Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,513
Na Mwandishi WETU
HUMPHREY POLEPOLE anafahamika kwa harakati zake kupambana na watu anaowaita wahuni; akimaanisha watu wasiofuata taratibu katika uongozi.
Amewahi kuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Uenezi, Itikadi na Mafunzo.
Huyo ndiye Polepole, ambaye hadi jana mchana – Jumapili ya Julai 13, alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba.
Lakini, inaonekana wahuni – ambao amekuwa akitangaza kuwepo ndani ya CCM—wamemzidi nguvu kwani jana alimwandikia barua rasmi Rais Samia Suluhu Hassan, akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo.
Polepole ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya uwakilishi wa kidiplomasia pamoja na kuachana rasmi na majukumu yake yote ya uongozi wa umma.
Katika barua hiyo, ambayo nakala yake imesamba mitandaoni ikiwemo katika ukurasa wake wa Instagram, Polepole mwenyewe, anasema amefikia uamuzi huo baada ya “tafakari ya kina” kuhusu mwelekeo wa sasa wa uongozi wa taifa.
Katika barua hiyo ya kurasa mbili ambayo imenakiliwa pia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Polepole amesema anashindwa kuendelea kuwa sehemu ya uongozi ambao kwa maoni yake, hauzingatii tena “misingi ya haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi.”
“Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi wa umma... nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki kama Colombia, Venezuela na Guyana,” ameandika Polepole.
Aeleza sababu za kujiuzulu
Polepole, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (2020–2022), amesema amefuatilia kwa karibu mwenendo wa serikali ya sasa na kugundua kuhusu “mwelekeo wa uongozi usioelekezwa ipasavyo katika kusimamia haki za watu na heshima ya utu.”
Barua yake ikaendelea kueleza; “Kushindwa kwa uongozi katika ngazi mbalimbali kutekeleza majukumu kwa misingi ya serikali kwa ajili ya watu, kumeharibu imani yangu niliyojenga kwa miaka mingi,” amesema.
Ameongeza kuwa matukio ya kisiasa ya hivi karibuni ndani ya CCM na serikali, yameonesha “ukiukwaji wa misingi na utamaduni wa demokrasia ya ndani ya chama, hasa katika uteuzi wa wagombea.”
Aikosoa CCM
Akitolea mfano kauli maarufu ya CCM inayosema “Chama kwanza, mtu baadaye,” Polepole amesema amejiuliza kwa kina kuhusu utekelezaji wa kauli hiyo, akihoji maslahi ya nani yanapewa kipaumbele kati ya chama, mtu binafsi au taifa.
“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utiifu wa misingi ya katiba ya nchi, chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini,” amesema.
Bado anataka mabadiliko
Katika hitimisho la barua yake, Polepole amesema atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM na mzalendo kwa taifa, huku akionyesha matumaini kwamba siku moja taifa litaongozwa kwa misingi ya haki na maadili bila uoga.
“Ninaamini siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa rasilimali na nidhamu ya uongozi... bila hofu ya Mungu,” ameeleza.
Adai CCM kuna wahuni
Polepole amekuwa akidai kuwa ndani ya chama chake cha CCM kuna wahuni kadhaa ambao amedai “wanakiharibu chama hicho.”
Bila kutaja majina ya wanachama wenzake anaodai kuwa ni wahuni, Polepole amedai kuwepo kwa njama za “kumuumiza” kutoka kwa hao anaowatuhumu, lakini anasisitiza kuwa “hawamuwezi kwa kuwa analindwa na Mungu.”
Amekuwa akidai kuwa hao wahuni ipo siku wataondoka na kukiacha chama chake kikiwatumikia zaidi wananchi, kinyume na hali ilivyo sasa.
Wasifu wa Polepole
Umaarufu wa Humphrey Polepole ulianza kabla ya mchakato wa kuandika Katiba mpya chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete – kiongozi wa awamu ya nne.
Wakati huo Polepole alijipambanua kuwa mwanaharakati.
Alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakipaza sauti kwa hoja za kudai katiba mpya.
Baadaye sifa zake zikazidi na kujipatia umaarufu akiwa Katibu wa Uenezi, Itikadi na Mafunzo wa CCM kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge na kisha kuteuliwa kuwa balozi mwaka 2022.
