KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977
(Toleo hili la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977,
limezingatia na kuweka pamoja mabadiliko yote yaliyofanywa katika Katiba
ya Muungano tangu ilipotungwa mwaka 1977 hadi tarehe 30 Aprili, 2000.
SEHEMU YA PILI.
WABUNGE, WILAYA YA UCHAGUZI NA UCHAGUZI WA WABUNGE
77.-(1) Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi watachaguliwa na wananchi kwa kufuata masharti ya Katiba hii na vile vile masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu Katiba hii inayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi.
(2) Isipokuwa pale ambapo Tume ya Uchaguzi, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, itaagiza vinginevyo, kutachaguliwa Mbunge mmoja tu katika jimbo la uchaguzi.
(3) Wagombea uchaguzi katika jimbo la uchaguzi watatakiwa watimize masharti yafuatayo-
(a) wawe wamependekezwa mmoja mmoja, na chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi katika jimbo hilo;
(b) wamewasilisha majina yao kwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au uliofafanuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.