China na nchi za Afrika zinaendelea kufurahia ushirikiano na urafiki wao wa kudumu ambao uliwekewa jiwe la msingi na mwasisi wa China Mwenyekiti Mao Zedong na viongozi wengine waasisi wa Afrika.
Katika kipindi chote cha zaidi ya miongo sita China na Afrika siku zote zimekuwa zikiheshimiana, zikithaminiana, zikiungana mkono na zaidi ya yote zimekuwa zikihitajiana kwa kila hali.
Watu wa China na Afrika wamekuwa pamoja kwa shida na raha na kuambatana bega kwa bega huku wakifuata njia ya kipekee ya ushirikiano wa kunufaishana ambao umezaa ‘Pendekezo la Ukanda Mmoja Njia Moja’ na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Katika Mkutano wa kilele wa FOCAC wa mwaka 2024 uliomalizika hivi karibu hapa Beijing, pande hizo mbili ziliamua kujenga jumuiya yenye nguvu zaidi kati ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja wa hali zote na kuongoza uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika katika zama mpya.
Akielezea umuhimu wa mkutano wa FOCAC wa Beijing kwa mahusiano ya China na Afrika, mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Afrika nchini China, Rahmat Allah Mohamed Osman, anasema anaamini kuwa China na Afrika zina mahitaji ya kunufaishana, na kueleza matumaini yake juu ya utekelezaji wa sera nyingi zaidi za China katika kuunga mkono masuala ya kilimo, viwanda na kukuza ujuzi wa watu wa Afrika.
Soma Pia: China inapanua uwekezaji Afrika huku Marekani ikiizuia kuongeza uwezo wake wa uzalishaji
Mwaka 2023, China ilizindua Mpango wa Kusaidia Maendeleo ya Viwanda barani Afrika, ikitekeleza mpango wa China wa kusaidia kuboresha kilimo barani Afrika na pia kuzindua Mpango wa Ushirikiano kati ya China na Afrika wa kuwandaa watu wenye ujuzi chini ya mfumo wa FOCAC, ili kusaidia maendeleo na ustawi wa Afrika.
Kupitia mipango hii, ushirikiano kati ya China na Afrika utaendeleza utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Afrika yaani "Ajenda 2063" na kuharakisha ukuaji wa viwanda barani Afrika.
Kwa mujibu wa Osman, mipango hii inashughulikia maeneo ambayo yanahitaji uharaka zaidi, kwenye juhudi za kuleta usasa barani Afrika na pia itasaidia nchi za Afrika kuongeza uwezo wao wa maendeleo. Hakuna asiyefahamu kuwa nchi za Afrika zina faida kubwa ya idadi ya watu, wakati huohuo pia zikiwa na idadi kubwa ya vijana, kwa maana hiyo China inaposhirikiana na Afrika kukuza watu wenye ujuzi itasaidia pakubwa kuibua wataalamu katika nyanja mbalimbali barani Afrika.
Zikiwa zinahitajiana zaidi hasa katika wakati huu ambao dunia inaendelea kuwa na mabadiliko ya kasi, ni matarajio ya kila mtu kwamba China na Afrika zitabeba jukumu muhimu zaidi. Kwa upande mmoja, ikiwa inahitaji ujuzi na uwekezaji kutoka China, Afrika itaendelea kunufaika na ujenzi wa miundombinu, kuongeza watu wenye ujuzi, kupata nishati na mfumo wa uwekezaji thabiti ili kuendeleza muundo wa biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kwa upande mwingine, kadiri uchumi wa China unavyoendelea kukua zaidi, utakuwa na uwezo zaidi wa kutoa idadi kubwa ya vijana wenye ujuzi barani Afrika na uwezo wa uzalishaji.
Suala hili linaendana vizuri na matarajio ya Afrika ya kuongeza uzalishaji wa viwanda na biashara ndani ya Afrika kupitia Jumuiya ya Biashara Huria ya Bara la Afrika.
Osman alibainisha kuwa China na Afrika zinapiga hatua kubwa katika kuimarisha biashara ya pande mbili. Maua na maparachichi ya Kenya hivi sasa yanapatikana kwa wingi kwenye soko la China, na kahawa ya Ethiopia na Rwanda inafurahiwa na watumiaji wa China. Hata hivyo amesema biashara kati ya China na nchi za Afrika bado ina uwezo mkubwa wa kukua.
Juu ya yote hayo Bw. Osman anakosoa kauli ya nchi za Magharibi ya kwamba China inajihusisha na ukoloni mamboleo barani Afrika. Ni wazi kwamba China na nchi za Afrika zimekuwa na mambo mengi wanayofuatilia kwa pamoja, wakati huohuo China ikisikiliza sauti ya nchi za Afrika kila mara na kuiunga mkono thabiti.
Tukirejea kwenye historia tunaona kuwa wakoloni wa Magharibi walipora rasilimali za Afrika na kuonesha kutojali ujenzi wa ndani na maendeleo barani Afrika. Kwa hiyo kauli kama hizi za China kujihusisha na ukoloni mamboleo barani Afrika ni za kuchekesha na ni za watu waliofilisika kimawazo.