Amewahi kushiriki kikamilifu katika utengenezaji wa sera za vijana, katiba mpya, na kampeni za chama hicho tawala.
Tangu 2023 alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, akihudumu pia kwa nchi nyingine za Amerika ya Kati.
Hatua yake yashtua
Kujiuzulu kwa Polepole kumewashitua watu kadhaa wakileza kushangazwa kwao na tukio hilo lisilo la kawaida.
Wachambuzi wa siasa wanasema kujiuzulu kwa Polepole ni tukio la nadra linaloweza kuibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa siasa za ndani ya CCM na nafasi ya maadili katika uongozi wa umma.
“Kwa mtu aliyewahi kuwa msemaji mkuu wa chama na mbunge, hatua hii siyo ya kawaida, Inaashiria maumivu ya ndani kwa watu waliomo kwenye mfumo, lakini wamepoteza imani,” amesema mchambuzi wa masuala ya siasa aishiye Kinondoni, Dar es Salaam, Issa Majebele.
Amesema kikubwa zaidi kilichoshitua ni ujumbe ulio katika barua ya kujiuzulu ambayo Polepole ameipeleka kwa Rais Samia na kuisambaza hata kabla ya kujibiwa.
Wanasema ujumbe huo unaonyesha dhahiri kuisema serikali iliyopo madarakani.
Serikali bado kimya
Hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, siyo serikali wala uongozi wa CCM uliotoa taarifa yoyote rasmi kuhusu barua hiyo ya kujiuzulu ya Polepole.
Nyongeza: Mazingira ya kujiuzulu kwa Polepole
Kiini cha umauzi wake kinapatikana kwenye barua yake pale Polepole anaposema maneno yafuatayo:
"Kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia Haki za watu, Amani na kuheshimu watu, kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali."
Kisha Polepole anakata shauri kwa kusema kuwa "siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi."
Baada ya maneno hayo Polepole anataja ndoto yake.
"Ninaamini siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa rasilimali na nidhamu ya uongozi," anaeleza.
Maneno haya yanathibitisha fikra kwamba Polepole amejiuzulu ili kukwepa lawama zinazoelekezwa dhidi ya serikali ya wamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia, kwa sasa.
Serikali ya Samia inashutumiwa kwa ujasiri wa m kukiuka wazi wazi haki turufu (non-derogable rights) za raia zinazotambuliwa na Katiba ya nchi pamoja na mikataba ya KImataifa ambayo imeridhiwa na Tanzania.
Haki turufu ni haki zinazopaswa kuheshimiwa na kila mtu, kila mahali na kila wakati.
Kwa mujibu wa ibara namba 5, 8 na 32 za Katiba ya Tanzania (1977) kama zikisomwa pamoja na ibara ya 4(2) ya Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia (ICCPR), ambao imeridhiwa na Tanzania, haki turufu ni zifuatazo:
KUna haki ya kuishi; haki ya uhuru dhidi ya mateso au ukatili, unyama na kudhalilishwa; na haki ya uhuru dhidi ya majaribio ya matibabu au ya kisayansi bila idhini;
Pia kuna haki ya uhuru dhidi ya utumwa na ukoloni; haki ya uhuru dhidi ya kifungo kwa kukosa uwezo wa kutimiza wajibu wa kimkataba; haki ya uhuru dhidi ya kuhukumiwa chini ya sheria za uhalifu zilizotungwa baada ya tukio; haki ya usawa mbele ya sheria;
Kadhalika, kuna haki ya kuhesabiwa mwenye haki hadi pale hatia itakapothibitishwa na mamlaka husika; haki ya uhuru wa mawazo; haki ya uhuru wa dhamiri; haki ya uhuru wa dini; na haki ya kushiriki katika utawala wa nchi.
Lakini, matukio yafuatayo yanavunja wazi wazi haki turufu tajwa, na serikali imeziba masikio: mauaji ya Ali Mohamed Kibao, kutekwa na kupotezwa kwa Deusdedith Soka na wenzake wapatao 84 kwa mujibu wa taarifa ya chama cha sheria cha Tanganyika.
Pia kuna kuteswa na kujeruhiwa kwa wafuasi wa Chadema wakiwa wanaelekea mahakamani Kisutu kwenye kesi, kutekwa na kupotezwa kwa Mdude Nyagali huko Mbeya, na kubuniwa kwa kesi hewa ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu Mwenyekiti wa Chadema na kjumweka kizuizini.
