Balantanda
JF-Expert Member
- Jul 13, 2008
- 12,480
- 4,775
- YAONYESHA MBOWE, NDESAMBURO WANAKIDAI CHAMA SH53 MILIONI
Fidelis Butahe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) kimesema kwamba kama kuna mtu mwenye ushahidi kuwa kuna baadhi ya viongozi wa chama hicho ni mafisadi atoe ushahidi.
Vilevile, kimetoa taarifa kwamba mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo wanakidai chama hicho jumla ya Sh53milioni walizokikopesha.
Hata hivyo, Chadema imechukua hatua hiyo inayokifanya kuwa chama cha kwanza kuweka wazi mapato yake ya fedha na matumizi yake, baada ya wanachama kuutuhumu uongozi kuwa unafuja fedha za chama.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alilieleza gazeti hili jana kuwa kati ya fedha hizo, Mbowe anadai Sh 42milioni na Ndesamburo Sh 11milioni.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Dk Slaa alisema: "Deni la Ndesamburo ni Sh11m, wakati Mbowe anadai Sh 42milioni ambazo zinaweza kuongezeka muda wowote kwa sababu chama kinajiendesha kwa michango.
"Nasema hivi, tutaendelea kukopa na kulipa bila kukoma kwa sababu hata Marekani wanatumia utaratibu kama huu.
"Mbowe ataendelea kuwa mtia saini wa chama, hilo halina mjadala. Wasioelewa hapa inatakiwa waelewe kuwa fedha zote za chama lazima zipite kwanza kwa mdhamini, sasa kunapoibuka maneno kuwa fedha za Chadema zinatafunwa na mwenyekiti, hakuna ukweli wowote."
Dk Slaa alikuwa akielezea maamuzi ya kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichofanyika Desemba 2 hadi 3 kwenye hoteli ya Keys iliyo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili taarifa zilizohoji uteuzi wa Mbowe kuwa mtiaji saini wa chama kwa mujibu wa taratibu za fedha.
"Baada ya kujadili kiliamua kwamba, Mbowe kwa wadhifa wake aendelee kuwa mtiasaini kama sehemu ya usimamizi wa kifedha uliopo kwenye taratibu za fedha za chama zilizopitishwa na vikao vya juu vya chama," alisema.
Dk Slaa alisema Chadema hakuna ufisadi na kwamba haiogopi kukaguliwa, iko tayari kukaguliwa kwani ukaguzi ni kazi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG.
"Fedha za Chadema, CUF na UDP ukizijumlisha huwezi kufikia hata nusu ya fedha zinazotafunwa CCM.
Chadema hatuwezi kuogopa kukaguliwa na CAG na hatuwezi kumwita atukague... kwani hajui kazi yake? Sisi hatuna wasiwasi na hilo tunajiamini, labda anaogopa kuwa akifanya hivyo anaweza kuiumbua CCM," alisema Dk Slaa.
"Wanaosema Chadema ni mafisadi warejee sheria namba 375 hapo ndipo watakapojua kuwa kelele zao ni 'makelele ya debe tupu', lakini pia wanaosema hayo waje hapa wakiwa na vielelezo vinavyoonyesha jinsi hizo fedha zinavyotafunwa sio kusemea pembeni"
Maamuzi hayo ya CC ya Chadema yamekuja huku aliyekuwa ofisa habari wa chama hicho, David Kafulila na ofisa wa masuala ya Bunge Danda Juju ambao walienguliwa nyadhifa hizo na baadaye wenyewe kujitoa Chadema, wakikitupia tuhuma nzito chama hicho.
Kwa nyakati tofauti Kafulila na Juju walishutumu kitendo cha Mbowe kuwa mtiaji saini wa fedha za chama huku wakimwomba CAG kukagua mapato na matumizi ya chama hicho kujionea ubadhirifu.
Kafulila alieleza hayo juzi katika hafla iliyoandaliwa na NCCR-Mageuzi kuwapokea wanachama wapya. Alisema Chadema kuna ufisadi na kusisitiza kuwa kama viongozi wa chama hicho wakiendelea kujificha, atawaumbua.
