazwa vyema- ripoti ya Kamati ya Masha itawekwa wazi kwa umma, Kamati ya Bomani itafanya kazi yake kwa uwazi na kuwa na vikao vya masikilizano na umma(public hearings) na ripoti yote itawekwa wazi kwa umma.
Mamlaka ya Kamati yanaibua mjadala- Uamuzi wa Rais Kikwete kuunda Kamati badala ya Tume unanifanya nihoji dhamira yake. Rais Kikwete anafahamu kabisa kuwa Kamati haina mamlaka ya kutosha ya kuita mashahidi na kuwataka kutoa ushahidi wa kiapo kama ambavyo Tume ya Rais inavyo. Uamuzi wa kuunda Kamati unafanya dhamira ihojiwe, je masuala ya madini ikiwemo sheria na mikataba hayana masuala nyeti yanayohitaji mamlaka ya Tume kuweza kuyafuatilia? Kwa vyovyote vile- kamati ya Jaji Bomani pamoja na kuundwa na Rais kwa mujibu wa sheria za nchi yetu haiwezi kuwa na mamlaka makubwa(executive authority). Kama Rais Kikwete aliweza kuunda tume kadhaa haraka katika kipindi kifupi cha utawala wake, ni vipi suala hili ameacha kuliundia tume na badala yake ameunda kamati? Suala la Mamlaka ni nyeti kwa kuwa ikumbukwe kuwa suala alilolitaka Zitto Kabwe bungeni ni kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ambayo ni wazi ingekuwa na mamlaka yanayoshabihiana na yale ya Tume ya Rais.
Ukitafakari masuala hayo kiundani utaoana suala la kujadiliwa si kuwepo au kutokuwepo kwa Zitto Kabwe kwenye kamati- Hoja ni Kamati yenyewe na dhamira ya Rais Kikwete katika kuiunda Kamati hiyo. Katika muktadha huo basi; maoni yangu ni kuwa kama serikali haitarekebisha kasoro hizo zilizopo kuhusiana na hiyo kamati, Zitto Kabwe kama mmoja wa wajumbe bado anapaswa kuendelea kushiriki ili kuwasilisha na kuwakilisha fikra mbadala katika kamati hiyo. Zitto akawe hamira ya kuumusha na kuchachusha hoja na mchakato wa kamati ya Bomani. Na kuendelea kumjadili Zitto Kabwe badala ya kuendelea kujadili masuala hayo ni kukwepesha mjadala wa msingi.
Kwa maoni yangu, CHADEMA kama chama cha demokrasia na maendeleo kimefanya uamuzi wa busara mpaka sasa kuruhusu mjadala huu. Maoni tofauti baina ya baadhi ya wanaCHADEMA yamewasaidi kuimulika kamati na kufahamu undani wake- utamaduni huu wa kuhoji na kutoa fikra mbadala ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu na unapaswa kuendeleza. Imenisikitisha kwamba Gazeti la Mtanzania na Rai wamemua wazi kusambaza ujumbe kwamba kwa kuwa na maoni hayo mimi(na wamenitaja kwa jina) kwamba natanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya Taifa. Na wamehusisha maoni yangu na kuchunguzana nani atagombea urais 2010 kupitia CHADEMA mintaarafu umaarufu wa Mbowe na Zitto. Kwa maoni yangu, huu ni mkakati mwingine wa wakagawe uwatawale (divide and rule); haya mambo ya Urais yanatoka wapi tena wakati Zitto hata miaka 40 ya kugombea Urais atakuwa hajafikisha wakati huo? Bahati njema, naamini viongozi wa CHADEMA hawawezi kuchonganishwa na habari za magazetini.
Kwa maoni yangu mimi, hoja zote zinatetea maslahi ya taifa na ni za kizalendo. Wanaotaka kamati iwe na muundo, mfumo mzuri na mamlaka zaidi wanatetea maslahi ya taifa na ni wazelendo kama ambavyo wenye mtizamo tofauti nao ni wazalendo. Ni kupitia fikra hizi mbadala ndipo tunapata kilichobora zaidi na kukiendea kama taifa. Hivyo, kama ambavyo itikadi ya CHADEMA inaamini katika siasa zilizojuu ya vyama zinazosimamia ziadi maslahi ya taifa. Hivyo hivyo, wanaopinga muundo, mfumo na mamlaka ya kamati, hawafanyi hivyo kwa manufaa ya kisiasa ya CHADEMA, wanataka CHADEMA itumike kama chombo tu cha kutumika kusimamia fikra hizi mbadala na matokeo yoyote mazuri ya fikra hizi yatasimamia rasilimali za taifa na matokeo yale yatanufaisha watanzania wote bila kujali itikadi. Wazalendo hawakai kimya wanapoona jambo lolote katika taifa lao linakwenda tofauti na hoja zao ama za makundi ya kijamii ambayo wanayawakilisha. Maoni ya pande zote ni mazuri kufanya watchdog function kwa kamati; kwa mfano mijadala kama hii inaweza kupelekea kamati kuacha kufanya kazi kwa kificho; kamati kufanya kazi kwa undani zaidi na pengine hata kufanya matokeo ya Kamati hii kutekelezwa kwa sababu ya ufuatuliaji wa karibu wa wa vyombo vya habari na umma. Mambo haya ni muhimu yakajadiliwa wakati kamati inaendelea kufanya kazi kwa sababu kazi ya kamati miezi mitatu inagharamiwa na walipa kodi watanzania; fedha hizi zingeweza kutumika kujenga madarasa- hivyo kama kamati haitafanya kazi kwa kadiri ya matakwa ya umma matokeo yake ni hasara kwa taifa kwa ujumla bila kujali itikadi. Ifahamike mjadala kuhusu ufisadi na hatma ya rasilimali za Tanzania ni suala pana kuliko Kamati ya Bomani. Nikumbushe kauli niliyoitoa mwaka 2005 wakati wa uchaguzi- Tanzania ni yetu sote; SIASA SIO UADUI.
Naamini Kamati kuu ya kesho baada ya kupokea maoni mbalimbali italipokea na kulitolea msimamo wa chama suala hili na PAMOJA TUTAFIKA.
Nautoa waraka huu leo Ijumaa 23 Novemba mwaka 2007:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa(CHADEMA)
0754694553
mnyika@yahoo.com
PS: Natarajia Gazeti la Mtanzania la 24/11/2007 na Gazeti la Rai la Wiki ijayo mtachapa maoni yangu kama sehemu ya maadili ya vyombo vya habari ya kutoa fursa kwa mhusika kutoa maoni yake kabla ya kuandika habari inayomhusu. Naamini mtachapa ufafanuzi wangu kuhusu suala hili.
Kwa maelezo zaidi na rejea(tazama viambatanisho):
Sehemu ndogo ya maoni yangu ya 4 Novemba 2007 Kama yalivyonukuliwa Na Tanzania Daima 5 Novemba, 2007(maoni baada ya Mkutano Mkuu wa CCM)
Ujumbe kwa baadhi ya Wahariri nilioutoa 19 Novemba, 2007