Kadhalika, kuna ukatili wa polisi dhidi ya raia wasio na silaha, polisi kuziteka ofisi za Makao Makuu ya Chadema huko Mikocheni, na kuwindwa kwa watia nia wa Chadema katika ngazi ya ubunge na udiwani.
Vile vile kuna kutekwa na kupotezwa kwa Shedrack Yusuph Chaula aliyechana picha ya Rais, kuvamiwa kwa makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Kurasini jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumnyamazisha Padre Kitima kwa kumwua, kufutwa kihuni kwa usajili wa Kanisa la Gwajima, na orodha inaendelea.
Mwaka 2021 Rais Samia aliingia madarakani baada ya kula kiapo cha kulinda, kuhifadhi na kutetea Katiba ya nchi, inayotaka haki turufu, ambazo sasa zinavinjwa wazi wazi na serikali anayoiongoza.
Matukio haya ya uvunjaji wahaki za raia yameshamiri zaidi baada ya tamko la Rais Samia kwamba Katiba ya nchi ni kitabu tu kama vitabu vingine.
Kwa sababu hii, wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kisheria na kikatiba wanasema kwamba, tayari Rais Samia amesaliti kiapo chake kiasi kwamba amepoteza sifa ya keundelea kukalia kitu cha Urais.
Barua ya kujiuzulu kwa Polepole iliyoandikwa tarehe 13 Julai 2925 inasomeka kama ifuatavyo:
YAH: TAARIFA YA KUJIUZULU NAFASI YA UBALOZI NA NAFASI YA UONGOZI WANGU WA UMMA
KUTOKA KWA:
Humphrey Hesron Polepole,
S.L.P. 32,
Dar es Salaam.
Whatsapp: +13057764396.
KWENDA KWA:
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ikulu,
Dar es Salaam,
Tanzania.
Mheshimiwa Rais,
Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.
Uamuzi huu si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yetu, uzoefu wangu kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Novemba 2020 – Machi 2022), na hatimaye kama Balozi katika vituo vya Lilongwe – Malawi (Machi 2022 – Aprili 2023) na Havana – Cuba (Aprili 2023 – Julai 2025).
Mheshimiwa Rais, nilipokea kwa heshima kubwa uteuzi na dhamana uliyonipa kuwa mwakilishi wa nchi yetu katika ngazi ya kimataifa.
Niliamini na ninaendelea kuamini lilikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza maslahi mapana ya nchi yetu katika maeneo ya uwakilishi ulinipa dhamana ya kuyasimamia.
Ni heshima kubwa na isiyopimika kuaminiwa kuwa Mwakilishi wako, Nchi yetu, Taifa letu, wananchi na Mamlaka ya nchi. Kwa hili, nasema asante.
Hata hivyo, kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia Haki za watu, Amani na kuheshimu watu, kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali.
Kudhoofika kwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi; mambo haya yanateteresha maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Haya yote yamezidi kunifanya nikose amani ya moyo na imani katika uongozi niliopo ndani yake sasa.
Matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM) – hususan katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama ambao kwa kila awamu huwa msingi wa kukihuisha Chama na fursa ya kufanya Mageuzi ambayo kwa pamoja hukipa chama sura ng’aavu mbele ya umma kabla ya uchaguzi; desturi hii ya kufanya mageuzi ndani ya chama imekuwa nguzo muhimu ya ukubalifu na ushindi wa CCM mbele ya umma.
Imekuwepo kauli maarufu ya CCM isemayo “Chama kwanza mtu baadaye”, mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa ni maslahi ya nani yanapiganiwa wakati huu, mtu, kikundi au Chama Taasisi?
Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini.
Nitaendelea kuwa mwana CCM wa kawaida, mzalendo na raia mwaminifu kwa Taifa na nchi yetu.
Ninamwamini Mungu wa Mbinguni na ninahamasika na tumaini kuu kwamba siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa miiko na nidhamu ya uongozi, dhamira njema, siasa safi, uongozi bora na hofu ya Mungu.
Mheshimiwa Rais, nakushukuru kwa fursa uliyonipa, naamini historia itatoa tafsiri sahihi ya hatua hii.
Kwa heshima kubwa,
Humphrey Hesron Polepole.
NAKALA KWA:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
KIAMBATANISHO CHA BARUA YA POLEPOLE