Hata hivyo, jana Dk Slaa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kafulila na Juju wanazungumza maneno ya uongo kwa lengo la kujipatia umaarufu wakati hata siku moja hawakuwahi kuzungumza au kulalamika kwa barua kuhusu suala la matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama hicho.
"Hapa naomba mnielewe waandishi kikao hiki cha kamati kuu kilikuwa hakijadili mgogoro ndani ya chama. Baadhi ya ajenda zilizojadiliwa ni tathmini ya uchaguzi wa serikali za mitaa, mikakati ya kutekeleza mipango na mikakati ya chama, kuthibitisha makatibu wa wilaya na mikoa, taarifa za rufaa mbalimbali za uchaguzi wa ndani, taarifa za mfumo wa kiuanachama kwa njia ya elektroniki, taarifa za fedha, uteuzi wa bodi ya wadhamini pamoja na kupanga tarehe ya mkutano wa baraza kuu na mkutano mkuu na mengineyo," alisema Dk Slaa.
"Pamoja na hayo suala la Kafulila na Juju lilizungumzwa pia kwenye mkutano huu lakini halikuwa ajenda kuu. Hapa mnielewe lilijadiliwa lakini halikuwa ajenda kuu."
Alisema kuwa Chadema haiwezi kupangiwa na mtu jinsi ya kujiendesha na kusisitiza kuwa anayejua machafu ya Chadema ajitokeze wazi na kusema bayana kama mbunge huyo wa Karatu anavyofanya bungeni.
"Mimi kumwita Kafulila na Juju 'sisimizi' kuna tatizo gani? Hiyo ni kama 'analogy' tu ni misemo ya kisiasa mbona rais wa awamu ya pili aliwahi kusema kuwa yeye ni kichuguu akijifananisha na Nyerere, hilo sio tatizo," alisema.
"Akina Kafulila walitakiwa kutambua kuwa kila chama kina msemaji wake, sasa wao kikao cha chama wanasema kana kwamba chama kimekaa 'geto', hapo kwa nini wasichukuliwe hatua?
"Maamuzi niliyoyafanya kwa Kafulila na Juju yamepongezwa na CC, wanachotakiwa kujua ni kwamba hata mimi leo nikiondoka Chadema itaendelea kuwepo, kuondoka ndani ya chama ina maana kuwa umeshindwa kuendana au kuhimili ajenda za chama"
Akizungumzia ajenda ya hali ya siasa nchini ambayo ilijadiliwa katika kikao hicho, Dk Slaa alisema taifa limegubikwa na migogoro na malumbano yanayosababishwa na uongozi mbovu na udhaifu wa kisera wa serikali na taasisi zake.
"CCM nayo imegubikwa na malumbano ya hali ya juu yanayoashiria kufilisika kwa hali ya juu kimaadili kama tulivyoeleza kwenye orodha ya mafisadi Septemba 15. 2007," alisema Dk Slaa.
Alisema Kamati Kuu imebaini pia kuwa uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa ulikuwa wa kihuni na kulitia aibu taifa kwa kuwa uliendeshwa kinyume na kanuni na misingi ya demokrasia na haki za binadamu.
"Kuhusu rufaa mbalimbali katika chaguzi za ndani, kamati kuu ilijadili taarifa na kuielekeza sekretarieti ifuate maelezo na vielelezo vya ziada ili maamuzi yaweze kufanywa katika kikao kijacho," alisema Dk Slaa.
Kuhusu mikakati ya chama kuelekea uchaguzi mkuu 2010, Dk Slaa alilaani kitendo cha serikali kwa kushirikiana na utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kukataa kuongeza mkataba wa aliyekuwa mhadhiri wake, Prof Mwesiga Baregu ambaye ni mjumbe wa CC wa chama hicho.
Alilalamika kuwa hiyo imekuwa tabia ya serikali kwa sababu iliwahi kumfanyia hivyo Dk Masumbuko Lamwai wakati akiwa NCCR-Mageuzi. Kwa sasa Dk Lamwai ni mhadhiri wa sheria Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam na kada wa CCM.
Source: Gazeti la Mwananchi