Chombo cha “Shenzhou” No.12 cha China hivi karibuni kilifanikiwa kuwapeleka wanaanga watatu kwenye anga ya juu. Baada ya kuunganisha chombo hicho na behewa la Tianhe lililorushwa angani mapema, wanaanga hao waliingia kwenye behewa hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa Wachina kuingia kwenye kituo cha anga ya juu, ikimaanisha kuwa China imefungua ukurasa mpya katika shughuli za safari ya anga ya juu.
China imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya anga za juu tangu ianzishe mradi wa kupeleka watu kwenye anga za juu. Licha ya kurusha Chombo cha “Shenzhou” No.12, katika miaka ya hivi karibuni, China imefanikisha kazi nyingi za kuchunguza anga za juu, ikiwemo “Chang’e” No. 4 kutua nyuma ya Mwezi, “Chang’e” NO. 5 kuchukua sampuli Mwezini na kurudi duniani, na “Tianwen” No. 1 kutua kwenye sayari ya Mars na kutuma picha za sayari hiyo duniani. Katika safari hii, wanaanga watatu wa China watakuwa angani kwa miezi mitatu, na kufanya kazi mbalimbali, zikiwemo kutembea nje ya behewa, na kufanya majaribio ya sayansi na teknolojia, ili kufanya maandalizi kwa kukamilisha ujenzi wa kituo cha China kwenye anga ya juu.
China imepata mafanikio hayo katika shughuli za anga za juu wakati imewekewa vizuizi vya teknolojia na nchi za magharibi haswa Marekani. Mwaka 1998, chini ya uongozi wa Marekani na Russia, nchi 16 zilianzisha Kituo cha Kimataifa cha Anga ya Juu. Mradi huo wa ushirikiano wa kimataifa uliikataa China, ambaye ni nchi ya tatu duniani kwa uwezo wa teknolojia ya anga za juu. Ili kuzuia zaidi maendeleo ya shughuli za anga za juu ya China, Marekani ilipitisha sheria ya Wolfe, na kupiga marufuku kufanya ushirikiano na mawasiliano na China katika shughuli za anga za juu. Hali hii iliilazimisha China kuendeleza teknolojia ya anga za juu kwa kujitegemea. Hadi sasa China imepata mafanikio makubwa, na itakamilisha kituo chake cha anga ya juu mwakani, na itakapofika mwaka 2030, kituo hicho kinatarajiwa kuwa kituo pekee angani.
Kinyume na Marekani na nchi nyingine za magharibi zilivyofanya, China inapenda kushirikiana na nchi nyingine katika utafiti wa teknolojia za anga za juu. Msaidizi wa mkurugenzi wa ofisi ya mradi wa kupeleka wanaanga kwenye anga za juu ya China Ji Qiming amesema, anga za juu si mali ya nchi yoyote, na kutafiti anga za juu ni shughuli za pamoja za binadamu wote. Amesisitiza kuwa China siku zote inafuata kanuni ya kutumia anga za juu kwa njia ya amani, usawa, na kunufaishana ili kupata mafanikio ya pamoja. Pia amesema, China inakupenda kufanya ushirikiano na mawasiliano na nchi yoyote inayotaka kutumia anga za juu kwa njia ya amani. Ameongeza kuwa kituo cha China kwenye anga ya juu kitakuwa jukwaa mpya la ushirikiano wa kimataifa.
Takwimu zinaonesha kuwa, hadi sasa nchi 27 zimeiomba China kuwaruhusu wanaanga wao kuingia kwenye kituo hicho. Idara ya safari ya anga za juu ya Ulaya imetuma wanaanga wao kufanya mazoezi nchini China, na baadhi yao wameanza kujifunza lugha ya Kichina.