By Albanie Marcossy:
Katiba inachezewa?
Samia Suluhu Hassan ni RAIS; sio Kaimu!
Baada ya Kusoma tamko la Chama cha Wanasheria Tanganyika, TLS, na lile la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, na kupitia mijadala kadhaa katika mitandao yetu ya kijamii, nimelazimika mshangao wangu niupeleke mwenyewe kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Habari hii inahusu uwepo wa Baraza la Mawaziri chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Rais Samia tangu alipoapishwa hata sasa namuona anawatumia watu wale wale waliokuwa Mawaziri, manaibu Waziri na Mwanasheria mkuu wa Serikali iliyopita kana kwamba ndio utaratibu.
Niliposoma katika Ibara ya 38(2)(f) nikapata ufafanuzi wa kukoma kwa urais wa john Pombe magufuli, pale alipofariki na kumbe nafasi yake itajazwa kwa utaratibu uliowekwa na Katiba. Kabla ya Ibara hii, ile Ib. 37(5) inatamka wazi kuwa endapo Rais atafariki, Makamu wa Rais, ataapishwa kuwa RAIS…. Na kuwa ataongoza kwa kipindi chote kilichosalia ndani ya miaka mitano. Kumbesa, Ib.42(1) ikamtambua Makamu wa Rais kuwa ndiye rais Mteule na kuwa atashika mamlaka ya Rais ndani ya siku 7. Katiba hii hii inasema katika Ib. 42(5) kuwa rais Mteule ataapa (kwamba aliyekuwa makamu wa Rais lazima aapishwe kuwa Rais). Kwamba pamoja na kiapo chake sambamba na Rais aliyetangulia, ni lazima aapishwe kwanza kushika madaraka ya Rais. Vivi hivyo, Waziri Mkuu, Mawaziri na manaibu wao, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyeteuliwa kushika nafasi na Rais aliyepita, atapaswa kuapishwa upya (endapo atateuliwa) kuendelea kushika nafasi hiyo na rais aliyeingia madarakani.
Pamoja na kumpa Makamu wa Rais nafasi ya kuwa Rais lakini katiba hii inatamka kwenye Ib. 47(2) kuwa MR lazima awe alichaguliwa na kwamba atakoma kuwa Makamu wa Rais siku atapoapishwa kuwa Rais. Na kuwa Mawaziri na manaibu Waziri wote watakoma kuwa katika nafasi hizo “…mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika nafasi yake” (URais) kulingana na Ib.58(5)b.
Hivyo ni wazi kabisa kuwa Katiba yetu haina utata kwenye urithisho wa madaraka kati ya Rais na makamu wake endapo Rais atafariki. Na hakuna utata wa nafasi za Waziri Mkuu, Mawaziri, manaibu waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali: kwamba nafasi zao zitakoma mara kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka ya URais. Pia ni jambo lililo wazi kabisa: hakuna kiapo cha urithi. Kuanzia Makamu wa Rais anayekwenda kuwa Rais, Waziri Mkuu na hata Mwanasheria Mkuu na Manaibu Waziri; hata rais aliyechaguliwa mara ya pili hawezi kuendelea na kazi bila kuapishwa upya; inakuwaje Mawaziri hawa waendelee kubaki mamlakani bila kuapa mbele ya Rais mpya? Je, kwa kiapo hicho, watamtii Rais aliyepo au marehemu? Mtu pekee anayebaki kwenye Baraza la Mawaziri ni Rais wa SM/Zanzibar. Naye pia atapaswa kula kiapo kwa Rais mpya.
Hivyo basi:
1. Ni wazi kuwa kwa sasa nchi yetu haina Waziri Mkuu, Mawaziri na manaibu Waziri; na pia hakuna Mwanasheria Mkuu wa serikali. Baraza la Mawaziri lilivunjika (hakuna haja ya kulivunja) siku kabla ya Mhe. Samia Suluhu Hassan hajaapishwa kuwa Rais. Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitenguka;
2. Lile ulilohudhuria siku ile mara tu baada ya kuapishwa lilikuwa ‘Kongamano la Waliokuwa Mawaziri’ kwenye seruikali ya awamu ya tano;
3. Matendo yoyote wayatendao ‘Waliokuwa Mawaziri na Manaibu wao na Mwanasheria Mkuu’ yachukuliwe kama nia njema ya kisiasa (good political intentions to serve. Kwa namna yeyote wakijiingiza kwenye maamuzi ya kisheria tutaiingiza knchi kwenye mtanzio wa kikatiba punde;
4. Siamini endapo watu hawa wote hawajui walifanyalo. Huenda kuna msukumo nyuma ya pazia; huenda ni kwa kutokujua au upepo wa kisiasa na mkanganyiko wa msiba. Endapo ndivyo, tafadhali Mh. Rais ashauriwe haraka kuchukua hatua za kuliondoa baraza hilo kimya kimya;Kuendelea kuwepo madarakani watu wanaojua hawakuteuliwa wala kuapishwa na Rais, kwa madai yeyote, ni kusema aliyepo madarakani anakaimu nafasi ya Rais. Mama Samia Suluhu Hassan alichaguliwa na Wananchi kushika nafasi ambayo Rais akifariki yeye ndiye ataapishwa kuwa Rais; ameapishwa kwa mujibu wa Katiba kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anapaswa kuteua na kuwaapisha Mawaziri wake kama Katiba inavyotaka.
Wananchi tunakuhimiza Rais wetu, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Nchi na Serikali, simamia Katiba yetu.