China na Tanzania mwaka huu wa 2024 zinaadhimisha miaka 60 tangu zianzishe uhusiano wa kidiplomasia. Kupitia maadhimisho haya nchi hizi mbili sasa zinatarajia kupanua uhusiano wao wa kiutamaduni na kiutalii na kuimarisha mawasiliano kati ya watu wa pande mbili katika sekta mbalimbali.
Hivi majuzi ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Tanzania walikuja Beijing kwenye uzinduzi wa Mwaka wa Utamaduni na Utalii kati ya China na Tanzania ili kusherehekea maadhimisho hayo yaliyofanyika Jumatano ya Mei 15, katika Jumba la Taifa la Opera la China mjini Beijing. Uzinduzi huo pia ulishuhudia nchi zote mbili zikionesha utamaduni wao adhimu.
Wakati wa hafla hiyo, filamu ya dakika 25 iliyopewa jina la “Amazing Tanzania” ilioneshwa kwa mara ya kwanza, ikilenga kutangaza rasilimali za utalii wa Tanzania kwa watazamaji wa China. Chini ya uongozaji wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi, mwigizaji maarufu wa China Jin Dong alianza safari ya kuvutia ya kuchunguza vivutio mbalimbali vya Tanzania. Safari hiyo ilijumuisha Kisiwa cha marashi ya karafuu cha Zanzibar, mlima mrefu zaidi barani Afrika Kilimanjaro na wanyamapori waliosheheni katika Mbuga ya Taifa ya Serengeti.
Mbali na filamu hii fupi ya kutangaza rasilimali za utalii wa Tanzania, katika sherehe za uzinduzi wa Mwaka wa Utamaduni na Utalii kati ya China na Tanzania, pia lilifanyika tamasha murua la muziki wa kitamaduni, ngoma na sarakasi pamoja na muziki wa China. Wasanii mbalimbali kutoka Tanzania na China walitumbuiza na kufanya sherehe hizi kufana mno, huku viongozi kadhaa wakiwemo mawaziri wakishindwa kujizuia na kuinuka kucheza pamoja na wasanii hawa.
Baada ya sherehe hizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba, walikutana na kujadili kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika siku zijazo, huku wakitangaza zama mpya ya uhusiano wa kidiplomasia wenye lengo la kujenga dunia bora, iliyoendelea na salama.
Katika mazungumzo yao waziri Wang aliisifu Tanzania kwa urafiki wake thabiti katika miongo sita iliyopita, akisema, nchi hii imejidhihidirisha kuwa rafiki wa kweli katika shida na raha.
“Tanzania imekuwa rafiki wa China siku zote. Kwa China, miaka 60 ina maana kubwa katika uhusiano. Hatua inayofuata baada ya hii ni kuendeleza uhusiano huu katika enzi mpya ya kujenga dunia yenye mafanikio, haki na salama kwa watu wote,” alisema Wang.
China na Tanzania zimekuwa zikiungana mkono kwa muda mrefu katika masuala yanayohusu maslahi yao ya pamoja, kwa maana hiyo kupitia maadhimisho haya ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, ni matarajio ya kila mtu kwamba ushirikiano huu utapanuka zaidi katika maeneo muhimu kama vile biashara, miundombinu, usindikaji na utengenezaji, uchumi wa kidijitali, uchumi wa bluu na nishati.
Katika kuonesha kwamba China ipo bega kwa bega na Tanzania, waziri Wang alitangaza mchango wa China wa dola 500,000 za kimarekani (sawa na shilingi bilioni 1.3b) kwa ajili ya kusaidia wahanga wa mafuriko yaliyotokea hivi karibuni nchini Tanzania, ambapo waziri Makamba alimshukuru mwenzake Wang akisema huu ni ushahidi tosha wa urafiki kati ya nchi mbili.
Kabla ya shamrashamra za maadhimisho yaliyofanyika hivi majuzi mjini Beijing, maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania yalisherehekewa na kupata mapokezi maalum huko jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, huku Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania ambaye pia alikuwepo kwenye maadhimisho ya Beijing, Angellah Kairuki alisisitiza kuwa China na Tanzania zimefurahia ushirikiano wa miongo sita tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1964 na kusema Tanzania sasa inajikita zaidi katika kuimarisha ushirikiano wake na China.
"Tunatarajia miaka mingi zaidi ijayo tutaendelea kuwa na ushirikiano imara na wa karibu, hasa katika diplomasia, lakini pia mawasiliano baina ya watu wa pande mbili katika biashara, uwekezaji, elimu, utalii, na maendeleo ya kiuchumi.” Alisema waziri Kairuki