Mwaka wa 2015, nchi zote duniani zilifikia makubaliano kwenye mkataba wa Paris kuhakikisha kuwa juhudi zinafanywa na nchi zote duniani kudhibiti ongezeko la joto duniani kuwa chini ya nyuzi 1.5 sentigredi, na kutaka nchi zote kuhamasisha raslimali kufanikisha jambo hilo. Baadhi ya nchi zimefanya juhudi na kuendelea kutekeleza jambo hilo, lakini nchi nyingine bad hazijachukua hatua za maana.
Takwimu nyingine zilizotolewa na taasisi ya utafiti wa mambo ya nishati ya Global Energy Monitor (GEM), unaonesha kuwa mwaka huu wa 2024 China inakaribia kufikia uwezo wa uzalishaji wa GW1,200 za umeme wa nishati ya jua na upepo, miaka sita kabla ya lengo lililowekwa na serikali. Ripoti pia imeonesha kuwa uwezo wa China uko mbele ya nchi zote duniani kwenye miradi ya uzalishaji wa nishati endelevu ambayo inafanya kazi, ambayo inaendelea kujengwa na ambayo inapangwa kujengwa.
Hali halisi ya sasa pia inaonesha kuwa juhudi za China hazijaishia ndani tu, kwani bidhaa nyingi za uzalishaji wa umeme kwa nishati za jua na upepo, na hata vifaa vya matumizi ya nishati ya jua na upepo vinavyouzwa katika sehemu mbalimbali duniani, vingi vinatoka China. China pia iko mstari wa mbele kwenye kushirikiana na nchi nyingine nyingi za dunia ya tatu kwenye ujenzi wa kandarasi za kuzalisha nishati mpya na nishati safi, iwe ni umeme unaotokana na nishati ya maji (Hydroelectric power) au umeme unaotokana na joto la ardhini (Geothermal energy).
Cha ajabu ni kwamba, baadhi ya wanasiasa wa nchi za magharibi badala ya kuunga mkono mchango wa China, wamekuwa wakitumia hali hiyo kama njia ya kuishambulia China kwa kisingizio kuwa “China inatumia uwezo wa uzalishaji kupita kiasi” kujaza bidhaa hizo kwenye soko la dunia. Ukweli ni kwamba China isipotumia uwezo wake kwenye kuuza bidhaa za nishati safi duniani, nchi zinazoikosoa China hazitauza bidhaa hizo, na kufanya kuwe na uhaba wa bidhaa hizo kwenye soko la dunia, na pia kuleta ombwe kwenye juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Jambo la muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa nchi zote duniani zinashirikiana kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, badala ya kutumia suala hili kama jukwaa kisiasa kwa wanasiasa wa nchi za magharibi.