Na Caroline Nassoro
Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC utafanyika tarehe 16 Oktoba hapa Beijing. Lakini kabla ya kufanyika kwa Mkutano huo, ikiwa sasa watu wa China wanakuwa katika mapumziko ya siku saba ya kusherehekea miaka 73 ya kuzaliwa kwa taifa la China, siku ya taifa inayoangukia tarehe mosi, Oktoba, tuangazie mafanikio ambayo China imeyapata katika miaka hii 10 tangu Xi Jinping achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, leo hii tukiangazia suala la ujenzi wa miundombinu. Leo tutaangazia suala zima la maendeleo makubwa ambayo China imepata katika sekta ya sayansi na teknolojia.
Pamoja na umuhimu mkubwa wa elimu, sayansi na teknolojia pia inachukua nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi yoyote. China, ikiwa nchi kubwa inayoendelea, imepata mafanikio makubwa katika sekta hii, ikiwa ni pamoja na uvumbuzi.
Mwezi Oktoba mwaka 2021, rais Xi Jinping alitoa wito kwa wanasayansi na wanateknolojia nchini humo kujitahidi zaidi ili kuijenga China kuwa nchi yenye nguvu katika sekta ya sayansi na teknolojia. Rais Xi alisema, wakati China ikianza safari mpya ya kujenga nchi ya kijamaa ya kisasa katika nyanja zote, uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia utakuwa na nafasi muhimu katika kukuza maendeleo ya jumla ya nchi hiyo.
Katika kuhakikisha China inapata maendeleo makubwa katika sekta ya sayansi na teknolojia, China inatumia uvumbuzi wa kipekee wa kuzalisha mbegu za aina mbalimbali za vyakula katika anga za juu.
Mwaka 1990, wanasayansi wa China walitangaza zao la kwanza lililopandwa angani, ambalo ni aina ya pilipili hoho iitwayo Yujiao 1. Liu Luxiang, mtaalamu wa mabadiliko ya anga ya juu wa China na mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Mutagenesis anasema kwamba, ikilinganishwa na aina za kawaida za pilipili hoho zinazokuzwa nchini China, Yujiao 1 huzalisha matunda makubwa zaidi na ni sugu kwa magonjwa.
Maendeleo makubwa ya China katika sekta hii ya anga za juu katika miongo ya hivi karibuni yameiwezesha nchi hiyo kupanda maelfu ya mbegu kwenye anga za juu. Mwaka 2006, China ilifanikiwa kupanda zaidi ya kilo 250 za mbegu na vijidudu kutoka kwa spishi 152 kwenye satelaiti ya Shijian 8. Na mwezi Mei mwaka huu, mbegu 12,000 ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za nyasi, shayiri na alfalfa zilirudi kutoka katika ziara ya miezi sita kwenye kituo cha anga za juu cha China cha Tianhe kama sehemu ya jukumu la chombo cha Shenzhou 13.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Serikali la China, ilitoa mwongozo utakaowezesha kuongeza uelewa wa sayansi na uvumbuzi kwa umma. Mwongozo huo umeeleza ulazima wa kutoa umuhimu sawa kwa kuwezesha uvumbuzi wa kisayansi kwa umma, na uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, itakapofika mwaka 2025, huduma za umma kwa ajili ya uelewa wa sayansi zitaongezeka kidhahiri, na watafiti wengi watachukua nafasi halisi katika kueneza elimu ya sayansi, na kiwango cha watu watakaokuwa na ufahamu kuhusu masuala ya kisayansi kitazidi asilimia 15, na mazingira ya kijamii yanayothamini sayansi na uvumbuzi yataanzishwa.
Kwa ufupi, katika miaka 10 iliyopita, China imepata mafanikio makubwa katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi, na kuifanya kuwa ni nchi yenye nguvu kubwa ya sayansi na teknolojia. Pia kutokana na mwongozo huo uliotolewa hivi karibuni, ni wazi kuwa, katika miaka kumi ijayo, China itakuwa ni nchi inayoongoza katika sekta ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi.