Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinarejea msimamo wake wa awali wa tarehe 19 Novemba 2025 kutotambua mchakato mzima wa Tume iliyoundwa na Samia Suluhu Hassan, na kinapinga kwa ujumla wake ripoti iliyowasilishwa leo tarehe 23 April 2026 na Tume hiyo chini ya Jaji Mohamed Chande Othman.
CHADEMA inasisitiza kuwa, kwa mujibu wa kauli ya wazi ya Samia Suluhu Hassan mwenyewe, ripoti hiyo ni yake binafsi. Hivyo, haiwezi kuchukuliwa kama nyaraka huru yenye kuakisi ukweli au haki kwa waathirika wa matukio yaliyoripotiwa.
Chadema inasitiza kuwa ripoti hii na mchakato wake wote ni batili kwa sababu zifuatazo;
Jambo la kwanza na la msingi zaidi, msimamo wetu unatokana na ukweli kwamba mteuzi wa tume hiyo Ndugu Samia Suluhu Hassan hana uhalali wa kisiasa, kisheria na kimaadili. Alijipachika Urais kupitia mchakato usio huru, usio wa haki, usio wazi na usiokidhi viwango vya kidemokrasia kama ambavyo walivyosema Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Afrika (UA) na wale wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ndugu Samia hana mamlaka ya kimaadili wala kisiasa kuunda chombo cha kuchunguza uhalifu mkubwa uliofanywa na utawala wake dhidi ya raia.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi (Commissions of Inquiry Act, 2002: Chapter 32), tume ya aina hii ni chombo cha Rais, kinachofanya kazi kwa matakwa na maelekezo yake. Kwa mantiki hiyo, si chombo huru, na hakiwezi kutoa ukweli wala haki katika mazingira ambapo serikali ndiyo mtuhumiwa mkuu.
Zaidi ya hapo, haiwezekani mtuhumiwa akajichunguza mwenyewe halafu tutarajie haki. Serikali ya Samia ndiyo iliyopanga, kuratibu na kutekeleza mauaji, utekaji, mateso, ubakaji, unyanyasaji na ukiukwaji mpana wa haki za binadamu.
Wote walioteuliwa ndani ya tume hiyo waliwahi kuwa au ni watumishi wa Serikali na pia ni Wanachama wa chama anachokiongoza Ndugu Samia (CCM) jambo ambalo kimsingi linakiuka kanuni ya msingi kwamba tume huru haipaswi kuwa na uhusiano wowote na Serikali wala chama tawala.
Hawa wajumbe wakati wote wamekuwa sehemu muhimu ya kuiingiza nchi yetu kwenye maafa haya, na baadhi yao ni watuhumiwa wa kupanga na kutekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wakiwa madarakani.
Hii si tume huru; ni njama ya kuficha ukweli, kufuta ushahidi na kuendelea kuwaumiza waathirika.
Chama kinaendelea kusisitiza hitaji la kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa na kitaifa utakaokuwa na uaminifu, uwazi na uwezo wa kubaini ukweli bila upendeleo.
Aidha, CHADEMA kinaendelea kufanya uchambuzi wa muhutasari wa ripoti uliosomwa na Jaji Mohamed Chande Othman pamoja na hotuba iliyotolewa baada ya kupokelewa kwa ripoti hiyo. Kauli kamili ya Chama itatolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika tarehe 28 na 29 Aprili 2026.
Imetolewa leo Alhamisi tarehe 23 Aprili 2026
Brenda Rupia
Mkurugenzi wa mawasiliano na uenezi
View attachment 3577994
View attachment 3577993